Thursday, September 12, 2013

UROHO WA UTAJIRI CHANZO CHA UJANGILI WA TEMBO



na Zawadi Chogogwe

NAIBU Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, amesema kuwa kuongezeka kwa umaskini katika jamii nchini, kunasababishwa na baadhi ya watu wenye uroho wa kutaka utajiri wa haraka.
Nyarandu alitoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam katika mapokezi ya matembezi ya hiari yaliyoandaliwa na ‘African Wildlife Trust’.
“Uroho wa kutaka utajiri wa haraka umewafanya baadhi ya wafanyabiashara wakubwa na wadogo pamoja na watumishi wa umma kujiingiza katika ujangili,” alisema.
Aliongeza kuwa ujangili umechangia kupungua kwa idadi ya tembo kutoka 350,000 miaka ya 1960 hadi 110,000 mwaka 2009 ambapo idadi hiyo inaongezeka kila mwaka.
Alitoa mfano kuwa kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita (2010 -2012) jumla ya tembo waliouawa ni 1008 ambapo mwaka 2010 (259), mwaka 2011 (276) na mwaka 2012 (473).
“Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imekuwa ikipambana na majangili hao ndani na nje ya hifadhi za taifa ambapo kwa kipindi hicho wamewakamata majangili 4,066 wakiwa na bunduki 1,899 ambazo zilitaifishwa,” alisema.
Nyalandu alitoa wito kwa wanojihusisha na uovu huo kuacha mara moja vinginevyo watajikuta wamenaswa na vyombo vya dola na kufikishwa mahakamani.
Matembezi hayo yalikuwa ni ya kupiga vita ujangili unaofanywa nchini, ambayo yamefanyika siku 19 kutoka jijini Arusha hadi Dar es Salaam kwa kuwashirikisha watu 1,000.
Naye Mkurugenzi wa African Wildlife Trust, Patric Patel, alisema kuwa Desemba watu 150 watatoka Arusha kuja Dar es Saalam kwa kutumia baiskeli lengo lao likiwa ni kutunza hifadhi za taifa na kupambana na ujangili.




No comments:

Post a Comment