Polisi akilinda sehemu ya shehena ya
meno ya tembo iliyokamatwa Dar es Salaam hivi karibuni. Picha ya Maktaba
Posted Ijumaa,Mei9 2014 saa 8:25 AM
Kwa ufupi
- Kati ya meno hayo 108 yaliyokamatwa katika matukio ya ujangili, 74 yalitoweka katika kituo cha polisi wakati 34 yalibadilishwa na meno madogo, tofauti na yale yaliyokuwa yamekamatwa yakihusishwa na kesi ya ujangili Na. 3/2009 na kesi nyingine ya uhujumu uchumi Na. 2/2010 ambazo zilikuwa zikiendelea mahakamani mkoani Lindi.
Dodoma. Meno ya tembo yaliyohifadhiwa kwa ajili ya vielelezo
mahakamani yalitoweka katika Kituo cha Polisi cha Kilwa mkoani Lindi.
Tukio hilo limenukuliwa katika
Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ikisema meno
makubwa 108 ya tembo na kilo 20 za meno mengine ya tembo yaliyokuwa
yamehifadhiwa kama kielelezo cha kesi za uhujumu uchumi, yamebainika kutoweka
kinyemela.
Ripoti hiyo iliyowasilishwa bungeni
juzi, imebainisha kuwa meno mengine makubwa ya tembo yaliyokuwa na uzito wa
kilo 498.3 yamebadilishwa kinyemela na meno madogo, hivyo kusababisha hasara ya
kilo 203.66 za meno ya tembo ambazo thamani yake haikufahamika.
CAG Ludovick Utouh katika ripoti
hiyo ya mwaka ulioishia Juni 30, 2013, amebainisha kuwa kumbukumbu katika Pori
Tengefu la Miguruwe zilionyesha kuwa katika kipindi cha kuanzia Juni 5 hadi
Juni 8, 2012 meno makubwa 108 yalikuwa miongoni mwa vielelezo kituoni hapo.
Kati ya meno hayo 108 yaliyokamatwa
katika matukio ya ujangili, 74 yalitoweka katika kituo cha polisi wakati 34
yalibadilishwa na meno madogo, tofauti na yale yaliyokuwa yamekamatwa
yakihusishwa na kesi ya ujangili Na. 3/2009 na kesi nyingine ya uhujumu uchumi
Na. 2/2010 ambazo zilikuwa zikiendelea mahakamani mkoani Lindi.
Pia ilibainika kuwa kilo 20 za meno
ya tembo ambayo yalikamatwa na kuhifadhiwa kama kielelezo cha majalada
KLM/IR/184/2009, KLM/IR/235/2009 na KLM/IR/567/2010 yalitoweka.
Gari la ujangili latoweka
Ukaguzi huo pia ulibaini kuwa gari
lililokamatwa likiwa kielelezo baada ya kukutwa na kilo 26 za meno ya tembo
yenye thamani ya Sh135 milioni liliondolewa kinyemela katika Kituo cha Polisi
Kilwa.
CAG katika ukaguzi huo alibaini
upungufu katika usimamizi wa meno ya tembo na nyara nyingine za taifa katika
chumba cha meno hayo Dar es Salaam na vituo vya mikoani.
CAG katika taarifa yake hiyo amesema
kutokana na kukosekana kwa kumbukumbu sahihi, meno ya tembo yanaweza kuibwa au
kupotea bila menejimenti kuwa na taarifa yoyote, hivyo ameishauri Serikali
kuhakikisha kunakuwa na udhibiti wa kutosha katika usimamizi wa nyara za
Serikali nchi nzima.
No comments:
Post a Comment