Thursday, October 31, 2013

Migogoro ya wafugaji yatikisa Bunge

 chanzo-Tanzania daima

WABUNGE wawili jana walitaka Bunge liahirishe shughuli zake ili lijadili migogoro kati ya wafugaji inayoendelea nchini pamoja na malalamiko kuhusu Operesheni Tokomeza Ufugaji Haramu na Operesheni Tokomeza Ujangili.
Wabunge hao; Said Nkumba (Sikonge) na Kangi Lugola (Mwibara) walitaka wabunge wajadili jambo la dharura kuhusu migogoro ya wafugaji inayoendelea nchini.
Mbali na migogoro hiyo walitaka pia operesheni hizo zijadiliwe na wabunge kwa kuwa kwa sasa zinatumika kuwanyanyasa wafugaji na hali inayotishia machafuko kutokea nchini.
Alianza kusimama Nkumba baada ya kumalizika kwa kipindi cha maswali na majibu na kunukuu kanuni ya 47 (1, 2, 3) akitaka shughuli za Bunge zilizopangwa jana ziahirishwe, ili kujadili jambo hilo la dharura kuhusu migogoro ya wafugaji.
Alisema kwa sasa ipo migogoro ya aina tatu ambayo ni kati ya wafugaji na wakulima, wafugaji na wawekezaji na wafugaji na wahifadhi.
“Tatizo hili limekuwa kubwa kiasi cha kutishia uvunjifu wa amani hasa katika mikoa ya Mbeya, Morogoro na Pwani.
“Na zaidi operesheni mbalimbali zinazoendelea kwa sasa zimesababisha uhasama na athari kubwa kwa wakulima na wafugaji kutokana na kupoteza mali zao, mifugo kuuawa na kupotea na vifo vya watu,” alisema.
Kwa upande wake, Lugola ambaye naye alilitaka Bunge kujadili migogoro hiyo, alisema hali ya wafugaji kwa sasa ni mbaya kutokana na operesheni hizo.
“Hivi ninavyozungumza ng’ombe 4,000 wamekamatwa kwa nguvu huko Kaliua na tayari ng’ombe 12 wameshachambuliwa kwa ajili ya kupigwa risasi kuwashinikiza wafugaji  walipe sh 180,000 kwa kila ng’ombe.
“Tusipojadili jambo hili mnada utaendeshwa na ng’ombe 4,000 watauzwa, ng’ombe wengine wanatumbukizwa kwenye madimbwi. Tatizo hili lisiposhughulikiwa litaleta machafuko makubwa hasa pembezoni mwa Serengeti,” alisema.
Hoja za wabunge wote hao ziliungwa mkono na wabunge.
Hata hivyo, Spika wa Bunge, Anne Makinda, alisema kikanuni hoja hizo hazitakiwi kuungwa mkono.
“Hoja zote ni nzito haziwezi kudharauliwa, naiagiza serikali ikafanyie kazi jambo hili na ilete taarifa bungeni katika mkutano huu,” alisema.


Mawaziri wajadili mgogoro wa wakulima, wafugaji



Na Sharon Sauwa, Mwananchi

Posted  Alhamisi,Oktoba31  2013  
Kwa ufupi
Alisema wafugaji hao wamekuwa wakitozwa faini kubwa na kujeruhiwa katika operesheni hiyo ambayo imekuwa haina masilahi kwa wafugaji.

Dodoma. Mawaziri watano wamekutana mjini hapa kujadili malalamiko ya wafugaji kuhusiana na operesheni tokomeza inayolenga kupambana na majangili.

Mawaziri hao ni Mambo ya Ndani, Maliasili na Utalii, Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi na Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa. Hayo yalisemwa jana na Katibu Mkuu wa CCM, Abdurhaman Kinana, alipokuwa akizungumza na wawakilishi wa wafugaji.

“Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete alikutana na wawakilishi wa wafugaji kutoka katika mikoa ya Simiyu na Shinyanga, “alisema. Wafugaji hao walifika kwa Kinana ili awaite mawaziri wanaohusika waweze kuwaeleza malalamiko yao na kuyatafutia ufumbuzi.

Awali, Mbunge wa Maswa Magharibi, John Shibuda (Chadema), alisema wafugaji wamekuwa wakinyanyaswa katika operesheni hiyo.

“Naomba uwaambie Wabunge wa CCM waisisitize Serikali kusitisha operesheni hii ambayo imekuwa ikitokomeza mifugo na maisha ya wafugaji,”alisema Kinana.

Alisema wafugaji hao wamekuwa wakitozwa faini kubwa na kujeruhiwa katika operesheni hiyo ambayo imekuwa haina masilahi kwa wafugaji.

Akizungumza katika kikao hicho, Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi alisema wakati Serikali ikiendelea kuchukua hatua za kuondoa malalamiko hayo, wafugaji wahakikishe kuwa hawachungi katika mashamba ya wakulima.



TAHARIRI-TANZANIA DAIMA -Watawala wanawalinda majangili




JANA vyombo mbalimbali vya habari hapa nchini viliandika kuhusu madai ya wabunge kutaka kuwafichua mapapa wa ujangili.
Madai hayo yaliibuliwa siku ya kwanza ya mkutano wa 13 wa Bunge unaoendelea sasa mjini Dodoma baada ya Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola (CCM), kuituhumu serikali kwa kutoa hoja nyepesi bungeni.
Mbunge huyo alikuwa akitaka kujua hatua iliyofikiwa na serikali kwenye uendeshaji wa Operesheni Tokomeza Ujangili inayofanyika kwenye mbuga zote nchini.
Mbunge alilaani namna operesheni hiyo inavyoendeshwa kwa kukiuka haki za binadamu kwa sababu watu wasio majangili wanakamatwa, kuteswa na kuharibiwa mali zao ilhali majangili wanaojulikana wakiachwa waendelee na uhalifu wao.
Wakati mbunge huyo akilalama, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha, aliwatuhumu wabunge na wanasiasa wengine kwa kuingilia utendaji wa operesheni hiyo kwa kuwatetea wanaokamatwa kwa tuhuma za ujangili.
Kauli ya Waziri Nahodha, ililenga kumpiga kijembe Waziri mwenzie wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, ambaye hivi karibuni, msaidizi wake (ofisi ya ubunge) alikamatwa mkoani Iringa kwa tuhuma za ujangili.
Hoja ya Lugola ni kuitaka serikali kuhakikisha wanakata mizizi ya ujangili kwa kuwa biashara hiyo inafanywa na matajiri wakubwa wenye ushawishi kwa watawala ndani na nje ya nchi.
Tunaunga mkono hoja hiyo kwa maana ya kuitaka serikali kuacha kukamata ‘vidagaa’ wa ujangili huku ‘mapapa’ yakifumbiwa macho.
Tanzania Daima tunafahamu kwamba ujangili, hasa wa tembo na bidhaa zake unatishia ustawi wa wanyama hao.
Takwimu zinaonyesha kwamba kila siku tembo 30 wanauawa kwenye hifadhi mbalimbali nchini. Hiyo ni dalili kwamba katika kipindi cha miaka isiyozidi 10 Tanzania itakuwa na hifadhi zisizo na tembo.
Katika hili tunaitaka serikali kuchukua hatua makini bila kutizamana machoni, licha ya ukweli kwamba utekelezaji wa operesheni hiyo utawaacha wahusika, sababu ni biashara inayofanywa na matajiri wakubwa wenye uswahiba na watawala.
Tunaishangaa serikali kwa kuendelea kuwaacha kazini makamanda wa polisi wanaopakana na hifadhi mbalimbali. Hao lazima wawe watuhumiwa wa kwanza wa ujangili kabla ya kwenda kuwakamata wanavijiji wanaoingia mbugani kutafuta kitoweo.
Mara kadhaa makamanda hao wamehusishwa ama wakiwalinda majangili na kuwavusha mipakani au kwa kutumia magari ya serikali kufanya uwindaji haramu.
Si hivyo tu, makamanda hao wanatuhumiwa pia kuvuruga ushahidi na wakati mwingine kuwatorosha watuhumiwa wa ujangili jambo linalokwamisha utendaji wa mahakimu wanaosikiliza kesi za ujangili.
Kuwakamata makamanda hao inashindikana kwa sababu waliowaweka ndiyo wanaowatuma kuwalinda majangili wanaoua wanyamapori wetu.
Dhamira ya kweli ikiwepo, ikasukumwa na utashi wa kisiasa kisha wananchi wakaelezwa athari za kuua wananyama pori hao, tunaamini mitaji ya mapapa wa ujangili itapungua kwa kiasi kikubwa.

chambuzi- Operesheni dhidi ya ujangili iungwe mkono




Na Mwananchi

Posted  Alhamisi,Oktoba31  2013  saa 24:0 AM
Kwa ufupi
Ni kweli, operesheni hiyo inatakiwa isiwe ya mateso, unyanyasaji, ukatili wala fursa ya ulipaji wa visasi, bali inatakiwa kuendeshwa kwa umakini, weledi na haki ili kuhakikisha kila mmoja anatendewa kadri ya matendo yake.
Kwa wiki kadhaa hapa nchini inaendeshwa operesheni ya kupambana na ujangili wa tembo na wanyama wengine chini ya kikosi maalumu kinachoundwa na maofisa kutoka katika vyombo vya dola, maarufu kwa jina la Operesheni Tokomeza.
Taarifa mbalimbali zimekuwa zikiripotiwa kuhusiana na utekelezaji wa majukumu ya kikosi hiki, ikiwamo watu mbalimbali kukamatwa wakidaiwa kuhusika na ujangili, hasa wa meno ya tembo, uhalifu ambao kwa siku za karibuni umeichafua sana nchi yetu kimataifa.
Watu mbalimbali wakiwamo viongozi wa umma na wa kisiasa wamekamatwa katika maeneo ya Serengeti, Ngorongoro, Arusha, Ruaha, Iringa, Mahenge, Maswa, Meatu na kwingineko ambako pia, ushahidi wa aina tofauti umepatikana kuhusiana na vitendo vya ujangili.
Kukamatwa kwa watuhumiwa katika maeneo yote hayo ni ushahidi kwamba majangili wana mtandao mpana unaotumia nguvu za kifedha, kisiasa au za ulinzi wa dola kujiimarisha katika maeneo mengi ya nchi, na kuendelea kuhujumu maliasili za taifa.
Hata hivyo, pamoja na lengo zuri la operesheni hiyo, yapo madai ya kikosi hicho kutumia mabavu na ukiukwaji wa haki za binadamu, ikiwamo kupiga watu ovyo, kujeruhi na hata kuua watu kadhaa wanaotuhumiwa kujihusisha na ujangili.
Pamoja na kwamba malalamiko dhidi ya operesheni hiyo yanatakiwa kushughulikiwa na ukiukwaji huo wa haki za binadamu kukomeshwa, madai hayo yanatakiwa kutazamwa kwa umakini kulingana na unyeti wa tukio na mazingira yake.
Ni kweli, operesheni hiyo inatakiwa isiwe ya mateso, unyanyasaji, ukatili wala fursa ya ulipaji wa visasi, bali inatakiwa kuendeshwa kwa umakini, weledi na haki ili kuhakikisha kila mmoja anatendewa kadri ya matendo yake.
Tunatambua kuwa operesheni yoyote inayowahusisha watu wazito inakuwa na changamoto na vikwazo vingi, hali inayowasukuma hata wabunge kuanza kushinikiza Serikali kutoa orodha ya vigogo wanaodaiwa kujihusisha na vitendo vya ujangili.
Kwa mujibu wa madai ya wabunge hao na taarifa za vyombo vya habari, biashara hiyo haramu inawahusisha baadhi ya wabunge, mawaziri, watumishi wa Serikali na maofisa katika vyombo vya dola.
Jeshi la Polisi limetajwa kuongoza miongoni mwa makundi manne ya majeshi, ambayo watumishi wake wamekamatwa wakijihusisha na ujangili katika matukio saba ya ujangili. Wengine ni kutoka Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na Magereza.
Mathalan, kwa jinsi tatizo hilo lilivyo kubwa, katika matukio ya karibuni yaliyohusisha maofisa wa vyombo vya dola, jumla ya meno ya tembo 686 yaliyotokana na kuuawa kwa tembo 343 yalikamatwa, na vipande vingine 447 vilipatikana.
Kwenye operesheni ya namna hii ambayo Serikali imekiri kuwapo fununu za wanasiasa kuwa miongoni mwa majangili, ni lazima kuwepo vikwazo na shinikizo la kuizuia au kukwamisha, kwa vitisho au malalamiko ya umma kutoka kila kona ili kuhakikisha operesheni husika haifanikiwi.
Kutokana na hali hiyo, tunaunga mkono kauli ya Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha aliyoitia juzi bungeni akiwataka wanasiasa kuacha kushikiza kwa kutumia nguvu zao za kisiasa, kusitishwa kwa operesheni hiyo kwa sababu yoyote, kwa kuwa tunaamini shughuli kama hii haiwezi kufanikiwa iwapo itaendeshwa kama lelemama.

Wednesday, October 30, 2013

ASKARI AKUTWA NA RISASI ,MAPANGA NA NYAMA PORI NYUMBANI



SIKU chache baada ya askari polisi wa idara ya upelelezi wilaya ya Serengeti wakiwa na raia wawili wakishirikiana kuuza jino la tembo,mmoja amekutwa na risasi,nyama mbichi ya pori na mapanga na sime nyumbani kwake.
Askari hao walikamatwa oktoba 25,mwaka huu majira ya usiku na kikosi cha oparesheni okoa maliasili kinachoongozwa na JWTZ baada ya kuweka mtego na kuwanasa kirahisi.
Upekuzi huo uliofanywa nyumbani kwa askari koplo Isaack na Sixbert na kushuhudiwa na maafisa wa polisi walikuta risasi 7 za bunduki aina ya SMG na SRA ,nyama mbichi ya porini kwenye ndoo ya mnyama anayedhaniwa kuwa nyumbu,mapanga 15 na visu 9 nyumbani kwa koplo Isaack.
Licha ya kubainika kuwepo kwa  Rco Mkoa wa Mara Mohammed kwenye upekuzi huo hata hivyo alipoulizwa kwa njia ya simu kushiriki upekuzi na nini kilibainika na inatoa ishara gani kwa idara yake alikana kuwa hakuwepo,”mimi sikuwepo huko Mugumu niko Musoma”alisema.
Alisema kuwa wao hawahusiki na operesheni hiyo,”kila wanachopata taarifa wanapeleka Dar es Salaam…sisi huku kama kuna information  kwa ajili ya kufanyia kazi tunawapa …nao wakituhitaji wanasema …tunashirikiana kwa karibu
Kukamatwa kwa vitu hivyo  kwa askari huyo kumezidi kuibua maswali na hofu kutoka kwa raia huku ikitiliwa shaka kuwa mtandao huo ni mkubwa na huenda wakawa na silaha maalum inayotumiwa kwa ajili ya uwindaji wa wanyama pori  na matukio mengine.
Kamanda wa polisi Mkoa wa Mara Fernandi Mtui akiongea na Mwananchi kwa njia ya simu kuhusiana na upekuzi huo alikiri ulifanyika lakini hakushiriki katika zoezi hilo kwa kuwa operesheni hiyo inaundwa na askari mchanganyiko na wanakuwa na hati maalum za upekuzi.
“Ni kweli upekuzi umefanyika lakini sikuhusika…sijajua kwa undani nini kimekamatwa…maana kikosi hicho wapo askari wa kwetu,usalama wa taifa,wanyamapori na JWTZ na wana searc warrant(Hati ya upekuzi)…mimi nasubiri kama wamekutwa na kosa wataletwa kwangu”alisema kamanda.
Kamanda Mtui alisema kwa kuwa si msemaji wa operesheni hiyo bado anasubiri taarifa ya uchunguzi na kama watabainika kuwa na tuhuma watashitakiwa kijeshi kabla ya kushitakiwa kiraia,”hapo ndipo nitakuwa na nafasi ya kulizungumzia hilo…nasema kila kitu kitawekwa wazi…sitawanyima taarifa.
Oktoba  25 majira kati ya saa 4-5 usiku  mwaka huu askari wawili waliotajwa kwa  jina moja moja la Koplo Isaack na Sixbert wa idara ya upelelezi walikamatwa wakiwa na raia mmoja Samweli Chacha walikamatwa  wakijaribu kuuza jino la tembo katika eneo la Sedeco mjini Mugumu baada ya kuweka mtego maalum.
Askari hao wakiwa na gari aina ya Toyota Corolla yenye namba za usajiri T269 BRN mali ya askari Sixbert walifika eneo hilo na jino hilo kwa ajili ya kuuza wakiwa na raia wawili  mmoja anadaiwa kutoroka baada ya wenzao kukamatwa.
Baada ya kukamatwa kwa askari hao  walichukuliwa na kupelekwa eneo la Andajenga lililomo ndani ya hifadhi ya Taifa ya Serengeti ambako kikosi hicho kina kambi maalum.


Serikali: Migogoro ya Tanapa, wananchi imalizwe

MWENYEKITI WA KAMA YA KUDUMU YA BUNGE YA MALIASILI ARDHI NA MAZINGIRA JAMES LEMBELI.


KAMATI  ya  Kudumu ya Bunge ya Maliasili na Mazingira, imeitaka serikali kuhakikisha inashughulikia migogoro yote ya ardhi inayohusu Tanapa na wananchi.
Akizungumza hivi karibuni na waandishi wa habari kamati hiyo ilipofanya ziara jijini Mbeya, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, James Lembeli, alisema kuna migogoro  ya mipaka inayozikabili baadhi ya hifadhi za taifa nchini.

Akitolea mfano, Lembeli alisema hifadhi ya taifa ya Ruaha yenye eneo oevu la  Ihefu iliyoko mkoani hapa ilikumbwa na mgogoro huo baada ya Kkikao cha Maendeleo cha Mkoa (RCC), kushindwa kusimamia suala hilo kikamilifu.
Alisema  baada ya kujitokeza mgogoro huo serikali iliunda kamati mbalimbali kwa ajili ya kuchunguza na tayari umeshafanyiwa kazi.

Alisema kilichosababisha kuchelewa kutolewa kwa maamuzi ya kamati ni kesi zilizofunguliwa  mahakamani zinazohusu  mgogoro huo wa mipaka katika hifadhi hiyo.

Aidha alienda mbali na kusema kuwa serikali inapaswa kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha  wananchi wake hawapati mateso au  usumbufu usio wa lazima katika maeneo  yao kwa  kwani ndiyo wenye rasilimali hizo.

Pia alibainisha kuwa maeneo mengi  yanayotumiwa na wananchi, yamekuwa na migogoro mingi inayohusu mipaka ya ardhi hasa wakati wa shughuli za upanuzi wa hifadhi za taifa au uwezekezaji  mkubwa unapotakiwa kufanyika jirani na makazi ya wananchi.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Maimuna Kibenga, alisema mipango ya wizara yake iko katika hatua nzuri ikilenga kuondoa au kumaliza migogoro yote ambayo imekuwa ikijitokeza katika maeneo mengi ya hifadhi za taifa nchini.

Maimuna alisema kuwa wizara yake kupitia bodi ya hifadhi za taifa imekuwa ikifanya kazi kwa kufuata taratibu kanuni na sheria zinazoiongoza wizara hiyo hivyo hatarajii kuona mambo yanaenda kinyume kwa kuwa kila mtumishi wa wizara hiyo anatakiwa kufanya kazi kwa kuheshimu na kuzingatia sheria.

Pia Dk. Martin Loibooki ambaye ni Mkurugenzi  wa Hifadhi za Taifa (Tanapa), alisema kuwa kazi na majukumu ya Wizara  ya Maliasili na Utalii ni uhifadhi si vinginevyo.

Hata hivyo alitahadharisha kuwa huenda shirika hilo  likafungwa  katika siku zijazo kutokana na mifumo mipya iliyopo ambayo lengo lake halilengi kuendeleza shirika bali kusababisha  mwingiliano wa kiutendaji na kudhoofisha uwajibikaji kwa kuwa mfumo uliopo, hauko  kwa ajili ya maslahi ya shirika hilo.


juu 


Ujangili walitesa Bunge

chanzo Tanzania daima 

TUHUMA za ujangili na Operesheni Tokomeza UIjangili inayoendeshwa na serikali, jana ziliiteka Bunge baada ya Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola (CCM), kuituhumu serikali kwa kutoa hoja nyepesi bungeni.
Lugola alisema operesheni hiyo inafanyika kwa kukiuka haki za binadamu, kwamba watu wasiokuwa majangili wamekamatwa, kuteswa na kuharibiwa mali zao ilhali majangili wanaojulikana wakiachwa waendelee na uhalifu wao.
Wakati mbunge huyo akitoa tuhuma hizo, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha, aliwatuhumu wabunge na wanasiasa wengine kwa kuingilia utendaji wa operesheni hiyo kwa kuwatetea wanaokamatwa kwa kujihusisha na ujangili.
Kauli ya Nahodha ilionekana kumpiga kijembe Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, ambaye wiki iliyopita msaidizi wake (ofisi ya ubunge) alikamatwa mkoani Iringa kwa tuhuma za ujangili.
Jana Lukuvi alidai anao ushahidi ‘mzito’ wa mateso aliyoyapata msaidizi wa ofisi yake, ambaye aliachiwa juzi baada ya kuonekana kutohusika na ujangili kama ilivyokuwa ikidhaniwa.
Hoja ilivyoanza
Hoja hiyo ilitokana na swali la nyongeza lililoulizwa na Mbunge wa Kahama, James Lembeli (CCM), aliyetaka kujua kwanini serikali inaendelea kuwalinda wanasiasa, askari na watendaji wake wanaojihusisha na ujangili.
Lembeli pia alitaka kujua kwanini serikali haiwachukulii hatua za kisheria makamanda wa polisi wa mipakani, hasa wale wanaopakana na mbuga ya Serengeti, wanaojihusisha na ujangili, kutorosha nyara za serikali pamoja na kushirikiana na majangili.
Akijibu maswali hayo, Naibu Waziri wa Maliasili na Mazingira, Lazaro Nyalandu, alisema kamwe wizara yake haiwalindi wanasiasa, wabunge, maofisa wa polisi na watendaji wa serikali wanaohusika na ujangili.
Nyalandu alisema kuanzia sasa kila kiongozi atakayekamatwa kwa tuhuma za ujangili atatangazwa hadharani.
Alisema si sahihi kuwatuhumu wabunge, polisi na watendaji wengine wa serikali bila ya kuwa na utafiti juu ya tuhuma zao.
Hoja ya Lugola
Mara baada ya kipindi cha maswali na majibu kumalizika, Lugola aliomba mwongozo wa spika akitumia kanuni ya Bunge ya 67, ambapo alilitaka Bunge liiagize serikali kutoa taarifa ya operesheni hiyo inayofanyika nchi nzima.
Lugola aliomba mwongozo huo akisema kuwa majibu ya Waziri Nahodha na Nyalandu juu ya suala hilo ni ya mzaha mzaha yenye lengo la kuendeleza kulindana.
Mbunge huyo alilitaka Bunge liilazimishe serikali kutoa taarifa rasmi juu ya Operesheni Tokomeza Ujangili.
Mara baada ya Lugola, kuzungumza alisimama Lukuvi ambaye alitaka serikali iachwe imalize operesheni hiyo bila kutoa taarifa kwani wakifanya hivyo wanaweza kusababisha wahusika wakimbie au kupoteza ushahidi.
Alisema  taarifa za operesheni hiyo zitapelekwa katika kamati zinazohusika mara baada ya kufikia tamati na baadae zitafikishwa bungeni kulingana na taratibu zinazotakiwa.
Lukuvi pia alionyesha simu yake ya mkononi akidai ina ushahidi wa mateso yanayofanywa dhidi ya wanaokamatwa kwa tuhuma za ujangili.
“Nina ushahidi wa msaidizi wangu alivyoteswa baada ya kukamatwa kuwa ni jangili, huyu wamemuachia jana, nawaombeni tuache operesheni hii imalizike ndipo tupatiwe taarifa zake,” alisema.
Naibu Spika Job Ndugai, aliunga mkono kauli ya Lukuvi akidai taarifa za operesheni hiyo zikitolewa sasa zitaharibu zoezi hilo.
Hoja ya Lema
Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, amesema anatarajia kuwasilisha maelezo binafsi bungeni kuitaka serikali izuie uwindaji wa tembo katika vitalu vilivyo karibu na hifadhi au mbuga.
Lema alisema ameamua kufanya hivyo kutokana na ujangili kuzidi kushika kasi. Inakadiriwa tembo 30 wanauawa kila siku.



Anti-poaching unit accused of killings


By Mussa Juma and Zephania Ubwani in Arusha, Bernard Lugongo in Dar, Peter Nyanje and Frank Kimboy,The citizen

Posted  Wednesday, October 30  2013 
In Summary
Other reports say eight pastoralists from Orbomba Village in Longido District have not been seen since they were arrested last week.
Dar/Dodoma/Arusha. The anti-poaching campaign in the country has come under sharp criticism following reports of widespread human rights abuses, including the killing of a woman believed to have died at the hands of officers of the anti-poaching unit--which is comprised of the police, the army and intelligence officers.
Emaliana Gasper Maro, 46, is reported to have been snatched from her house by people who identified themselves as anti-poachers. They said they wanted to question the resident of Galapo in Babati, Mara Region. This came only a few days after they reportedly grabbed her husband, Elias Kibuga, 56.
Mr Kibuga has not been seen since but Emiliana’s body was found at Mrara hospital mortuary in Babati. Scores others are missing. The officers are also said to have burnt houses and are reported to be holding large herds belonging to pastoralists in Arusha region. The government has reportedly been urged to stop the exercise and ensure that lives and property are respected.
Yesterday, the government came under attack from MPs in Parliament over claims of widespread abuse of human rights.
The Manyara region police commander, Mr Akili Mpwapwa, confirmed the reports but said an ongoing investigation would unearth the truth. “I have received reports of the death of Emaliana and the investigations have started,” Mr Mpwapwa said.
The results of a post-mortem that was jointly carried out by the police and the family doctor have not been made public.
A total of 27 pastoralists and 2,169 livestock are being held by the anti-poaching unit, according to the coordinator of the Tanzania Pastoralist Community Forum, Mr Joseph ole Parsambei. “We will go to court to stop this exercise if human rights violations continue,” said Mr Parsambei.
Other reports say eight pastoralists from Orbomba Village in Longido District have not been seen since they were arrested last week. The unit is also said to be holding 2,000 livestock. Efforts to get the authorities to address the allegations hit a wall.
The minister for Natural Resources and Tourism, Mr Khamis Kagasheki, who had set off the special anti-poaching campaign when he gave the shoot-to-kill order during the Global Elephant March in October 4, was tight lipped. “I have nothing to say on that issue,” Mr Kagasheki told The Citizen. “Every ministry has its spokesperson. Talk to him not me.”
The director for Wildlife at the ministry of Natural Resources and Tourism, Mr Alexander Songorwa, referred the matter to Tanzania People’s Defence Force (TPDF). The TPDF spokesman, Mr Erick Komba, told The Citizen he was not aware of the allegations. He added: “The operation is carried out jointly by the police, game wardens and intelligence.”
The Attorney General, Justice Frederick Werema, said no minister had the powers to give a shoot-to-kill order. He told The Citizen: “I did not hear the minister give the order. I suppose he was aggrieved by the high rate of poaching in the country. All security forces must arrest suspects. They can only shoot in self-defence.”
It is estimated that Tanzania loses 30 elephants per day--or 10,000 a year. If the poaching trend persists, there might well be no elephants in Tanzania in 10 years. Of the ivory seized in ports and airports in the past decade, it is estimated that one-third originated from Tanzania. The elephant population in the country has dropped to below 100,000 from about 130,000 a few years ago.
In Parliament, Alphaxard Kangi Lugola, the outspoken Mwibara MP (CCM), said it was amazing that while the actual poachers are known, the government has been targeting people who have nothing to do with the vice.
“We have heard names of people suspected of poaching who include government officials and politicians,” he charged. Mr Lugola wanted the government to table in Parliament a report on Operation Tokomeza, which is aimed at addressing poaching.
Mr James Lembeli (Kahama–CCM) said evidence suggests that public officials, MPs and big businessmen are behind the poaching but they have not been touched.
The State Minister in the PM Office (Policy, Coordination and Parliament), Mr William Lukuvi, said his assistant was arrested two days ago, beaten seriously and tortured--and was released only yesterday by the anti-poaching unit. He added: “We should wait for the operation to end and the ministry will table a report before a relevant committee.”
The acting leader of government business in Parliament, Mr Shamsi Vuai Nahodha, said the government was aware of the accusations and asked those involved in the operation to respect human rights. “There are also politicians who have been influencing this operation,” he added. “When we started, we asked you to bear with us, please give us time and space to conduct this operation.”


