Operesheni hii ianze kwa kutaja wabunge majangili
Posted Jumatano,Februari5 2014 saa 10:59 AM
Kwa ufupi
- Ni vyema tukakiri hapa kwamba awamu ya pili ya operesheni hiyo inaonyesha dalili za mafanikio hata kabla haijaanza, kwani Serikali inaonekana imejizatiti ipasavyo kwa kuweka utaratibu wa kuratibu na kutekeleza operesheni hiyo ili kasoro zilizojitokeza katika awamu ya kwanza zisirudiwe, pia kwa kuonyesha bayana kuelewa ukubwa wa tatizo na changamoto itakazopambana nazo wakati wa utekelezaji.
Serikali imetangaza rasmi kuanza upya kwa
‘Operesheni Tokomeza Majangili’, baada ya kuisitisha zaidi ya miezi
mitatu iliyopita kutokana na operesheni hiyo kukumbwa na matatizo ya
utekelezaji, ambapo vilitokea vitendo vya ukatili na mateso na kuwaacha
raia 13 na askari 6 wakiwa wamepoteza maisha. Matukio hayo ya
kusikitisha yalisababisha mawaziri wanne kupoteza nyadhifa zao
serikalini baada ya Kamati ya Bunge ya Maliasili na Utalii iliyoundwa
kuchunguza vitendo hivyo kuwasilisha taarifa yake bungeni.
Ni vyema tukakiri hapa kwamba awamu ya pili ya
operesheni hiyo inaonyesha dalili za mafanikio hata kabla haijaanza,
kwani Serikali inaonekana imejizatiti ipasavyo kwa kuweka utaratibu wa
kuratibu na kutekeleza operesheni hiyo ili kasoro zilizojitokeza katika
awamu ya kwanza zisirudiwe, pia kwa kuonyesha bayana kuelewa ukubwa wa
tatizo na changamoto itakazopambana nazo wakati wa utekelezaji. Hii ni
pamoja na kubuni mbinu na mikakati mipya ya utekelezaji na kuhakikisha
zoezi zima linaendeshwa kwa kuzingatia haki za binadamu.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu
alisema juzi wakati akitangaza kuanza kwa operesheni hiyo kuwa, Serikali
inatambua kwamba inapambana na watu wenye nguvu kubwa, ikiwa ni pamoja
na majangili na wafadhili wa mtandao wa biashara ya pembe za ndovu.
Alisema watawakamata kuanzia maporini, ofisini na hata majumbani. Hiyo
ni kauli nzito inayoashiria kwamba Serikali mara hii pengine inayo
dhamira ya kweli ya kutokomeza vitendo vya ujangili katika hifadhi za
Taifa, kwani operesheni iliyopita ilihujumiwa na baadhi ya viongozi wa
kisiasa na Serikali, ambao wao binafsi ama ndugu zao walikuwa
wakihusishwa na ujangili.
Miezi mitatu sasa baada ya kusitisha operesheni ya
awali, tuhuma bado zimepamba moto kwamba mikakati ya kuwang’oa mawaziri
ambao wizara zao zilihusika katika utekelezaji wa operesheni hiyo
zilisukwa na baadhi ya wabunge waliokuwa wakihusishwa na ujangili, huku
wengine kadhaa wakidaiwa kufanya hivyo kwa masilahi binafsi ya kisiasa.
Kutokana na Kamati ya Kudumu ya Bunge kuliambia
Bunge kwamba inayo majina ya wabunge na wanasiasa wanaotuhumiwa
kujihusisha na ujangili, wananchi wengi sasa wanataka operesheni hiyo
mpya isianze kabla majina ya watu hao hayajawekwa wazi, vinginevyo
operesheni hiyo itaonekana kama kiini macho.
Ni kwa sababu hiyo tunaitaka Serikali mara hii
isiwe na mzaha katika kuendesha operesheni ijayo. Kwa upande mmoja
iwaondoe wakulima na wafugaji ndani ya hifadhi, kwani nchi yetu inayo
ardhi ya kutosha nje ya hifadhi hizo kwa shughuli za kilimo na ufugaji.
Ukweli ni kwamba wananchi hao ndiyo mawakala wa majangili wakubwa
wanaomaliza tembo na maliasili nyingine. Pili ihakikishe makazi ya watu
yako mbali na hifadhi, kwani imegundulika wengi wa wafanyabiashara na
wanasiasa wanaoishi karibu na hifadhi hizo nchi nzima wanajihusisha na
ujangili na kwa kiasi kikubwa ndiyo waliofadhili njama za kuihujumu
operesheni iliyopita.
Wakati tukisubiri uundwaji wa Tume ya Kimahakama
kushughulikia ukiukwaji wa haki za binadamu wakati wa operesheni ya
awali, tunawataka wanasiasa, wakiwamo wabunge waiache Serikali itekeleze
wajibu wake katika operesheni itakayoanza hivi punde. Baadhi ya wabunge
waliopinga operesheni hiyo wanahusika na ujangili. Pengine ndiyo maana
wananchi hawana tena shauku ya kuona Tume ya Kimahakama ikiundwa.
No comments:
Post a Comment