Saturday, September 26, 2015

Rais Kikwete: Tanzania itaendelea kupambana na ujangili




Na Mwandishi maalum
26th September 2015
 
Rais Jakaya Kikwete
Rais  Jakaya Kikwete ameeleza changamoto kubwa zinazozuia kukua  haraka kwa sekta ya utalii katika Afrika na kushindwa kuchuma matunda  ni kutotangazwa sahihi kwa sekta hiyo katika bara hilo.

Alisema pamoja na kuwa na vivutio vingi vya utalii, Bara la Afrika,  bado linabakia nyuma kwa kiasi kikubwa katika kuvutia watalii wa  kimataifa na mapato yanayotokana na utalii. Alisema Tanzania  itaendelea kutenga eneo kubwa la ardhi yake kwa ajili ya hifadhi na  pia kukabiliana na ujangili dhidi ya tembo, ambao hata hivyo amesema  umepungua katika mwaka uliopita.

Aliyasema hayo juzi wakati alipotoa hotuba ya ufunguzi wa shughuli za  miaka 10 ya chama cha Usafiri cha Afrika (ATA) na miaka 10 ya Jukwaa  la Rais Kuhusu Utalii ñ Presidential Forum on Tourism kwenye Kituo  cha Kimmel cha Chuo Kikuu cha New York (New York University Kimmel  Center) Africa House, mjini New York.

Rais Kikwete alitumia mkutano huo pia kuaga jukwaa hilo akiwa kama  Rais wa Tanzania. Kwa mujibu wa Katiba, Oktoba 25 itakuwa mwisho wa  kipindi chake cha pili. 

Rais Kikwete anahudhuria shughuli za mwaka huu za Baraza Kuu la Umoja  wa Mataifa (UNGA) baada ya kumaliza kuendesha vikao vya Jopo la Watu  Mashuhuri Duniani ambao wanatafuta jinsi gani dunia inavyoweza  kujiandaa vizuri zaidi kukabiliana na magonjwa ya mlipuko, jijini  hapa.

Rais Kikwete ametambulishwa na kukaribishwa kutoa hotuba yake na Dk.  Yaw Nyarko, Raia wa Ghana na Mkurugenzi wa Africa House ambaye pia ni  Profesa wa uchumi kwenye Chuo Kikuu cha New York na Edward Bergman,  Mkurugenzi Mtendaji Mwanzilishi wa ATA.

Rais Kikwete na familia ya Bergman ya New York, walianzisha na  kujadili wazo la  kuanzishwa kwa chama hicho miaka 10 iliyopita.

Mawaziri waliozungumza kwenye shughuli hiyo iliyoendeshwa na Peter  Greenberg, Mhariri wa Usafiri wa Televisheni ya CBS ni Lazaro  Nyalandu wa Tanzania,  Dk. Maria Mutagamba, Waziri wa Utalii,  Wanyamapori na Nyaraka wa Uganda ambaye pia ni Rais wa ATA na NíDiaye  Ramatoulaye Diallo, Waziri wa Utamaduni, Utalii na Usanii wa Vinyango  wa Mali.

Mawaziri wengine ni Phylis Kandie wa Masuala ya Afrika Mashariki,  Biashara na Utalii wa Kenya na Pohamba Shifeta wa Mazingira na Utalii  wa Jamhuri ya Namibia.

Rais Kikwete alisema: Changamoto kuu zinazokabili maendeleo ya utalii  katika Afrika ni miundombinu ya kitalii, utangazaji wa masoko ya  utalii na matatizo ya usafiri wa anga kuingia na kutoka Afrika.

Lakini pia kuna jambo kubwa la mtazamo hasi kuhusu Afrika. Kwa  kawaida, vyombo vya habari vya nje vinalielezea Bara la Afrika kama  Bara hatari ambalo sifa zake kuu ni migogoro, magonjwa na matatizo  yanayotokana na umasikini.

Alitaka ukweli kuhusu Afrika uelezwe kwa usahihi na waafrika wenyewe.
Alisema picha inayojengwa ni kuwa tatizo la nchi moja ni tatizo la  bara zima kitu ambacho si cha kweli. 
Alisema upotoshaji huo umesababisha watu kufuta safari za kitalii  kwenda Afrika wakati ugonjwa wa ebola ulipolipuka nchi za Guinea,  Liberia na Sierra Leone. 
CHANZO: NIPASHE
http://www.ripoti.com/openx/www/delivery/lg.php?bannerid=647&campaignid=424&zoneid=267&loc=http%3A%2F%2Fwww.ippmedia.com%2F%3Fl%3D84690&referer=http%3A%2F%2Fwww.ippmedia.com%2F%3Fm%3D54%26lang%3DSW&cb=67018f5d6d
Habari Zaidi