‘Tunataka majina ya vigogo majangili’










 WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII BALOZI KHAMISI KAGASHEKI
Na Sharon Sauwa na Habel Chidawali,Mwananchi

Posted  Jumatano,Oktoba30  2013  saa 24:0 AM
Kwa ufupi
“Inashangaza sana kuwa wale wanaotajwa hawachukuliwi hatua, lakini wananchi wanazidi kuteseka… Mathalani, zipo taarifa kuwa wakuu wa polisi katika mikoa inayopakana na Mbuga ya Serengeti ndio waratibu wa shughuli za ujangili, lakini hatujasikia hao wakichukuliwa hatua,”
Dodoma. Wabunge jana walichachamaa na kushinikiza kutolewa kwa orodha ya vigogo wanaojihusisha na ujangili wakati wa kikao cha kwanza cha mkutano wa 13 wa Bunge unaofanyika mjini Dodoma.
Wabunge hao walitaka kutajwa kwa majina ya mawaziri, viongozi wa Serikali na wabunge wanaojihusisha na biashara hiyo.
Baada ya kumalizika kwa kipindi cha maswali na majibu, Mbunge wa Mwibara (CCM), Kangi Lugola, aliomba mwongozo, akiitaka Serikali kuwataja hadharani na kuwachukulia hatua viongozi wake na wanasiasa, wakiwamo mawaziri na wabunge, ambao wanatajwa kuhusika na vitendo vya ujangili nchini.
Lugola aliomba mwongozo wa Naibu Spika baada ya kutoridhishwa na jibu lililotolewa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Kahama (CCM), James Lembeli.
Katika jibu hilo, Nyalandu alilieleza Bunge kuwa Operesheni Tokomeza inayolenga kukomesha vitendo vya ujangili nchini bado inaendelea, lakini alishindwa kulieleza Bunge ni nani hasa wamebainika kuhusika na vitendo hivyo.
Lugola, hata hivyo, aliitaka Serikali kuwasilisha ripoti bungeni kuhusiana na utekelezaji wa operesheni hiyo.
“Tangu Aprili tumekuwa tukipewa majibu mepesi kuhusiana na operesheni hii, wakati suala hili si la masihara,” alionya Lugola.
Lugola alisema kuwa taarifa zimewataja watu wanaohusika na vitendo hivyo wakiwamo viongozi serikalini, mawaziri pamoja na wabunge, lakini tangu operesheni hiyo ilipoanza hakuna yeyote miongoni mwa hao wanaotajwa ambaye amekamatwa isipokuwa wananchi wa kawaida.
Alisema operesheni hiyo imekuwa ikiendeshwa kwa unyama kwani wanaokamatwa hupigwa na kuteswa bila ya ushahidi unaoonyesha kuhusika kwao na vitendo vya ujangili.
“Inashangaza sana kuwa wale wanaotajwa hawachukuliwi hatua, lakini wananchi wanazidi kuteseka… Mathalani, zipo taarifa kuwa wakuu wa polisi katika mikoa inayopakana na Mbuga ya Serengeti ndio waratibu wa shughuli za ujangili, lakini hatujasikia hao wakichukuliwa hatua,” alisema.
Kabla ya Naibu Spika kutoa majibu ya mwongozo ulioombwa na Lugola, Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, alisimama na kukiri kuwapo kwa vitendo vya utesaji wa watu wanaokamatwa katika operesheni hiyo.
Alitolea mfano tukio la kukamatwa kwa msaidizi wake jimboni ambaye alipigwa na kuteswa na askari hao kabla ya kuachiwa baada ya kushikiliwa kwa siku moja, huku akionyesha kuwa ushahidi wa tukio hilo anao kwenye simu yake.
“Lakini sisemi haya kwa kutaka kuitetea Serikali kuwa isilete ripoti hapa bungeni. Nadhani kuwa kuleta ripoti hivi sasa haitakuwa vizuri. Ni vizuri tusubiri mpaka kazi hii ikamilike na nina uhakika kuwa Wizara itaandaa ripoti na kuiwasilisha kwenye kamati husika,” alisema na kuongeza:
“Nadhani kuwa `entry point’ (mahali pa kuanzia) yetu iwe ni kwenye ripoti hii itakayowasilishwa kwenye Kamati,”
Suala la ujangili limeingizwa bungeni wakati kukiwa na usiri mkubwa wa nani anahusika na vitendo hivyo, huku majina ya vigogo wanaotajwa kuhusika nayo wakiwa hawafahamiki.
Polisi watajwa vinara
Awali akijibu swali la msingi lililoulizwa na Mbunge wa Kigamboni (CCM), Dk Faustine Ndugulile, Nyalandu alisema Jeshi la Polisi ni vinara miongoni mwa makundi manne ya majeshi ambayo watumishi wake wamekamatwa wakijihusisha na ujangili.
Katika matukio saba ya ujangili yaliyowahusisha watumishi tisa wa vyombo vya ulinzi na usalama, Nyalandu alisema kati ya hao sita ni polisi wakati kwa kupande wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na Magereza alikamatwa mtu mmoja mmoja.
“Katika matukio hayo, jumla ya meno ya tembo 686 na vipande 447 vikiwa na uzito wa kilogramu 4,253.9 vilikamatwa, jambo ambalo linaonyesha ukubwa wa tatizo hilo kwa vyombo vya ulinzi,” alisema Nyalandu.
Katika swali la msingi, Dk Ndugulile alitaka kufahamu idadi ya matukio ya upatikanaji wa pembe za ndovu yaliyohusisha vyombo vya ulinzi na usalama.
Katika swali la nyongeza, Lembeli ambaye ndiye aliyeuliza swali hilo kwa niaba ya Dk Ndugulile, aliitaka Serikali kuacha kigugumizi na kueleza ukweli kuwa wapo baadhi ya viongozi, wakiwamo wabunge ambao wamekuwa wakijihusisha na biashara hiyo.
“Katika biashara ile kuna hali ya kulindana sana, hebu Serikali itueleze taarifa za kuwa wahusika wengine ni wanasiasa na baadhi ya wabunge, ukweli uko wapi, na kuna taarifa kuwa viongozi wa Polisi wanaoishi kuzunguka hifadhi zetu ndio ambao wanatumiwa kusafirisha nyara hizo, Serikali inasemaje?” alihoji Lembeli.
Nyalandu alisema Tanzania iko katika hali mbaya katika kiwango cha mauaji ya tembo ambapo wastani unaonyesha kuwa kila siku tembo 30 huuawa na majangili.
“Hata hivyo, suala la ulinzi bado tuko nyuma sana kwani wastani wa ulinzi wa kimataifa ni askari mmoja kwa kilomita za mraba 25, lakini sisi askari wetu mmoja analinda kilomita za mraba 150 ndani ya hifadhi,” alisema Nyalandu.
Serikali yakiri tatizo
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha akizungumza bungeni kwa niaba ya Waziri Mkuu, alikiri kuwapo fununu za wanasiasa ambao wamekuwa wakijihusisha na biashara hiyo na kusema Serikali italifanyia kazi jambo hilo.
Nahodha aliwataka Watanzania kuwa watulivu wakati vyombo vya Ulinzi na Usalama vinaposhughulika na kusafisha tatizo hili na kuonya wanasiasa kuacha kutoa shinikizo kwa kutumia nguvu zao za kisiasa.


Tuesday, October 29, 2013

MJADALA BUNGENI KUHUSU UJANGILI

Toka jan-okt mwaka huu  matukio 7 yaliyohusisha  kukamatwa kwa maaskari wa polisi,magereza,jwtz  na wanyama pori wakihusika na biashara haramu ya meno ya tembo yametajwa bungeni.
Matukio hayo yalihusisha ukamataji wa meno  646,na vipande zaidi ya 440 ,hali hiyo inatia shaka juu ya vyombo vyenye dhamana ya ulinzi wa maliasili .

Akijibu maswali ya liyoulizwa na James Lembeli aliyetaka kujua maafisa wa polisi walioko mikoa iliyo kando ya hifadhi ya Taifa ya Serengeti  kushirikiana na  majangili kutorosha nyara na pia kulindana kwa kuwa watuhumiwa baadhi ni wanasiasa.

