Thursday, April 3, 2014

MAONI: Hakimu huyu anakwamisha vita dhidi ya ujangili

   
  Posted  Jumatano,Marchi26  2014  saa 11:53 AM
Kwa ufupi
  • Pamoja na Serikali kuendesha vita hiyo kwa kutumia mbinu  mbalimbali, ikiwamo kuanzisha ‘Operesheni Tokomeza Ujangili’, vitendo hivyo bado vimeshika kasi ya kutisha na wanyamapori wanaendelea kuuawa.
Jana na leo tumechapisha habari zinazothibitisha kwamba vita dhidi ya vitendo vya ujangili hapa nchini havitafanikiwa iwapo vita hiyo haitachukuliwa kama suala mtambuka. Pamoja na Serikali kuendesha vita hiyo kwa kutumia mbinu  mbalimbali, ikiwamo kuanzisha ‘Operesheni Tokomeza Ujangili’, vitendo hivyo bado vimeshika kasi ya kutisha na wanyamapori wanaendelea kuuawa. Tunasema vita dhidi ya ujangili ni suala mtambuka, kwa maana ya vita hiyo kuhusisha taasisi nyingi na mihimili yote ya dola.
Tunazungumzia habari tulizochapisha jana na leo ambazo  zimeonyesha kwamba baadhi ya mahakimu nchini wamekuwa wakikwamisha vita hiyo kwa kutoa hukumu zinazokinzana na Sheria ya Wanyamapori namba 5 ya mwaka 2009 na ile ya makosa ya uhujumu uchumi. Baadhi ya hukumu dhidi ya makosa ya ujangili zimetolewa kinyume cha sheria.
Pengine tuzungumzie hapa mwenendo wa baadhi ya kesi za ujangili na uhujumu uchumi zilizofunguliwa katika Mahakama ya Wilaya ya Serengeti, mkoani Mara ambazo zimethibitisha kwamba mahakama hiyo, chini ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Amon Kahimba imekuwa ikitoa hukumu zinazokinzana na sheria husika. Moja ya hukumu hizo ni ile iliyohusu shauri namba Eco. 119/2012, ambapo washtakiwa walikiri kosa na kutiwa hatiani katika makosa matatu ya kupatikana na silaha na nyamapori ndani ya hifadhi yenye thamani ya Sh2.55 milioni. Washtakiwa hao walihukumiwa na hakimu huyo, Julai 29, 2013 kifungo cha miezi 18 jela au kulipa faini ya Sh100, 000.
Katika kesi ya pili namba Eco.55/2011 mbele ya hakimu huyo, washtakiwa wanne walitiwa hatiani kwa makosa matatu yaliyokuwa yakiwakabili. Makosa hayo ni kuingia hifadhini bila kibali, kukutwa na silaha na vipande vya nyama ya nyumbu, pembe ya pofu na mikia 13 ya nyumbu, vyote vikiwa na thamani ya Sh6.2 milioni. Katika hukumu yake ya Julai 31, 2013 kila mshtakiwa alihukumiwa kifungo cha miezi miwili gerezani na adhabu zote kwenda pamoja.
Katika kesi nyingine, mtuhumiwa mmoja alikamatwa Januari 17, 2013 na kushtakiwa kwa makosa matatu ya kukutwa na meno ya tembo yenye uzito wa kilo 46 yenye thamani ya Sh39.5 milioni. Hakimu huyohuyo alimruhusu mtuhumiwa kujidhamini mwenyewe baada ya kushindwa kukidhi masharti ya dhamana, kinyume cha kifungu cha 148(5)(C) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.
Sheria zilizopo zinachukulia makosa ya kuingia na kukutwa na silaha hifadhini kama makosa ya jinai, lakini watuhumiwa wanapokutwa na nyara aina yoyote na silaha za kivita, makosa hayo huwa ya uhujumu uchumi. Kwa maana hiyo, uamuzi wa Hakimu Kahimba unakinzana na vifungu vya 86(1) na (2)(ii) vya Sheria ya Wanyamapori namba 5 ya mwaka 2009, ikisomwa sambamba na kifungu cha 60 (2) cha Sheria ya Uhujumu Uchumi Sura ya 200 (RE:2002). Baada ya kutiwa hatiani washtakiwa walipaswa kwenda gerezani kwa miaka isiyopungua 20 na isiyozidi 30.
Tunachojaribu kuonyesha hapa ni mfumo mbovu wa Mahakama na Serikali ambao hauna taratibu za ufuatiliaji wa utekelezaji wa sheria zilizopo, ikiwa ni pamoja na mfumo dhaifu wa uendeshaji kesi katika ngazi za upelelezi, uendeshaji mashtaka na utolewaji wa hukumu. Jambo la kujiuliza ni kuwa, kama hukumu zinazotolewa zinakiuka sheria, kwa nini Jamhuri haikati rufaa katika mahakama za juu?


Mshtakiwa meno ya tembo ajidhamini mahakamani



 
Na Waandishi Wetu, Mwananchi

Posted  Jumatano,Marchi26  2014  saa 11:9 AM
Kwa ufupi
  • Rebeca Julius Mwita (32) anakabiliwa na mashtaka matatu ya kukutwa na nyara hizo za Serikali zenye uzito wa kilo 46 zikiwa na thamani ya Sh39.5 milioni aliruhusiwa kujidhamini mwenyewe kinyume cha kifungu cha  148 (5)(c) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.

