Sunday, August 18, 2013

AKAMATWA NA MENO YA TEMBO



Mvietnam adakwa na Meno ya ndovu uwanjhttp://www.mwananchi.co.tz/image/view/-/1596856/data/43/-/appotyz/-/ico_plus.pnga wa ndege

Kwa ufupi
Baada ya kufanyiwa upekuzi wa kina katika begi lake alikutwa na bangili 138 na vijiti 362 vilivyotengenezwa kwa meno ya tembo.

D’Salaam. Raia wa Vietnam, anashikiliwa na Jeshi la Polisi baada ya kukutwa na shehena ya pembe za ndovu ya kilo 19 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).

Mtu huyo amekamatwa wakati bado suala la watu kukamatwa na dawa za kulevya likiendelea kurindima. Julai 5 mwaka huu, wasichana wawili Agnes Gerald (Masogange na Melisa Edward ) walipitisha kilo 180 za dawa hizo na kwenda kukamatiwa Afrika Kusini.

Agosti 14 mwaka huu pia mtu mmoja alikamatwa akiwa na kete 86 za dawa za kulevya aina ya heroini na misokoto 34 ya bangi.

Akizungumza na waandishi wa habari jana ofisini kwake, Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere, Deusdedit Kato alisema, raia huyo alikamatwa juzi jioni akiwa anatokea Msumbiji na ndege ya Air Mozambique na alikuwa katika harakati za kubadilisha ndege ili apande ndege ya Dubai.
“Jana (juzi) majira ya saa 10:45 alasiri hapa uwanja wa ndege, alikamatwa raia wa Vietnam akitokea Msumbiji na ndege ya Shirika la Ndege la Mozambique Airlines… alikuwa katika harakati za kubadilisha ndege ili apate ya kwenda Vietnam kupitia Dubai, ndipo maofisa wetu wa polisi, uwanja wa ndege na maliasili wakamshtukia,” alisema na kuongeza: “Ilikuwa ni kwa ‘physical inspection’ (uchunguzi wa macho), aliweza kugundulika.
Baada ya kufanyiwa upekuzi wa kina katika begi lake alikutwa na bangili 138 na vijiti 362 vilivyotengenezwa kwa pembe za ndovu. Vyote vina uzito wa kilo 19 na thamani ya Sh18.4 milioni.”
Hata hivyo, alisema kuwa jitihada za kumhoji mtuhumiwa bado zinaendelea kwa kuwa hajui lugha ya Kiswahili wala Kiingereza.
“Bado tunatafuta mkalimani ili tumhoji kwa kina halafu atafikishwa mahakamani. Sheria inaruhusu mtu kushtakiwa popote anapokamatiwa, siyo lazima tumrudishe Msumbiji au kwao Vietnam,” alisema Kato. Akizungumzia hali ya ulinzi uwanjani hapo, Kato alisema kuwa imeimarishwa na kwamba ukitokea uhalifu huwa ni wa kupangwa tu.
“Siku zote tunawakamata wahalifu kama hawa, ikitokea kama ule mzigo wa mabegi tisa ya dawa za kulevya, haina maana kwamba ulinzi ulilegea, watu walijua kitu kinachoendelea. Sasa ndiyo tunajiuliza, kwa nini walijua halafu wakanyamaza,” alisema Kato..