 Naibu waziri wa maliasili na utalii Lazaro Nyalandu alisema hakutakuwa na kulindana na operesheni Tokomeza inayohusisha vyombo vyote vya ulinzi haitamuacha hata mtu mmoja 
anayetuhumiwa kuhusika na vitendo vya ujangili hata angalikuwa mwanasiasa.

Hata hivyo Lugola mbunge wa mwibara ameibuika na mwongozo kuwa operesheni tokomeza inayohusu ujangili wa tembo,"kuna watu wako ndani ya hifadhi wamekamatwa na wanapigwa...lakini wawindaji wa tembo hawakamatwi,hawapigwi huu ni mzaha,hapa kuna kulindana maana inaonekana wanaohusika ni watu wakubwa ,wabunge ,mawaziri wasemwe na wakamatwe si kuendelea kuonea wananchi wasiokuwa na hatia,naomba mwongozo wako.

Lukubi anasema taarifa itatolewa kwa kamati ya Maliaisli maana operesheni inayoendelea inalenga kuwabaini na kuwakamata wahusika ,amekiri kuwa msaidizi wake wa jimbo amekamatwa na amepigwa sana na alikutwa ofisini kwa Lukuvi na anao ushahidi wa kilichotokea.

Monday, October 28, 2013

WAHUKUMIWA KIFUNGO KWA KUINGIA H.IFADHINI BILA KIBALI

   Oktoba 28,2013.
Serengeti:
WAKAZI wanne kutoka wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha wamehukumiwa na mahakama ya  wilaya ya Serengeti  kifungo cha miezi sita jela ama kulipa faini ya sh,120,000 kila mmoja  kwa kosa la  kuingia hifadhi ya taifa ya Serengeti bila kibali.
Waliohukumiwa na mahakama hiyo ni  Ndotei Sundi(30)Siatoi Warukwar(19) Kitupe Lesiani (30)wakazi wa kijiji cha Warbai na Daud Kesoi(19)mkazi wa kijiji cha Maranja  Ngorongoro ambao walikosa fedha na kuamriwa kwenda gerezani.
 walitenda kosa hilo oktoba 23 mwaka huu majira ya saa 8:00 mchana.
Mbele ya hakimu mkazi wa mahakama hiyo  Franco Kiswaga , Mwendesha mashitaka  wa polisi sajenti Paskael Nkenyenge  alidai oktoba 23 mwaka huu majira ya saa  8:00 mchana  askari wa hifadhi hiyo wakiwa doria eneo la Naabi waliwakamata washitakiwa hao na hawakuwa na kibali cha kuingia hifadhini.
Washitakiwa wote walikiri shitaka la kuingia hifadhini bila kibali na kuilazimu mahakama hiyo kutoa adhabu kulingana na kosa walilotenda.
Akitoa hukumu Hakimu Kiswaga ameiambia mahakama kuwa kufuatia washitakiwa kukiri shitaka bila kuisumbua mahakama ,anawahukumu kila  mmoja  kulipa faini ya shilingi 120,000  ama kutumikia kifungo cha miezi sita jela ili iwe onyo kwa wenye tabia kama hiyo .
Mwisho.

Tido: Sekta ya habari inaweza kukuza utalii



Chanzo- Mwananchi

Posted  Ijumaa,Oktoba25  2013 
Kwa ufupi
Alisema muda umefika kwa filamu na matangazo yote yanayoelezea vivutio vya utalii Afrika kuandaliwa, kurekodiwa na kurushwa na Waafrika wenyewe.
Arusha. Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi Communications (MCL), Tido Mhando amesema tasnia ya habari ikitumika vyema inaweza kutoa mchango mkubwa kuinua sekta ya utalii kutokana na kuaminiwa na kufikia watu wengi kwa wakati mmoja.
Mhando alisema hayo jana akizungumzia nafasi ya vyombo vya habari katika kuinua sekta ya utalii Afrika wakati wa mkutano wa Umoja wa Vyombo vya Utangazaji Kusini mwa Afrika (SABA).
Kwa mujibu wa Mhando , umuhimu wa vyombo vya habari unachagizwa na maendeleo na matumizi ya sayansi na teknolojia inayorahisisha utengenezaji na urushaji wa matangazo yenye ubora.
Naye Meneja Uhusiano wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Innocent Mungi aliwataka watengenezaji wa vipindi na filamu kutoka nchi za Kusini mwa Afrika kuandaa, kutengeneza na kurusha vipindi vinavyoonyesha na kutangaza vivutio vya utalii vinavyopatikana katika ukanda huo, ili kukuza sekta ya utalii.
Alisema muda umefika kwa filamu na matangazo yote yanayoelezea vivutio vya utalii Afrika kuandaliwa, kurekodiwa na kurushwa na Waafrika wenyewe.
Awali akifungua Mkutano Mkuu wa 21 wa SABA, Makamu wa Rais, Dk Mohammed Gharib Bilal alivitaka vyombo vya SADC kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo katika nchi zao, badala ya kuacha kazi hiyo kufanywa na vyombo vya habari vya nje.
Dk Bilal alivitaka vyombo ya utangazaji kutumia kuaminika kwao kwa jamii kuhamasisha uhifadhi wa mazingira na ulinzi wa maliasili.

Sunday, October 27, 2013

Lembeli: Ruaha kiini cha mgogoro wa Ihefu



Jumamosi, Octoba 26, 2013 07:20 Na Pendo Fundisha, Mbeya
KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, imesema Hifadhi ya Taifa ya Ruaha ni kiini cha mgogoro wa ardhi unaoendelea katika Bonde la Ihefu kutokana na kumega maeneo yasiyoainishwa na kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Mbeya (RCC). Kauli hiyo ilitolewa mjini hapa jana na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, James Lembeli, katika ziara ya kukagua shughuli na miradi ya Serikali.

Alisema kikao cha RCC ndicho kilipaswa kuyaingiza maeneo hayo au kutoyaingiza ndipo hifadhi hiyo ingetekeleza majukumu yake ya kuweka mipaka.

Alisema eneo lililoongezwa na hifadhi hiyo ni kutoka kilomita 10,000 za mraba hadi kufikia kilomita 20,000 za mraba ambazo hazikuainishwa katika kikao cha RCC.

Aidha, imeitaka Serikali kutoa majibu haraka ya tume zilizoundwa kwa ajili ya kuchunguza mgogoro wa mpaka baina ya wananchi wa vijiji hivyo na hifadhi hiyo.

“Serikali iliunda tume mbalimbali za kuchunguza tatizo hili ikiwamo timu ya wataalamu iliyoundwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda. Hivyo ni vema ikaharakisha kutoa majibu kwa kuwa muda mrefu umepita pasipo kusema lolote lile,” alisema Lembeli.

Naye, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Maimuna Tarishi, alisema mgogoro huo upo njiani kumalizika kwa kuwa suluhisho lake limefika katika ngazi za mwisho.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa), Martin Loibooki, alisema jambo hilo limechukua muda mrefu baada ya kuwapo kwa mkanganyiko juu ya uwekaji wa mipaka hiyo, ambapo kuna wananchi walipeleka kesi hiyo mahakamani kuwa walipunjwa fidia zao.

