Sunday, March 30, 2014

Meno ya tembo ya mil. 120/- yanaswa Ifakara



Na Beatrice Shayo
30th March 2014
Maofisa wanyamapori mjini Ifakara mkoani Morogoro wamekamata vipande 14 vya meno ya tembo pamoja na meno mengine mazima  manne  yote yakiwa na  thamani ya Shilingi  milioni 120.

Katika kamata hiyo, mtuhumiwa  Sudi Nyumbi  mfanyabashara wa jijini Dar es Salaam, alinaswa akiwa katika kijiji cha Katindiuka wilayani Kilombero akiwa   na vipande 14 vya meno  hayo yenye thamani ya Sh. 72,000,000 na  manne yenye thamani ya sh 48,000,000.

Akizungumza na NIPASHE wakati wa mahojiano,  Afisa wa Wanyamapori Kilombeo, Madaraka Amani alisema mtuhumiwa alinaswa  Jumanne  wiki hii  wakati huo akitoka ndani ya lango la kizuizi cha ukaguzi  la Kidatu akielekea Dar es Salaam.

Amani alisema askari wa wanyapori waliokuwa kwenye doria kijiji cha Katindiuka waliwaona watu wawili wakiwa kwenye baiskeli na walipokuwa wakiwafuatilia walikimbia na kuitelekeza baiskeli pamoja na meno hayo manne.

Hata hivyo, alisema meno hayo manne inaonyesha kuwa yalikuwa yamechimbiwa  ardhini  na kwamba walikwenda kuyafukua. Aliongeza kuwa kabla ya oparesheni tokomeza ujangili ulikuwa umeshika kasi lakini baada ya kusimamishwa unaanza tena.

Ofisa tarafa mmoja ambaye hakutaka jina lake litajwe, alisema wanafanya juhudi za kupambana na ujangili ila tatizo lililopo ni kukosekana kwa ushirikiano  kesi zinapokuwa mahakamani.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI


No comments:

Post a Comment