Thursday, August 15, 2013

WAZIRI KAGASHEKI,MAJINA YA MAJANGILI WANAYO


WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki amesema kuwa wanayo majina ya wafanyabiashara wakubwa wanaojihusisha na ujangili nchini.
Akizungumza na waandishi jana jijini Dar es Salaam katika ofisi ndogo za Bunge, Balozi Kagasheki alisema kuwa wanaojihusisha na biashara hiyo wanafahamika, na kwamba tayari jitihada mbalimbali zimeanza kuchukuliwa.
Alisema kuwa mtandao huo wa majangili kwa sasa unajulikana na kuwa wanatarajia kufanya operesheni kubwa ambayo haijawahi kutokea ili kuwanasa.
Kagasheki alisema kuwa mtandao huo unahusisha wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi, na kuwa wapo katika mchakato wa kufuatilia nchi zinazonunua bidhaa zinazotokana na ujangili huo.
“Mtandao wa majangili kwa sasa unajulikana, tuna majina ya na tayari jitihada mbalimbali zimeanza kuchukua, hata kukamatwa kwa mfanyabiashara wa kizungu hivi karibuni ni jitihada hizo,” alisema.
Naye Waziri Kivuli wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Mchungaji Peter Msigwa (CHADEMA) alisema kuwa kutokana na tatizo la ujangili kuzidi kushamiri, amelazimika kuwasilisha barua ofisi ya Bunge kwa ajili ya kupeleka hoja binafsi ya kuweza kupata ufumbuzi wa suala hilo.
Alisema kuwa suala hilo si dogo kama inavyofikiriwa kwa kuwa tembo wanaendelea kumalizika kama juhudi za makusudi hazitachukuliwa.
“Japokuwa hoja yangu inaweza kushindwa kujadiliwa kwa kuwa suala hili linahusu watu wakubwa na wengine wenye majina. Maana niliwahi kuomba jambo hilo lifanyiwe kazi, lakini jitihada zangu ziligonga mwamba,” alisema.
Hata hivyo, Msigwa alishauri kwenda mbali zaidi ili kuibaini Kampuni ya TALL ambayo mkurugenzi wake alikamatwa na nyara za serikali.
Alisema kuwa hatua ya kukamata watu wanaokutwa na pembe za ndovu haitasaidia isipokuwa kutafuta mtandao wa wanaojihusisha na biashara hiyo na kuuweka hadharani.


Tuesday, August 13, 2013

KAMATI YASEMA VIGOGO WAHUSISHWA NA UJANGILI

Vigogo wahusishwa na ujangili

na Betty Kangonga

MWENYEKITI wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, James Lembeli, amesema kuna kila dalili kwamba baadhi ya vigogo serikalini wanahusika na biashara ya meno ya tembo nchini.
Matukio ya watu kukamatwa na meno ya tembo nchini yameongezeka siku hadi siku kwa kuwa Julai 29, mwaka huu, watu tisa walikamatwa na meno ya tembo, wawili kati yao wakiwa polisi wa Kituo cha Oysterbay, Dar es Salaam waliokamatwa Kisarawe, mkoani Pwani, wakisafirisha meno 70 ya tembo (kilo 305) kinyume cha sheria.
Lembeli aliyasema hayo katika kikao cha pamoja kati ya kamati yake na watendaji wa Wizara ya Maliasili na Utalii jijini jana na kusema kuwa meno hayo kwa hesabu za kawaida ni sawa na tembo 35, thamani yake ni zaidi ya sh milioni 850, huku juzi raia wa Uingereza Robert Dewar akikamatwa nchini akiwa na nyara za serikali zenye thamani ya sh 118,314900.
Raia huyo ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Trans Afrikas Longistics (TALL) alikamatwa na vipande nane vya meno ya tembo, vinyago 11, meno 20 ya tembo, meno 20 ya simba, kucha 22 za simba, ndege mmoja aina ya kasuku, vipande vya miti ya mpingo na idadi kubwa ya vinyago vitu vyote hivyo vilikuwa na uzito wa kilogramu 24, alivyokuwa navyo kinyume na sheria.
Lembeli alisema kuwa hatua ya kuendelea kwa matukio ya kuuawa kwa tembo nchini inatoa ishara kuwa serikali haina haja ya kuchukua hatua kwa sababu inafanywa na watu wakubwa.
Lembeli alisema kuwa kamati yake ilishatoa mapendekezo na ushauri wa kufanywa na serikali ili kukabiliana na wimbi la uuaji wa tembo lakini cha kushangaza hadi sasa hakuna utekelezaji wa jambo.
“Mimi siamini hata hizo takwimu za kukamatwa meno hayo kama zina ukweli wowote maana hadi sasa rasilimali hiyo inakwisha polepole na wala serikali haishtuki juu ya tatizo hilo,” alisema.
Alisema kuwa inasikitisha kuona biashara hiyo inafanyika kupitia bandari ya Dar es Salaam wakati kuna vifaa maalum vya ukagua mizigo.
Mwenyekiti huyo alisema kuwa pamoja na Rais Jakaya Kikwete kuomba Wizara ya Maliasili na Utalii kuwasilisha kwake iwapo wameshindwa kushughulikia suala hilo cha ajabu hadi sasa hawajatoa taarifa zozote.
“Rais Kikwete alipotembelea wizara hiyo aliwataka wawasilishe kwake suala hilo kama limeshindwa kushughulikiwa lakini hadi leo hawajawahi kutoa taarifa zozote,” alisema.
Lembeli alisema kwa kuwa mapendekezo waliyotoa yameshindwa kufanyika wameamua kumuachia Mungu suala hilo.
“Hayati Mwalimu Julius Nyerere alisema kuwa baba akidhihirisha kuwa ni mwizi lazima na watoto wake nao watakuwa wezi…hivyo mwenye kuweza kuwawajibisha wanaofanya biashara hii ni Mungu pekee,” alisema.