Saturday, October 26, 2013

TAHARIRI-TANZANIA DAIMA

Ujangili ni zao la kulindana


KWA muda mrefu sasa nchi mbalimbali zimekuwa kwenye mapambano ya ujangili, hasa ule wa meno ya tembo.
Inakadiriwa kila dakika 15 tembo mmoja huuawa duniani.
Biashara ya meno ya tembo hivi sasa imeshamiri zaidi.
Kwa mujibu wa Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki jino moja huuzwa kati ya dola za Marekani 1,500 na 2,000.
Pamoja na jitihada za kupambana na ujangili huu, bado matukio ya vifo vya tembo yanaongezeka kila kukicha kutokana na ukosefu wa vifaa pamoja na uadilifu mdogo wa watendaji waliopewa jukumu la kusimamia.
Tunaamini kama utaratibu wa kulindana, kuoneana aibu na kupuuzia mambo usingekuwepo, Tanzania ingepiga hatua kubwa katika mapambano dhidi ya ujangili.
Limekuwa jambo la kawaida kila kukicha kusikia watendaji wa serikali, vyombo vya dola, idara au taasisi mbalimbali kukamatwa wakiwa na meno ya tembo na nyara mbalimbali ambazo ni kosa la kisheria.
Pamoja na watu hao kukamatwa na nyara hizo, bado inaonekana hakuna uwajibishanaji ndiyo maana watumishi wengine wamekuwa wakiendelea na uahalifu huo, na hata kushirikiana na watu kutoka nje.
Tunaamini kuwa mpango wa serikali wa kutumia ndege zisizo na marubani kupambana na ujangili hauwezi kufanikiwa kama tabia ya kulindana, kuoneana aibu haitakomeshwa.
Tunaamini ‘Operesheni Tokomeza Majangili’ itakuwa na manufaa zaidi ikiwa Wizara ya Maliasili na Utalii itasafisha kwanza nyumbani kwake, ikiwemo kuwachukulia hatua kali watumishi wanaohusishwa na uhalifu.
Tunachukua fursa hii kumpongeza Waziri Kagasheki kwa kutangaza hadharani kuwa Kikosi Cha Kupambana na Ujangili (KDU), wanasiasa, watumishi wa umma na wafanyabishara mbalimbali wanahusika na biashara hii.
Tunajua kuwatangaza watu kuhusika na biashara hii ni hatua moja muhimu, hivyo ni vema hatua nyingine ya kuwakamata na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria ikachukuliwa.
Bila kuwajibishana, kudhibitiana, biashara ya meno ya tembo, faru na mazao ya misitu itaendelea kushamiri huku taifa likiangamia kwa kukosa mapato yatokanayo na wanyama hao.
Tunaamini kuwa serikali itaitumia kikamilifu Operesheni Tokomeza Ujangili kukabiliana na watu wote wanaohusishwa na vitendo hivyo vya kihalifu bila kujali nyadhifa zao.

Waziri Kagasheki matatani


•  Raia wa kigeni aliowaita majangili, walibambikwa kesi
na Grace Macha, Arusha-Chanzo Tanzania Daima

JESHI la Polisi mkoani Arusha, limeingia kwenye kashfa nzito baada ya kubainika kumdanganya Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki kwa kuwahusisha raia wawili wa kigeni na biashara ya ujangili wakati si kweli.

Hatua hiyo inakuja baada ya Waziri Kagasheki kudai kuwa watumishi wa serikali wanakwamisha juhudi za kukabiliana na majangili wa tembo, akitolea mfano wa Mkuu wa Upelelezi wa Polisi mkoani hapa (RCO), Duwan Nyanda, kwamba aliwatorosha raia wawili wa Saudia ambao walikamatwa wakiwa na meno ya tembo pamoja na silaha nzito.

Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali na nyaraka kadhaa, Tanzania Daima limebaini kuwa raia hao waliingia nchini Septemba 12, mwaka huu, kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) na kisha kufikia kwenye hoteli ya kitalii ya Mount Meru.
Nyaraka hizo zinaonyesha kuwa wageni hao waliondoka nchini Oktoba 4, mwaka huu, kupitia uwanja huo huo.

Kwa mujibu wa waraka wa upekuzi wa polisi (search order) uliosainiwa na Inspekta James, maofisa wa jeshi hilo walifika kwenye hoteli hiyo Oktoba 3, mwaka huu, na kupekua vyumba vya wageni hao, lakini hawakukuta kitu chochote kinachohusiana na nyara za taifa za maliasili kama ilivyodaiwa na Waziri Kagasheki. 

Nyaraka hiyo inaonyesha kuwa walioshuhudia upekuzi huo mbali na waliokuwa watuhumiwa, Ali na Nader, ni pamoja na Gidion David na Joseph Enock ambao waliisaini.
Tanzania Daima lilifika hotelini hapo na kuzungumza na meneja mapokezi, Enock Maselle ambaye pia alithibitisha kuwa Oktoba 3, mwaka huu, walifika polisi kwa ajili ya kukagua vyumba vya wateja wao, Ali na Nader.

Alisema kuwa waliwaruhusu, lakini akadai ni vigumu kujua nini kiliendelea.
Raia hao wanadaiwa kujihusisha na kutafuta watu nchini mwao ambao huwaleta Tanzania kutalii, na kwamba waliingia nchini na kundi la wageni tisa ambao walifanya safari kwa nyakati mbili tofauti, wakitembelea hifadhi za taifa za Manyara na Tarangire na 
Ngorongoro iliyopo chini ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA).

Mmiliki wa kampuni ya uwakala wa utalii ya Kalabash, Ally Kalabash aliliambia gazeti hili kwa simu kuwa Ali na Nader walimletea wageni tisa ambao alifanya nao safari ya siku tatu katika mbuga za Manyara, Ngorongoro na Tarangire.

“Hawa ni mawakala wapya, na hii ni mara yangu ya kwanza kufanya nao kazi, ila wageni walioniletea niliwahudumia mpaka siku wanaondoka, kwani wengine walilala Mount Meru Hotel na wengine Themi Suite,” alisema.

Naye Salim Islam Salim ambaye ndiye alikuwa karibu na raia hao wa Saudia, alisema kuwa  walipokuwa hapa nchini walikutana na Richard Kalembe ambaye aliwaambia anamiliki kampuni ya uwindaji wa kitalii ya RS Kalembe Hunting Routes.

Alisema kuwa Septemba 14, mwaka huu, Ali na Nader walimlipa Kalembe malipo ya awali kwa ajili ya kwenda kuwinda kitalii, kiasi cha dola za Marekani 3,000.
Salim alifafanua kuwa Kalembe aliwapatia wageni hao risiti yenye namba 012 ikionyesha kuwa bado wanadaiwa dola 7,000 endapo watatumia siku tano na ikiwa watatumia siku tisa wakiwinda, basi wangelazimika kuongeza dola 9,000.

Kwa mujibu wa Salim, baada ya Kalembe kupokea malipo hayo, hakufanya mawasiliano tena na wageni hao, hatua iliyowalazimu kutoa taarifa polisi Oktoba 2, mwaka huu.
Alisema kuwa siku iliyofuata, raia hao walipigiwa simu na polisi wa upelelezi aliyemtaja kwa jina moja la James, akiwaambia kuwa mtuhumiwa wao ameshapatikana, hivyo wafike polisi ili wakakabidhiwe fedha zao.

“Katika hali ya kushangaza, walipofika polisi waligeuziwa kibao na kuwekwa chini ya ulinzi, wakitakiwa kwenda kupekuliwa kwenye vyumba vyao katika hoteli waliyofikia ya Mount Meru, ambako hata hivyo hawakukutwa na kitu.

