Thursday, August 6, 2015

Ofisa Mhifadhi Wanyamapori atupwa jela miaka mitatu.



Ofisa Mhifadhi Wanyamapori atupwa jela miaka mitatu.


 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
Mahakama ya Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam, imemhukumu Ofisa Mhifadhi Wanyamapori wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Richard Nchasi, kulipa faini ya Sh. 900,000 au kwenda jela miaka mitatu baada ya kukutwa na makosa matatu.
 
Hukumu hiyo ilisomwa na Hakimu Mkazi, Juma Hassan, juzi  baada ya kupitia ushahidi uliotolewa na upande wa Jamhuri  na kumtia mshtakiwa hatiani kwa makosa hayo matatu.
 
"Kati ya makosa manne, mahakama imemtia hatiani mshtakiwa kwa makosa matatu ya kutumia nyaraka kwa lengo la kumdanganya mwajiri kwa kutoa hati za uwindaji wa wanyama," alisema Hakimu Hassan.
 
Hata hivyo, mahakama hiyo ilisema upande wa Jamhuri umeshindwa kuthibitisha shitaka la kuisababishia wizara hiyo hasara ya Dola 1,860 za Marekani (sawa na Sh. 2,976,000).
 
Awali, Mwendesha Mashitaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Leonard Swai, alidai kuwa katika tarehe tofauti kati ya Januari na Septemba, 2008, katika ofisi za wizara hiyo, jijini Dar es Salaam, mshtakiwa akiwa na wadhifa huo, aliandaa hati yenye namba 01235414 ya Agosti Mosi, 2008.
 
Inadaiwa kuwa hati hiyo ilikuwa ikionyesha kwamba Safari Club (T) Ltd, inatakiwa kulipa Dola 5,080 za Marekani (sawa na zaidi ya Sh. milioni 8.5) ikiwa ni ada ya uwindaji wa wanyama sita katika eneo la Kilwa South Mbemkulu, huku akijua si kweli.
 
Nchasi anadaiwa kuwa katika kipindi hicho, aliandaa tena hati yenye namba 01235410 ya Februari 21 mwaka 2008, kuonyesha kwamba kampuni hiyo inatakiwa kulipa ada ya Dola 6,580 (sawa na zaidi ya Sh. milioni 11) ya uwindaji wa wanyama watano katika eneo hilo.
 
Ofisa Mhifadhi huyo anadaiwa katika kipindi hicho, aliandaa tena hati yenye namba 01235415 ya Agosti Mosi, 2008, kuonyesha kampuni hiyo inatakiwa kulipa Dola 6,335 (sawa na zaidi ya Sh. milioni 10.6) ikiwa ni ada ya uwindaji ya wanyama saba kwenye eneo hilo.
 
Katika shitaka la nne, Nchasi anadaiwa katika kipindi hicho, jijini Dar es Salaam, akiwa mwajiriwa wa wizara hiyo, kwa kuelewa na kwa uzembe, aliisababishia wizara hiyo hasara ya Dola 1,860 (sawa na zaidi ya Sh. milioni 2.9) .
 
Hadi NIPASHE inaondoka mahakamani hapo jana 7:30 mchana mshtakiwa alikuwa hajalipa faini hiyo. 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment