Friday, August 24, 2012

Mlima Kilimanjaro

Mahema ya watalii wanayotumia kulala wakati wanapotembelea vivutio vya utalii nchini

Kagasheki aongeza uwazi Malisili

Kagasheki aongeza uwazi Malisili


Na Mwandishi Wetu

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, amebadili taratibu za kuwapata wajumbe wa bodi mbalimbali zilozopo chini ya Wizara hiyo.

Taarifa iliyotolewa Dar es Salaam jana kwa vyombo vya habari na Msemaji wa Wizara hiyo, Bw. George Matiko, ilisema kuanzia sasa wajumbe wa bodi hizo watapatikana kwa njia ya ushindani badala ya kuteuliwa moja kwa moja na Waziri.

Alisema hivi sasa kuna bodi nane zilizopo chini ya Wizara hiyo ambazo zimemaliza muda wake au kukaribia kuisha.

Aliongeza kuwa, bodi hizo ni za Taasii za Mashirika ambazo ni Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori (TAWIRI), Taasisi ya Utafiti wa Misitu nchini (TAFORI), Makumbusho ya Taifa, Chuo cha Mafunzo na Usimamizi wa Wanyamapori (MWEKA).

Bodi nyingine ni Chuo cha Mafunzo ya Wanyamapori Pasiansi, Wakala wa Mbegu za Miti (TTSA) na Leseni za Utalii (TTLB).

Bw. Matiko aliwataka Watanzania wenye sifa za kuwa wajumbe wa bodi hizo, kupeleka maombi yao kwa Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii. Baadhi ya watu ambao wamezungumzia hatua hiyo, walisema ni nzuri na imezingatia uwazi kupata wajumbe hao.
Source: Majira

Thursday, August 23, 2012

Waziri Kagasheki


Waziri Kagasheki amng'oa mkurugenzi wanyamapori

MKURUGENZI wa Wanyamapori katika Wizara ya Maliasiali na Utalii, Obeid Mbangwa na wenzake wawili, wamefukuzwa kazi kwa kashfa ya kutorosha wanyama hai 136 wa aina 14 tofauti kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) usiku wa Novemba 26, 2010.
Hatua hiyo imefikiwa baada ya tume mbili zilizoundwa kuchunguza suala hilo bila kuhusisha wizara yenyewe, kumaliza kazi yake na kukabidhi ripoti kwa Waziri.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki alisema jana mjini Dodoma kuwa mbali na watuhumiwa hao, mtumishi mwingine wa wizara hiyo amevuliwa madaraka, wawili wamepewa onyo kali la maandishi na wawili uchunguzi dhidi yao unaendelea.
Mbangwa wakati wa kashfa hiyo ya kusafirisha wanyama hai wanaokadiriwa kuwa na thamani ya Sh170 milioni kwa ndege ya kijeshi ya Qatar, alikuwa Mkurugenzia Msaidizi Matumizi ya Wanyamapori.
Wengine waliotumuliwa kazi ni Simon Gwera na Frank Mremi waliokuwa maofisa Uwindaji wa Kitalii, Cites na Utalii wa Picha mkoani Arusha.
Mkurugenzi Msaidizi, Uendelezaji Wanyamapori, Boneventura Midala amevuliwa madaraka kutokana na kutochukua hatua kikamilifu za ulinzi ambazo zingeweza kuzia kutokea kwa utoshaji wa wanyama.
Wakati tukio hilo alikuwa kurugenzi Msaidizi, Sehemu ya Kuzuia Ujangili.
Katika hatua hizo, maofisa wanyamapori Daraja la pili wawili waliotekeleza maelekezo ya wakuu wao wa kazi yaliyo kinyume cha sheria wamepewa onyo kali la maandishi.
Kagasheki aliwataja kuwa ni Martha Msemo, Ofisa Leseni ya Uwindaji wa Kitalii, Cites na Utalii wa Picha Arusha na Anthonia Anthony ambaye ni Ofisa Leseni Ofisi ya  Uwindaji wa Kitalii, Cites na Utalii wa Picha Dar es Salaam.
Rungu la wizara hiyo pia limemwangukia Mkuu wa Kituo cha uwindaji wa kitalii, Cites na utalii wa Picha Arusha, Silvanus Ukudo aliyepewa onyo kali la maandishi kwa kushindwa kufuatilia kupata maelekezo ya mkurugenzi wa wanyamapori kuhusu mtumishi wake aliyekiuka sheria katika utoaji wa vibali.
Ukudo pia ameonywa kwa kushindwa kupeleka kwa katibu mkuu taarifa kuhusu mtumishi huyo ili achukuliwe hatua za kinidhamu.
Kagasheki alisema uchunguzi unaendelea dhidi ya watumishi wengine wawili, Mohamed madehele, Ofisa Matumizi Endelevu ya Wanyamapori na Mariam Nyallu, Ofisa wa kituo cha Uwindaji wa Kitalii, Cites na Utalii wa Picha Arusha.
Alisema kwa upande wa wafanyabiashara waliohusika katika kashfa hiyo, kesi inaendelea mahakamani, na kwa upande wa Qatar, Serikali inaendelea kusubiri majibu, japo ni kwa muda mrefu, kwa kuwa Serikali ya nchi hiyo imendelea kukaa kimya.
“Tumefanya kila jitihada, tumewasiliana kupitia Makao Makuu ya Cites, Geneva, Uswis, lakini Qatar pamoja na kukubali kupokea maombi yetu kutoka Cites, imekaa kimya,” alisema Kagasheki.
Kuhusu hatua zaidi dhidi ya watuhumiwa hao, Waziri Kagasheki alisema, “kwa kuwa imebainika walihusika na vibali vilisababisha hao wafanyabiashara wakamatwe walivitoa wao, suala hilo halijaishia hapo.”
Waziri huyo alisema atajitahidi kadiri ya uwezo wake kusimamia wizara hiyo ili kuhakikisha sheria na taratibu zinafuatwa.
“Sheria zipo nzuri, udhaifu mkubwa ni kwa watendaji wetu,” alisema.

Kauli ya Mbangwa
Alipotakiwa kuzungumzia suala hilo Mbangwa alisema hajui chochote.
Alisema hadi jana alikuwa hana taarifa za kufukuzwa kwazi hivyo hawezi kusema chochote hasa bila ushahidi.
“Unasema wamenifukuza kazi, ndo wametangaza hivyo? Mimi sina taarifa hizo na hivyo  siwezi kuelezea chochote”alisema Mbangwa.