Tuesday, August 6, 2013

ZIARA YA WAZIRI MKUU WA THAILAND YINGLUCK SHINAWATRA KATIKA HIFADHI YA SERENGETI MKOANI MARA

Kamanda Ferdinad Mtui akiwa pamoja na wafanyakazi wa hotel ya 4 Season
         Bi Shinawatra akiwa ndani ya hotel ya 4 Seasons
           Eneno hili liko katika eneo la hotel ya 4 Seasons ambapo Tembo huja kunywa Maji

Saturday, August 3, 2013

TAZAMA PICHA YA FARU DUME ALIYEUAWA NA TEMBO DUME AUGUST MOSI MWAKA HUU

MZOGA WA FARU DUME AITWAYE LIMPOPO(11)ALIYEUAWA AGOSTI 1 MWAKA HUU NA TEMBO DUME ALIYEVUNJA UZIO WALIMOHIFADHIWA KATIKA ENEO LA NYABIKWABE KIJIJI CHA MAKUNDUSI KATA YA NATTA WILAYANI SERENGETI,FARU HUYO NI KATI YA WAWILI WALIOLETWA MWAKA 2007 NA KAMPUNI YA SINGITA GRUMETI RESERVES TOKA AFRIKA KUSINI.
 KUUAWA KWA FARU HUYO KUMETHIBITISHWA NA MKURUGENZI WA WANYAMA PORI TANZANIA PROFESA ALEXANDRE SONGORWA NA KUDAI KUWA WALIKUWA KWENYE ENEO MAALUM KAMA MRADI WA KAMPUNI HIYO,NA KUWA TEMBO DUME ALIPOINGIA KATIKA HIMAYA YA FARU HAO KULIPELEKEA FARU KUCHACHAMAA NA KUMFUKUZA NDIPO AKAMCHOMA KWA JINO LAKE SEHEMU YA MOYO NA KUMBANA SEHEMU YA NUNDU NA KUFA PAPO HAPO.
MBALI NA UJANGILI WA WANYAMA HAO PIA TEMBO NA FARU NI WANYAMA WASIOPATANA NA HUISHI KWA KUKWEPANA.

Thursday, August 1, 2013

WASHINDI WA TUZO ZA HABARI ZA TANAPA WAMALIZIA ZIARA YAO KWA KUTEMBELEA SHIRIKA LA UTANGAZAJI LA AFRIKA YA KUSINI (SABC)


Washindi wa Tuzo za Habari za TANAPA wakiwa nje ya jingo la Makao Makuu ya Shirika la Utangazaji la Afrika ya Kusini (SABC). Kutoka kushoto ni Festo Sikagonamo (ITV), Phinias Bashaya (Mwananchi), Lilian Shirima (TBC 1), Alex Magwiza (TBC Taifa), Maxmilian Bushoke mtanzania anayeishi Johannesburg na Albano Midelo (Nipashe).
Mkuu wa Idhaa ya Kiswahili ya  SABC Mike Arareng (kushoto) akiongea na washindi wa Tuzo za Habari za TANAPA walipomtembelea ofisini kwake.
 Meneja Uhusiano wa TANAPA Pascal Shelutete akifanya mahojiano katika Studio za SABC.
  Festo Sikagonamo wa ITV ambaye ni mshindi wa Tuzo za Habari za TANAPA akiwa katika studio za SABC.
 Lilian Shirima wa TBC 1 ambaye ni mshindi wa Tuzo za Habari za TANAPA akiwa katika studio za SABC.
Washindi wa Tuzo za Habari za TANAPA katika picha ya pamoja ndani ya chumba cha habari cha SABC na Mkuu wa Idhaa ya Kiswahili Mike Arareng( wa kwanza kushoto)  na mtangazaji wa SABC kutoka Kenya Christina ( wa tatu kushoto).