Wednesday, August 19, 2015

Ujangili tishio kwa ukuaji sekta utalii nchini




Na Waandishi wetu
19th August 2015
http://www.ippmedia.com/images/frontend/headline_bullet.jpg  Mwaka jana utafiti ulionyesha kuwa Tanzania imepoteza zaidi ya nusu ya tembo wake.
 
Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk. Adelhelm Meru.
Ujangili uliokithiri nchini Tanzania, unatishia kudhoofisha uchumi wa nchi ambao unazidi kukua.

Sekta ya utalii ina mchango mkubwa kwenye pato la taifa na katika kuongeza ajira.

Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk. Adelhelm Meru, ameonya kwamba kuna uwezekano ujangili ukaathiri ajira takriban milioni 3.8 kwenye sekta ya utalii katika ukanda wa Afrika Mashariki wakiwamo waongoza watalii, madereva, na hoteli na wahudumu wa migahawa. Kwa mujibu wa shirika la All Africa Tanzania pamoja na nchi nyingine barani Afrika zimeathirika mno kutokana na ujangili katika miaka 10 iliyopita. 

Mwaka jana, utafiti ulionyesha kuwa Tanzania imepoteza zaidi ya nusu ya tembo wake ambapo idadi imepungua kutoka tembo 110,000 mwaka 2009 kufikia chini ya tembo 44,000. 

Alisema Tanzania ina ajira 700,000 kutokana na idadi hiyo inaweza kuongezeka mara mbili endapo ujangili uliokithiri kwa wanyamapori utaisha.

Katika kuisaidia Serikali ya Tanzania, hivi karibuni mashirika ya Wildaid na African Wildlife Foundation, yalizindua kampeni mpya ijulikanayo kama `Ujangili Unatuumiza Sote’ kwa kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii.  

Utafiti uliofanywa na WildAid kwa kushirikiana na African Wildlife Foundation kwa kuwahoji Watanzania zaidi ya 2,000 waishio mijini na vijijini, uligundua kwamba asilimia 80 kati yao wanaelewa madhara yanayoweza kuikumba Tanzania endapo tembo watatoweka. 

Kati ya walihojiwa katika utafiti huo, asilimia 73 walisema wanyama pori ni mojawapo ya alama za taifa na urithi wa taifa.

Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wildaid, Peter Knights, alisema: “Ujangili kwa tembo ni wizi unaowaumiza Watanzania wa sasa na wa vizazi vijavyo.” 
CHANZO: NIPASHE