Wananchi wa kitongoji cha Uvinje
wakiwa kwenye kikao cha pamoja hivi karibuni kujadili uhalali wa kuendelea
kuishi katika eneo hilo linalodaiwa kuwa ni la hifadhi ya taifa ya
Saadan. Picha na Elias Msuya
Na Elias Msuya, Mwananchi
Posted Alhamisi,Mei22 2014 saa 12:44 PM
Posted Alhamisi,Mei22 2014 saa 12:44 PM
Kwa ufupi
Kitongoji hicho, ambacho ni kati ya
vitongoji nane vya Kijiji cha Saadani, kilitakiwa kiondolewe tangu mwaka 2005
baada ya hifadhi hiyo kupandishwa daraja kutoka pori la akiba na kuwa hifadhi
kwa mujibu wa Tangazo la Serikali Namba 281 la Septemba 16, 2005.
Hifadhi ya Taifa ya Saadani iliyopo
wilayani Bagamoyo Mkoa wa Pwani imeingia katika mgogoro na Kitongoji cha Uvinje
kilichomo ndani ya hifadhi hiyo.
Kitongoji hicho, ambacho ni kati ya
vitongoji nane vya Kijiji cha Saadani, kilitakiwa kiondolewe tangu mwaka 2005
baada ya hifadhi hiyo kupandishwa daraja kutoka pori la akiba na kuwa hifadhi
kwa mujibu wa Tangazo la Serikali Namba 281 la Septemba 16, 2005.
Hata hivyo wananchi wa kitongoji
hicho wanadai kuwa Rais Jakaya Kikwete alifika kijijini hapo kabla ya kuingia
Ikulu na kuwahakikishia kuwa hawataondolewa.
Maelezo ya wananchi
Wakizungumzia mbele ya watafiti wa
Taasisi ya Haki Ardhi iliyotembelea kijiji hicho hivi karibuni, baadhi ya
wananchi walisema kuwa kitongoji hicho kimekuwapo kwa muda mrefu na waliishi
bila bughudha hadi pori hilo lilipobadilishwa na kuwa Hifadhi ya Taifa.
Waliongeza kuwa, hata wakati Rais
Jakaya Kikwete alipokuwa mbunge wa Chalinze aliwatembelea mwaka 2005 na
kusisitiza kuwa hawataondolewa.
“Wakati hili ni pori la akiba
tuliishi vizuri tu na wazazi wetu walikuwa ni wafanyakazi wa pori. Lakini tangu
iwe hifadhi imekuwa taabu. Sasa tunafukuzwa wakati tumezaliwa hapa na wazazi
wetu wamezikwa hapa hapa,” anasema Hassan Akida.
Naye Zam Juma anaongeza kusema:
“Rais Kikwete alikuja hapa muda mfupi kabla hajagombea urais mwaka 2005. Tena
walikaa hapo (anaonyesha kwa kidole). Aliuliza maswali kuhusu huu mgogoro.
Wataalamu kutoka Tanapa walimweleza yote, likiwamo hilo tangazo katika gazeti
la Serikali.”
“Alisema, hawa watu
msiwatishe, msiwapige kwa bunduki, mahali hapa ni pao. Lakini tunashangaa bado
Tanapa wanatufuatilia tu. Malalamiko yetu yako wilayani, mkoani hadi Ikulu.”
Kuhusu uongozi wa Wilaya ya Bagamoyo
na Mkoa wa Pwani, Akida anasema awali walishapitisha azimio la kutokiondoa
kitongoji hicho, huku mkuu wa wilaya wa sasa, Ahmed Kipozi akidaiwa kupinga.
“Wakuu wa wilaya waliopita hapa kama
Grace Misaki, Hawa Ngulume, Selengo Mulengo na Magesa Mulongo na aliyekuwa mkuu
wa mkoa, Dk Christine Ishengoma (sasa mkuu wa mkoa wa Iringa) walisema hili
eneo ni letu. Waliagiza kwa barua kuwa tusihamishwe,” anasema Akida.
Hata hivyo mkuu wa Wilaya ya
Bagamoyo, Ahmed Kipozi na Mkuu wa mkoa wa Iringa, Dk. Christine Ishengoma
walipotafutwa kuzungumzia suala hilo walisita kutoa maelezo.
Wakati mgogoro huo ukiendelea wakazi wa kitongoji hicho wamekiri kumpokea
mwekezaji kutoka Uingereza aliyetajwa kwa jina la Bernard Bochad anayejiandaa
kujenga hoteli ya kitalii katika eneo hilo.Saadani wafafanua
Akizungumzia suala hilo, mhifadhi mkuu wa Saadani, Hassan Malungu amesisitiza kuwa kitongoji hicho kimo ndani ya hifadhi kinyume cha sheria na kwamba mambo ya siasa ndiyo yamechelewesha kukiondoa.
Alisisitiza kuwa sheria za hifadhi za Taifa haziruhusu makazi ya watu ndani yake.
“Kwa ufupi tu ukiangalia GN (Tangazo la Serikali) linaonyesha kuwa eneo lote la kitongoji cha Uvinje liko ndani ya hifadhi. Ni kweli lilikuwa eneo la watu ambao walikuwa watumishi wa pori la akiba tangu lilipoanzishwa mwaka 1968. Waliombwa kuondoka lakini waliendelea kuongezeka,” anasema.