“Baadaye walirudishwa polisi na kuelezwa sababu za kupekuliwa, kwamba walitiliwa shaka kuwa wanajihusisha na ugaidi,” alisema Salim.

Alifafanua kuwa polisi waliwaambia kuwa kutokana na tukio la kigaidi lililotokea hivi karibuni nchini Kenya, wamekuwa makini kwa kila mtu wanayemuhisi au kumtilia shaka, na hivyo humfanyia upekuzi.

Kwa mujibu wa Salim, baada ya maelezo hayo walielezwa kuwa wanaweza kuwadhamini. Yeye na mtu mwingine aliyemfahamu kwa jina moja la Ibra, walimdhamini Ali huku Nader akidhaminiwa na msichana mwingine ambaye hakumfahamu vizuri.

“Oktoba 4, tulifika pale polisi asubuhi, baada ya panda shuka, watuhumiwa hao waliwaeleza polisi kuwa wanapaswa kuondoka siku hiyo, hivyo wakaomba wapewe ruhusa wakabadili tiketi zao au wapelekwe mahakamani ili wajue wanashikiliwa kwa makosa gani.

“Tukiwa pale, akaja polisi mmoja mwanamke akasema ‘kama hawa mmewapekua mkaona hawana kitu, waachieni waende zao’. Ilikuwa kama saa tano asubuhi,” alisema.
Salim alisema kuwa wageni hao walipewa simu na hati zao za kusafiria na hivyo wakaondoka kituoni hapo, na baadaye jioni walipanda ndege ya Shirika la Ndege la Ethiopia na kurudi kwao.

Alisema kuwa alishangazwa na taarifa zilizoandikwa na vyombo mbalimbali vya habari zikiwahusisha Ali na Nader na uwindaji haramu huku wakidaiwa kukutwa na pembe za ndovu, jambo alilodai ni uongo na upotoshaji mkubwa.

Salim alisema madai ya kwamba dola 3,000 zilitolewa polisi kama rushwa si ya kweli, kwani kiasi hicho ni fedha anazodaiwa Kalembe alizochukua kwa raia hao, huku akidai taarifa iko polisi.

Alipotafutwa Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Liberatus Sabas kuzungumzia sakata hilo, alisema hayuko tayari kwa sababu linashughulikiwa na mkuu wa jeshi hilo, IGP Said Mwema ambaye ameunda tume ya uchunguzi.

Naye Waziri Kagasheki alipotafutwa, simu yake iliita bila kupokelewa.

Salim ageuziwa kibao


Katika hatua nyingine, Salim na Gerald Kashiro wamelalamikia kitendo cha kukamatwa na askari wa kuzuia ujangili kwa nyakati tofauti na kupewa mateso makali, huku mfanyabiashara Shafiq Feroz akidai kuwa alishikiliwa bila kuteswa.

Walisema chanzo cha mateso hayo ni nyama ya nyati kilo tano ambayo Feroz alimpatia Kashiro baada ya kuwa amemsindikiza kuwinda kwenye pori la Terati wilayani Simanjiro.
Kashiro alisema kuwa yeye alipopewa nyama hiyo alimwachia mke wake, Judith Gerald nyumbani akiendelea kuiandaa, huku yeye akiendelea na shughuli zake.

Alisema kuwa baadaye alipigiwa simu akiambiwa kuwa mkewe na mama mkwe, wamekamatwa na askari wa Kikosi cha Kuzuia Ujangili (KDU) wakiwa na wanajeshi.
Akisimulia mkasa mzima, Salim alisema kuwa Kashiro alimpigia simu akimuomba ampeleke alipo Feroz ili aweze kupeleka vibali vyake vya uwindaji kwa kambi ya KDU iliyopo Njiro waweze kuwaachia mkewe na mama mkwe.

Alisema kuwa baada ya kumfikisha kwa Feroz, aliwaacha wakaelekea Njiro, na yeye akarudi kuendelea na shughuli zake, lakini wakampigia simu tena wakimuomba akawadhamini kwani wameshikiliwa.

Kwa mujibu wa Salim, juhudi za kuwadhamini Kashiro na Feroz hazikufanikiwa, hivyo aliamua kuondoka. Lakini kabla hajafika kwenye lango kuu la kutokea, akaitwa na kuulizwa na askari nyumbani kwake ni wapi ili wakampekue.

Aliongeza kuwa alipopekuliwa nyumbani kwake Kimandolu, alikutwa na bunduki tatu aina ya riffle na bastola aina ya short-gun ambazo zote anazimiki kihalali na kwamba walijiridhisha baada ya kuwaonyesha nyaraka zote muhimu kisha wakarudi naye hadi KDU Njiro.

“Mimi na Feroz tuliambiwa tujidhamini wenyewe kwani tunaacha silaha zetu pale. Feroz naye alikuwa amepekuliwa kwenye hoteli ya Themi Suites alipokuwa amefikia kutoka Dar es Salaam anakokaa.

“Tulitakiwa kurudi siku inayofuata, yaani Oktoba 8, mwaka huu, lakini tulipofika siku hiyo, tukachukuliwa na kufungwa pingu, tukapakiwa kwenye gari tukapelekwa Terati. Huko kuna eneo limefungwa hema, tulipofika sikuamini kama Tanzania kuna watu wanateswa hivyo,” alidai.

Kwa mujibu wa Salim, aliwekewa vijiti katikati ya vidole vyake na kuanza kuminywa, lakini akawahakikishia kwamba hajihusishi na ujangili.

“Wakachukua dumu la maji baridi la lita 10 na muda huo ni usiku, baridi ni kali, wakanimwagia mwili mzima nikiwa na nguo, kisha wakaniambia nitambae kwenye mchanga mpaka saa tisa usiku ndipo nilipewa fursa ya kulala,” alisema Salim.

Alisema kuwa walikuwa watu wengi wanaopatiwa mateso ya aina mbalimbali, ikiwemo kuchapwa viboko pamoja na kufanyishwa kwa nguvu mazoezi ya kupiga ‘push-up’. Waliondolewa baada ya siku tatu wakapelekwa Serengeti kwenye eneo lililotengwa kwa ajili ya kikosi hicho.

Salim alisema kuwa walipofika huko waliendelea kuteswa, na aliomba kuonana na daktari baada ya hali yake kuzidi kuwa mbaya kwani anakabiliwa na matatizo ya kisukari pamoja na figo iliyokuwa ikimuuma sana kutokana na mateke aliyopigwa.

“Daktari alishauri nipatiwe dawa na nipumzishwe, jambo lililonipa hauweni ya kutoendelea kupata mateso, maana nilihamishiwa Kituo cha Polisi Bunda nilikokaa kwa siku nne kabla ya kufikishwa mahakamani.

 “Hata hivyo, baada ya kufikishwa mahakamani sikusomewa shitaka lolote, bali hakimu aliniambia kuwa mahakama inaniachia huru kwani sina kosa. Nilihoji ni kwanini nikateswa bure siku 14,” alisema.

Kashiro ambaye naye alilalamikia kuteswa, alisema kuwa amefunguliwa shitaka la uhujumu uchumi pamoja na Feroz. Watatakiwa kufika mahakamani Bunda Novemba 7, mwaka huu wakati shauri lao litakapofika kwa ajili ya kutajwa.

Operesheni Tokomeza Ujangili ilianza rasmi Oktoba 5, mwaka huu katika hifadhi za taifa, mapori ya akiba na mbuga za wanyama ikishirikisha Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Polisi, Usalama wa Taifa, Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA), Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) na Idara ya Wanyamapori.