Thursday, May 8, 2014

Kesi dhidi ya Wachina uvuvi baharini yapigwa kalenda



Na Hellen Mwango
8th May 2014
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imeahirisha kesi inayowakabili raia wawili wa China, Hsu Tai na Zhao Hanquing, ya kufanya shughuli za uvuvi katika Bahari ya Hindi eneo la uchumi la Tanzania bila kibali hadi Mei 20, mwaka huu baada ya upande wa Jamhuri kudai kuwa upelelezi wake bado haujakamilika.

Kesi hiyo iliahirishwa jana na Hakimu Mkazi Mkuu, Warialwande Lema.

Wakili wa Serikali, Ofumad Mtenga, alidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na upande wa Jamhuri uliomba tarehe ya kutaja.

Hakimu Lema alisema kesi hiyo itatajwa tena Mei 20, mwaka huu na washtakiwa wataendelea kusota rumande.

Awali, upande wa Jamhuri ukiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Prosper Mwangamila, ulidai kuwa kati ya Januari 10 na Machi 8, mwaka 2009, washtakiwa walikutwa wakifanya shughuli za uvuvi katika Bahari ya Hindi eneo la kiuchumi la Tanzania.

 Katika shitaka la pili, mshtakiwa Tai ambaye alikuwa nahodha na Hanquing wakala wa meli ya Tawaliq 1 waliyokamatwa nayo, wanadaiwa kuharibu mazingira ya Bahari ya Hindi kwa kutupa uchafu eneo la kiuchumi la Tanzania.

Mwangamila alidai kuwa katika shitaka la tatu, kati ya Machi 8 na 11, mwaka 2009, Mombasa Kenya na Temeke jijini Dar es Salaam, wakala Hanquing alimsaidia mshtakiwa wa kwanza aliyekuwa anafanya shughuli za uvuvi bila kibali kuepuka kukamatwa na Jamhuri dhidi ya tuhuma zinazomkabili.

Kwa mujibu wa Sheria za Uhujumu Uchumi, kesi hiyo itasikilizwa na Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam upelelezi utakapokamilika, hivyo washtakiwa hawakutakiwa kujibu chochote.
 

No comments:

Post a Comment