Saturday, June 14, 2014

AICC kukuza soko la utalii wa mikutano nchini

::
Na Mwandishi wetu
14th June 2014
Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC)
Mipango ya ujenzi wa Kituo cha Kimataifa cha Mount Kilimanjaro Conversion (MKICC) jijini hapa, kitakachogharimu Dola za Marekani milioni 300 imekamilika na ujenzi wake unatarajiwa kuanza hivi karibuni.

Kukamilika kwa kituo hicho kinachomilikiwa na Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC), kutasaidia kukuza soko la utalii wa mikutano nchini.

Mkurugenzi Mtendaji wa AICC, Elishilia Kaaya, alisema hayo jana wakati akizungumza na wajumbe wa bodi ya kituo hicho waliofanya ziara maalum kukagua miradi pamoja na vitega uchumi mbalimbali vya kituo hicho jijini hapa.

Kaaya alisema mipango ya ujenzi wa kituo hicho imeshakamilika ikiwamo kupata kibali kutoka serikalini pamoja na fedha za ujenzi. Alisema tayari kazi ya usanifu wa mradi huo imeshafanyika na sasa wanatarajia kumpata mzabuni wa ujenzi.

AICC inamiliki pia Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Mwalimu Nyerere kilichopo jijini Dar es Salaam.
Naye Makamu Mwenyekiti wa bodi hiyo, Abdul Mshangama, aliutaka uongozi wa kituo hicho kujikita katika ujenzi wa vituo hivyo vya mikutano kutokana na soko kubwa lililopo hapa nchini.

Alisema kwa sasa Tanzania bado haina kituo kikubwa chenye uwezo wa namna hiyo zaidi ya kile cha Dar es Salaam ambacho hata hivyo bado hakina uwezo wa kutosha kupokea kiasi kikubwa cha wageni na hata vifaa.

Naye mjumbe wa bodi hiyo, Dk. Khamis Kigwangala, aliushauri uongozi wa kituo hicho kufanya ujenzi wa hospitali za kisasa katika maeneo yaliyo wazi wanayoyamiliki kwakuwa kituo hicho hakipaswi kujikita tu katika utalii wa mikutano bali hata huduma za afya.

Alitaka kituo hicho kutambua utajiri wa rasilimali ardhi inayomilikiwa nacho hivyo kuitumia vyema kwa kuwekeza vitega uchumi hata ikibidi kwa kuingia ubia na wadau wa maendeleo katika sekta mbalimbali katika kujipanua zaidi.

Pia wajumbe walitembelea kuona ujenzi wa majengo mawili pacha yanayokamilika ujenzi wake ya nyumba za kuishi yenye jumla ya nyumba 32 za kuishi zenye vyumba vitatu vya kulala ambapo kila nyumba moja itakodishwa kwa kiasi cha dola 600 kila moja. 
CHANZO: NIPASHE
http://www.ripoti.com/openx/www/delivery/lg.php?bannerid=647&campaignid=424&zoneid=267&loc=1&referer=http%3A%2F%2Fwww.ippmedia.com%2Ffrontend%2Findex.php%3Fl%3D68900&cb=2ff1602a70

No comments:

Post a Comment