Monday, September 23, 2013

WATUMISHI TANAPA KUCHUNGUZWA


Tanapa kuchunguza tuhuma za ujangili
Na Daniel Mjema na Ibrahim Yamola, Mwananchi

Kwa ufupi
  • Shelutete alisema kutokana na majangili kubuni mbinu mpya kila siku, shirika limeunda kikosi maalumu (Rapid  Response Team) kwa ajili ya kukabiliana na uhalifu kwa haraka zaidi.
Arusha/Dar es Salaam. Shirika la Hifadhi za Taifa nchini (Tanapa), limeanzisha uchunguzi dhidi ya baadhi ya watumishi wake wanaotajwa kuwapo katika mitandao ya ujangili wa wanyama wakiwamo tembo.

Meneja Uhusiano wa Tanapa, Paschal Shelutete aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa, wale watakaothibitika kujihusisha na vitendo hivyo watachukuliwa hatua za kinidhamu na kisheria.

“Tumepokea tuhuma dhidi ya baadhi ya watumishi wetu kujihusisha na mitandao ya ujangili na uchunguzi dhidi yao umeanza ukishirikisha vyombo vya kiuchunguzi,” alisema Shelutete.

Shelutete alisema, tatizo la ujangili ni la kimtandao ukishirikisha majangili wa kimataifa wanaotumia ushawishi wa fedha na silaha za kisasa katika kuua tembo kwa lengo la kujipatia vipusa. “Wapo watumishi wamejikuta wakishawishiwa kujiunga na mitandao ya ujangili jambo ambalo ni kinyume kabisa na maadili ya kazi na hawa wakibainika kwa kweli hatuna msalie mtume,” alisema.

Shelutete alisema kutokana na majangili kubuni mbinu mpya kila siku, shirika limeunda kikosi maalum (Rapid  Response Team) kwa ajili ya kukabiliana na uhalifu kwa haraka zaidi.

Alisema uanzishwaji wa kikosi hiki umeonyesha mafanikio makubwa na kutoa mfano katika kipindi cha miezi sita iliyopita hakuna tembo aliyeuawa ndani ya Hifadhi za Manyara na Tarangire.

Shelutete alisema kwa miezi sita, majangili 1,116 walikamatwa katika hifadhi mbalimbali huku Hifadhi ya Taifa ya Serengeti (Senapa) pekee ikikamata majangili 248. 
Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Tembo nchini yaliyoandaliwa na UDSM kitengo cha Taasisi ya Kutathimini Rasilimali, Profesa Alexander Songorwa alisema wananchi ni wadau muhimu katika kampeni ya kupambana na ujangili.

No comments:

Post a Comment