“Hata wakati pori hili linabadilishwa kuwa hifadhi mwaka 2005, walikabidhi lakini wakasema kuna watu ndani. Sasa watu wa hifadhi wako makini zaidi na sheria, lakini kila wakitaka kuwaondoa kunakuwa siasa zinaingilia. Watu wakitaka madaraka ndiyo inakuwa hivyo… kwa hiyo siasa ndiyo zinachelewesha jambo hili,” alisema.
“Wakati nakuja hapa nimesikia kwamba wakati anafanya kampeni mwaka 2005, Rais Kikwete alipangiwa ratiba ya kutembelea kitongoji hicho. Lakini kwa kujua mgogoro huo, alisita ila hakuwa na la kufanya. Alipofika kule aliwaambia wakazi hao kuwa hata wakiondolewa, atahakikisha kuwa wanafaidika.”
Malungu aliongeza kuwa aliwahi kumuuliza mkurugenzi wake kuhusu msimamo wa Rais kwa mgogoro huo.
“Alinijibu kuwa Rais hajakataa watu kuondoka, ila anataka tumjengee kila mtu nyumba yake na tuwape fedha za kuanzia maisha. Sasa tukasema hii tutaifanyaje? Maana fidia ina taratibu zake, tutaibebaje hiyo?”
Anasema katika makubaliano, iliamuliwa kuwa walipwe fidia kwa taratibu za Serikali na isiwe chini ya Sh3 milioni kwa kiwango cha chini na kiwango cha juu kiwe Sh5 milioni, kulingana na eneo la mtu.
Hata hivyo, anasema licha ya kutekeleza utaratibu wa fidia bado wamegoma kuipokea mbali ya wachache kujitokeza.
“Tulifanya utaratibu ikiwa pamoja na kuandaa fidia. Watu walijitokeza pale kijijini kama 16 wakisema kuwa wako tayari. Siku ya kufanya tathmini tuliishirikisha Idara ya Ardhi, baadhi yao walikataa,” alisema Nguluma na kuongeza:
“Hiyo ilikuwa ni mwaka 2011 wakati wanakijiji walipowatishia wathamini, ikabidi mkuu wa wilaya awape ulinzi wa polisi. Hata hivyo ilishindikana kwa kuwa mwenyekiti wa kitongoji hakutoa ushirikiano wa kuonyesha maeneo ya watu.”
Anasisitiza kufuatwa kwa sheria za hifadhi licha ya kujua umuhimu wa uhusiano na wananchi wanaozunguka.
“Tuko makini sana kwenye sheria. Tangazo la Serikali likisema hivi, kwa kweli ndiyo tunavyofuata. Mipaka hii ndivyo ilivyowekwa, huwezi kulalamika tu. kama wanataka wapeleke bungeni ibadilishwe,” anasema.
Kauli ya Serikali
Licha mgogoro huo kuwepo kwa muda mrefu, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka amesema bado mgogoro huo haujafika mezani kwake bali anachokijua ni mgogoro kati ya hifadhi hiyo na shamba la Agro EcoEnergy.
“Hiyo kesi bado haijafika mikononi mwangu. Wailete tu niwasikilize. Ninachokijua ni mgogoro kati ya Saadani na Agro Ecoenergy ambao nilishasema kuwa watu wa hifadhi walikosea kubadilisha matumizi ya shamba la Razaba la Zanzibar na kuwa hifadhi na tumeshawaambia Wizara ya Maliasili na Utalii.”
Shamba la Razaba lililokuwa mali ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar lilichukuliwa na Serikali ya Muungano na kukabidhiwa kwa kampuni ya Agro Ecoenergy mwaka 2006.
Hata hivyo, kaimu mkuu wa Idara ya Ardhi, Maliasili na Mazingira wa Wilaya ya Bagamoyo, Clemence Mkusa alisema kuna kamati ya wilaya iliyokuwa ikiushughulikia mgogoro huo na kwamba tayari wameshapeleka taarifa katika Wizara za Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Wizara ya Maliasili na Utalii.
“Ni kweli huo mgogoro upo. Tunayo ramani inayoonyesha kuwa kitongoji cha Uvinje kiko ndani ya hifadhi na wanakijiji wanatakiwa waondoke. Tumeshapeleka mapendekezo yetu wizarani kwamba wafidiwe waondoke au wapewe hisa ya hifadhi hiyo. Tunasubiri majibu,” alisema Mkusa.
Naye mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Paul Sarakikya alikiri kuufahamu mgogoro huo na kusema kuwa kwa sasa kuna timu ya Waziri Mkuu iliyoundwa kushughulikia migogoro ya ardhi katika hifadhi zote nchini.
“Tusubiri tu hadi watakapotoa taarifa yao,” anasema Sarakikya.
Saadani ni hifadhi pekee ya Taifa
nchini na Afrika Mashariki yenye fukwe za bahari na inayotazamana na Bahari ya
Hindi na fukwe zake zinakutana na uoto wa asili wa nchi kavu.
Inapatikana katika mikoa ya Tanga na
Pwani. Uwepo wake ni matokeo ya pori la akiba la Saadani, ranchi ya Mkwaja na
sehemu ya kaskazini, sambamba na akiba ya msitu wa asili wa Zaraninge.
No comments:
Post a Comment