Thursday, February 6, 2014

UMAKINI WAHITAJIKA OPERESHENI TOKOMEZA UJANGILI AWAMU YA PILI

Tokomeza ujangili awamu ya pili ifanyike kwa umakini zaidi

5th February 2014

Katuni
Juzi, serikali ilitangaza nia yake ya kuanza upya kwa `Operesheni Tokomeza Majangili' wakati wowote.

Tangazo hilo lilitolewa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, kwenye mkutano ulioikutanisha serikali, mabalozi wa nchi mbalimbali na taasisi za kimataifa.
Hata hivyo, Waziri Nyalandu hakutaja siku maalum ya kuanza kwa operesheni hiyo ya awamu ya pili.

Kwa mujibu wa Waziri Nyalandu, operesheni ya awamu hii itawakumba watu wote wanaojihusisha na  ujangili pamoja mitandao ya biashara za pembe za tembo na faru na kwamba itafanyika kwa nguvu kuanzia porini, ofisini hadi majumbani.

Aidha, alisema serikali imefanya maandalizi ya kutosha kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa opereshehi hiyo baada ya kusitishwa Oktoba 31, mwaka jana.

Operesheni ya mwaka jana ilisitishwa kutokana na malalamiko ya kuwapo kwa vitendo vya ukatili, mateso, mauaji ya wananchi wasio na hatia pamoja na upotevu wa mali zikiwamo fedha na mifugo.

Hali hiyo ilisababisha aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, kujiuzulu kutokana na shinikizo kubwa kutoka kwa wabunge na wenzake watatu kutenguliwa uteuzi wao.

Mawaziri ambao uteuzi wao ulitenguliwa na Rais Jakaya Kikwete ni pamoja na Shamsi Vuai Nahodha (Ulinzi na JKT), Dk. Emmanuel Nchimbi (Mambo ya Ndani ya Nchi) na Dk. David Mathayo David (Mifugo na Uvuvi).

Sisi tunaunga mkono operesheni tokomeza majangili iendelee kwa lengo la kulinda rasilimali za taifa hili kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho.

Hali kadhalika, tunakubaliana na Waziri Nyalandu kuwa katika operesheni ya safari hii, serikali itapambana kikamilifu na maadui wakubwa ambao ni watu wanaotumiwa kuua wanyamapori na wafadhili wa mitandao.

Aidha, tunaamini kwamba ahadi ya Waziri Nyalandu kwamba katika zoezi hilo, dosari zilizotokea awali zitaepukwa na kuhakikisha kuwa operesheni hiyo ya awamu ya pili inafanyika kwa weledi na ufanisi mkubwa.

Tunakubaliana na Waziri Nyalandu kuwa ni muhimu zoezi hilo likafanyika kwa weledi na ufanisi mkubwa ili kuepuka dosari zote zilizojitokeza katika operesheni ya kwanza ambayo kwa hakika iliitia doa serikali.

Tunafamu pia wazi kwamba hata operesheni ya kwanza, lengo lake lilikuwa ni jema lakini ilitiwa dosari na baadhi ya watendaji ama kwa makusudi, uzembe  au kwa kutojua athari ya walichokuwa wakikifanya.

Mathalani, tumeambiwa na mmoja wa askari aliyeshiriki awamu ya kwanza ya operesheni hiyo kwamba licha ya kuwa na nia nzuri ya kutokomeza ujangili, lakini usimamizi haukuwa mzuri kutokana na mamlaka zote za utawala zilizohusika kukosa uratibu.

Tunaamini kwamba operesheni ya sasa serikali itakuwa imejipanga vilivyo ili kuhakikisha kwamba dosari kama hizo na nyinginezo, hazijitokezi tena.

Tunataka operesheni ya awamu hii, ifanye kazi kwa lengo lililokusudiwa na pasipo kumuonea ama kumwandama mtu yeyote asiyehusika.

Kama itafanyika kwa weledi kama alivyoahidi Waziri mwenye dhamana, Nyalandu, kwa hakika kila mwananchi ataifurahia na kila mtu atakuwa tayari kutoa ushirikiano kwa watendaji watakaopewa jukumu hilo zito.

Na kwa msingi huo, tungependa zoezi hili liwe rafiki kwa wananchi badala ya kuwa adui.

Aidha, pamoja na hayo, vile vile tungeshauri askari wote watakaofanya kazi hiyo, walipwe posho zao stahiki na kwa wakati badala ya kubaki wakilalamika.

Askari wasipolipwa stahiki ya posho zao, ni rahisi kurubunika na wakajikuta wanajiingiza kufanya  vitendo kinyume na adidu zao za rejea ama kuwafisha mioyo ya kufanya kazi hiyo.

Hii inatokana na ukweli kwamba askari walioshiriki operesheni ya awali, bado wanaidai serikali kiasi cha Sh. bilioni 1.5.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment