Juni 30,2014.
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu(LHRC)kupitia mawakili
na wanasheria wake kwa kushirikiana na Wasaidizi wa Kisheria na Haki za
Binadamu wilayani Serengeti Mkoa wa Mara wameanza wiki ya Msaada wa Kisheria
bure kwa wakazi wa wilaya hiyo.
Mwanasheria kutoka (LHRC )Rodrick Maro akiongea naWaandishi
wa habari mjini Mugumu alisema lengo ni kutoa msaada wa Kisheria bure kwa
jamii kuhusiana na masuala ya Kisheria,ushauri na kuwajengea uwezo Wasaidizi wa
Kisheria na Haki za Binadamu kuendelea kusaidia wananchi wasio na uwezo wa
kupata mawakili.
Alisema kuwa wilaya hiyo ni miongoni mwa wilaya ambazo
zimekuwa zikinufaika na huduma hiyo kutokana na kuwepo kwa wasaidizi wa
Kisheria na Haki za Binadamu ,hivyo wanakuwepo kwa wiki nzima wakitoa huduma
hiyo bure.
“Kuna matatizo mengi ya kisheria kwa wananchi hasa migogoro
ya ardhi,ndoa ,mirathi,ukatili wa kijinsia
na inapotokea watu wanakosa haki zao huchukua uamzi usiostahili ….hivyo
tunaona kuna hitaji kubwa la msaada wa
kisheria kwa jamii,”alisema
Mwenyekiti wa shirika la Wasaidizi wa Kisheria na Haki za
Binadamu wilayani Serengeti(WASHEHABISE)Samwel Mewama amesema huduma hiyo
ambayo imekuwa ikitolewa kila mwaka imesaidia wananchi wengi kujua haki zao na
kuzidai,njia ambayo inaimarisha msingi wa utawala bora.
Aidha Mewama amesema kuwa mwaka jana migogoro mingi ilihusu
mirathi,ukatili wa kijinsia,migogoro ya ardhi na ndoa ilipata ufumbuzi na
kuomba viongozi wahamasishe wananchi kujitokeza ili kupata ushauri utakao
saidia kutatua migogoro ambayo mingine inachangiwa na watendaji wa serikali
wasiojua hitaji la sheria.
Baadhi ya wakazi wa mji wa Mugumu wamesema utaratibu huo ni
mzuri na unawasaidia kwa kuwa watu wengi wanakosa haki zao kwa kutokujua sheria
na hawana uwezo wa kulipia mawakili ili kuwawakilisha.
Jumla ya wilaya 28 zilizo na Wasaidizi wa Kisheria na Haki
za Binadamu hapa nchini zinatarajiwa kufikiwa na huduma hiyo.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment