Tembo akikatiza katika barabara ndani ya hifadhi ya Taifa ya Serengeti(picha na Journo Tourism)
Na Peter Saramba, Mwananchi
.
Posted Juni21 2014 saa 8:54 AM
Na Peter Saramba, Mwananchi
.
Posted Juni21 2014 saa 8:54 AM
Kwa ufupi
- Kwa mujibu wa mpango wa Serikali, barabara hiyo ingepitia Mto wa Mbu-Engaruka-Loliondo- Kleins Gate-Serengeti-Mugumu-Nata na kuungana na ile ya Tarime-Musoma-Mwanza, hivyo kupunguza adha ya usafiri kwa wananchi wa maeneo haya ambao baadhi hulazimika kupitia Nairobi nchini Kenya.
Arusha. Mahakama ya Afrika Mashariki (EACJ), imeizuia Serikali ya
Tanzania kujenga barabara ya lami kupitia Hifadhi ya Taifa ya Serengeti,
ikieleza kuwa ujenzi huo utaathiri mazingira, maisha ya wanyamawwpori na
baoanuai ya hifadhi hiyo.
Katika hukumu iliyotolewa jijini
Arusha jana, jopo la majaji watatu wa mahakama hiyo wakiongozwa na Jaji
Kiongozi Jean Bosco Butasi, liliiamuru Tanzania kutotekeleza mradi wowote wa
ujenzi au ukarabati wa barabara hiyo utakaokuwa na madhara kwa mazingira na
baoanuai ya hifadhi ya Serengeti.
“Zuio la kudumu linatolewa dhidi ya
mdaiwa (Tanzania) kutekeleza mipango ya awali au pendekezo la ujenzi au
ukarabati wa barabara kwa kiwango cha lami kupitia Hifadhi ya Serengeti
itakayosababisha madhara kimazingira na baoanuai ya hifadhi hiyo,” inasema
sehemu ya hukumu hiyo.
Kila upande umeamriwa kubeba gharama
zake katika shauri hilo lililoshuhudia mgawanyiko kati ya taasisi na mashirika
yasiyo ya kiserikali, kwa yale ya Tanzania kuunga mkono ujenzi huo kwa madai
kuwa una faida kwa maisha na jamii inayoishi maeneo itakayopita barabara hiyo.
Kwa mujibu wa mpango wa Serikali,
barabara hiyo ingepitia Mto wa Mbu-Engaruka-Loliondo- Kleins
Gate-Serengeti-Mugumu-Nata na kuungana na ile ya Tarime-Musoma-Mwanza,
hivyo kupunguza adha ya usafiri kwa wananchi wa maeneo haya ambao baadhi
hulazimika kupitia Nairobi nchini Kenya.
Hukumu hiyo ilitolewa baada ya
Taasisi ya Africa Network For Animal Welfare (ANAW), ya jijini Nairobi, Kenya
kufungua kesi dhidi ya Serikali ya Tanzania kupinga ujenzi wa barabara hiyo
yenye urefu wa Kilomita 239, ikidai itaathiri mazingira, uhai wa wanyama na
baionuai wa Hifadhi ya Serengeti kwa kuongeza shughuli za kibinadamu.
Akisoma hukumu hiyo kwa niaba ya
majaji wenzake, Jaji Isaac Lenaola alisema Serikali ya Tanzania ina haki ya
kutunga sera na kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kwa ajili ya umma,
lakini sharti izingatie upembuzi yakinifu kuepuka athari za kimazingira na
baoanuai.
Jaji wa tatu katika jopo hilo ni
Jaji John Mkwawa kutoka Tanzania ambaye anakamilisha mkataba wake mwishoni mwa
mwezi huu. Nafasi yake tayari imejazwa na Jaji Fakih Jundu ambaye hadi uteuzi
wake Aprili 30, mwaka huu, alikuwa Jaji Kiongozi.
Hukumu hiyo inasema kuwa licha ya
haki ya nchi zote wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kupanga na
kutekeleza miradi na majukumu ya msingi kwa maendeleo ya wananchi, mipango hiyo
lazima izingatie hoja ya kidunia ya ulinzi na uhifadhi wa mazingira, maendeleo
endelevu, sheria na sera za kimataifa kuhusu mazingira na maliasili.
Mahakama imekubaliana na hoja za
walalamikaji waliokuwa wakiwakilishwa kwenye shauri hilo na wakili Saitabao Ole
Kanchory kuwa ujenzi wa barabara hiyo yenye urefu wa Kilomita 239, ungeathiri
mazingira na baionuai ya Hifadhi ya Serengeti nchini Tanzania na Maasai Mara
nchini Kenya kwa kuwa kungeongeza shughuli za kibinadamu.
Hukumu hiyo inasema kuwa licha ya
ukweli kwamba Serikali ya Tanzania ilipanga kuacha barabara yenye urefu wa
Kilomita 53 inayopita ndani ya hifadhi katika kiwango cha changarawe, bado
magari mengi yangepita kwenye barabara hiyo iwapo itajengwa kwa kiwango cha
lami.
Ujenzi wa barabara hiyo
ungetekelezwa ungekiuka ibara za 5(3), 8(1), 111(2) na 114 (1) ya mkataba wa
EAC, zinazozungumzia wajibu wa kila nchi mwanachama kupanga na kutekeleza sera
na miradi yote iliyo chini ya mamlaka na wajibu wao kwa kuzingatia ulinzi na
uhifadhi wa mazingira kwa faida na masilahi ya jumuiya nzima.
Desemba 10, 2010, ANAW ilifungua shauri namba 9 ya mwaka 2010 dhidi ya
Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Tanzania na kutaja madhara kumi
yatakayosababishwa na ujenzi wa barabara hiyo, ikiwamo kusumbua wanyamapori
katika maeneo yao ya asili, ongezeko la magari, kelele na uchafuzi wa hewa.Madhara mengine ni uchafuzi wa maji kutokana na kumwagika kwa mafuta ya magari yanapoharibika, ongezeko la uwindaji haramu, ongezeko la vifo vya wanyama kwa kugongwa na magari na kupotea kwa uoto wa asili.
Mwanasheria Mkuu aliyekuwa akiwakilishwa kwenye shauri hilo na Wakili Pascal Malata ambaye jana aliwakilishwa na wakili wa Serikali, Marcelino Mwamunyange alipinga maombi hayo akidai tayari Serikali ya Tanzania imechukua hatua kadhaa kuepuka madhara hayo ikiwamo kufanya upembuzi yakinifu wa madhara ya kimazingira na njia ya kuziepuka.
Awali, Serikali iliweka pingamizi ikidai ANAW haikuwa na haki kisheria kufungua madai hayo na wala Mahakama haikuwa na uwezo wa kuyasikiliza kwa sababu mradi huo unatekelezwa kwa kuzingatia sheria halali za nchi na wajibu wa Serikali wa kuleta maendeleo kwa wananchi wake. Pingamizi hilo lilitupwa na Mahakama.
Baada ya hukumu hiyo, Wakili Saitabao na wateja wake walielezea kufurahishwa na uamuzi wa Mahakama, waliodai ni ushindi mkubwa kwa wadau wote wa mazingira na ulinzi wa maliasili kwa ajili ya faida ya vizazi vya sasa na vijavyo.
“Ni siku kubwa kwa uhifadhi wa mazingira na wananchi wote wa EAC. Vizazi vijavyo vina haki ya kuona na kufaidi maliasili hii tuliyoirithi na tutachukua hatua za kisheria dhidi ya serikali yoyote ndani ya EAC kupinga uharibifu wa mazingira,” alisema Wachira Benson, katibu wa ANAW.
Wachira alisema kesi hiyo haikulenga kuzuia miradi ya maendeleo ya Tanzania, wala taasisi yake haichukii Watanzania, bali walitimiza wajibu wa kutetea mazingira kwa faida ya umma wote wa Afrika Mashariki, Afrika na dunia kwa jumla.
No comments:
Post a Comment