Mtuhumiwa anayeshtakiwa katika Mahakama ya Wilaya ya Serengeti kwa makosa ya kukutwa na meno ya tembo, ameruhusiwa kujidhamini mwenyewe, Mwananchi limebaini.
Rebeca Julius Mwita (32) anakabiliwa na mashtaka matatu ya kukutwa na nyara hizo za Serikali zenye uzito wa kilo 46 zikiwa na thamani ya Sh39.5 milioni aliruhusiwa kujidhamini mwenyewe kinyume cha kifungu cha  148 (5)(c) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.  Mwita alikamatwa Januari 17, 2013 na alifikishwa mahakamani siku nne baadaye, Januari 23 ambako alifunguliwa mashtaka manne ya kukutwa na meno ya tembo mawili na vipande vinne vya meno hayo, kinyume cha sheria.
 Mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Amon Kahimba, Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Anesius Kainunura alidai kuwa makosa yanayomkabili mshtakiwa ni kinyume cha Sheria ya Wanyamapori namba 5 ya 2009 kifungu cha 4(d) jedwali la 1 na Kifungu cha 57 (1) na 60 (2) cha Sheria ya Uhujumu Uchumi iliyofanyiwa marekebisho 2002.
 Baada ya kusomewa mashtaka, mtuhumiwa alishindwa kukidhi masharti ya dhamana hivyo alirejeshwa rumande hadi Februari 4, 2013 wakati kesi yake ilipotajwa kwa mara ya pili.    Masharti aliyopewa ni kujidhamini mwenyewe kwa ahadi ya maneno ya Sh1 milioni, kuwa na wadhamini wawili ambao kila mmoja alipaswa kuweka bondi Sh2 milioni na sharti la tatu lilikuwa ni mdhamini mmojawapo kuwasilisha fedha taslimu Sh18 milioni.
Kesi hiyo iliendelea kutajwa bila mtuhumiwa kupata dhamana hadi Julai 9 na 23, 2013 wakati  wadhamini wawili ,akiwamo mume wake walijitokeza kumdhamini, lakini walishindwa licha ya kwamba wakati huo masharti yalikuwa yamelegezwa.
 Tofauti na masharti ya awali, kila mdhamini alitakiwa kutoa ahadi ya mali isiyohamishika yenye thamani ya Sh2 milioni pia mshtakiwa kujidhamini kwa fedha ya maandishi Sh500,000.
 Hakimu Kahimba aliwakataa wadhamini hao kwa maelezo kwamba hawakuwa na sifa, hivyo kuamuru mtuhumiwa arejeshwe rumande hadi Agosti 14, mwaka jana na kesi hiyo namba Eco.03/2013, ingetajwa kisha kusomwa kwa maelezo ya awali.
Dhamana ya ghafla
Katika hali isiyo ya kawaida, Julai 23, wakati waendesha mashtaka, karani na yeye (hakimu) akiwa ameshaandika tarehe ya kutajwa kwa kesi hiyo,  aliamuru shauri la mshtakiwa huyo lisomwe upya mahakamani.
 Uchunguzi umebaini kuwa baada ya shauri hilo kusomwa upya, Hakimu Kahimba aliruhusu Mwita ajidhamini mwenyewe kwa ahadi ya maandishi ya Sh500,000 na kuamriwa kufika mahakamani Agosti 14, 2013.
 Akizungumza na gazeti hili, Hakimu Kahimba alisema alitumia busara zaidi katika uamuzi wake, kutokana na mshtakiwa kukaa mahabusu kwa muda mrefu kwa kukosa wadhamini.
 “Mshtakiwa pamoja na kuomba alegezewe masharti ya dhamana...Bado alishindwa, kutokana na kukaa muda mrefu na uhakika wa kumpata upo....Wakati mwingine tunatumia hekima zaidi,” alisema Kahimba.
Hata hivyo, hakimu huyo alikiri kuwapo kwa matukio kadhaa ya watuhumiwa wanaoruka dhamana, huku chanzo kikubwa kikiwa ni kuwapa masharti nafuu yanayokinzana na hitaji la sheria kwa kesi za uhujumu uchumi.
 Mwendesha Mashtaka Mwandamizi Mkoa wa Mara, Lusekelo Samwel alisema uamuzi huo umekiuka kifungu cha 148 (5)(c) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya jinai (CPA) 1985 (RE:2002) ambayo  inabainisha wazi masharti ya dhamana kwa makosa hayo.
 “Kwa kosa ambalo mshtakiwa atashtakiwa nalo likiwa na thamani inayozidi Sh10 milioni...mshtakiwa anatakiwa pamoja na masharti mengine kutoa fedha taslimu ambazo ni sawa na nusu ya thamani ya kiasi anachoshtakiwa nacho ama thamani ya mali isiyohamishika kama dhamana kwa mshtakiwa,” alisema Samuel.
 Naye Wakili Juma Thomas alisema: “Hakimu hawezi kulegeza masharti ya dhamana eti kwa sababu mshtakiwa ameomba, maana kwa haya makosa dhamana yake inaongozwa na sheria, hali ilivyo inatia shaka,” alisema Thomas.  Jana gazeti hili lilikuwa na habari inayohusu mahakama hiyo kutoa hukumu ambazo zinakiuka sheria, huku hakimu akidai kuwa wanazingatia haki za watu ambao huwa wamekaa mahabusu kwa muda mrefu.



No comments:

Post a Comment