Dar
es Salaam.
Rais Jakaya Kikwete amesema Serikali imenuia kumaliza kabisa ujangili nchini,
ikiwa ni hatua ya kunusuru wanyama walio hatarini kutoweka katika hifadhi za
taifa.
Hakusita kusisitiza
kwamba, nia ya dhati ya Serikali ni kuhakikisha mkakati huo unakamilika,
japokuwa kumekuwa na changamoto zinazotokana na ukubwa wa hifadhi hizo na uhaba
wa vitendea kazi pamoja na askari wa wanyamapori.
Akizungumza wakati wa
kupokea magari 11 ya kisasa kwa ajili ya kusaidia operesheni ya kupambana na
ujangili kutoka kwa Shirika la Frankfurt Zoological Society (FZS) la Ujerumani,
Kikwete alisema tatizo hilo limekuwa la muda mrefu, lakini juhudi za
kulikomesha zinafanyika.
Alisema, pamoja na ukubwa
wa tatizo hilo, bado kuna tatizo la uhaba mkubwa wa wafanyakazi wanaotakiwa
kudhibiti majangili, ambapo kwa sasa kuna wafanyakazi 1,155 sawa na asilimia 24
tu ya mahitaji halisi ya wafanyakazi 4,000 wanaohitajika.
“Mwaka uliopita, Serikali
ilisimamia ajira ya wafanyakazi 449 na sasa kuna ajira ya wafanyakazi 500.
Kwa maana hiyo
tutafikisha wafanyakazi wapya 949 na kufanya mahitaji ya wafanyakazi wapya kuwa
4,000 zaidi ili kuwezesha utekelezaji wa majukumu kwa viwango vya kimataifa,”
alisema.
Kwa mujibu wa viwango
vilivyopo sasa, mfanyakazi mmoja anasimamia eneo la kilometa za mraba 169
ikilinganishwa na viwango vya kimataifa vya kilometa za mraba 25 kwa kila
mfanyakazi mmoja.
Rais Kikwete alisema kwa
sasa Serikali itaendelea kuajiri idadi hiyo ya wafanyakazi kila mwaka kwa miaka
mitatu ijayo ili kuhakikisha pengo lililopo linazibwa.
Alisisitiza kuwa, kampeni
dhidi ya ujangili ni suala la kimataifa na Tanzania au nchi zilizoathirika
hazitaweza kulikabili bila ushirikiano wa kimataifa.
Alisema upo ulazima wa
kuteketeza mitandao yote ya ujangili na kuwawajibisha ipasavyo watakaonaswa,
kwani kwa kufanya hivyo kutasaidia kulinda urithi huo wa dunia.
Ukosefu
wa vifaa
Akifafanua, Rais Kikwete alisema kuongeza
idadi hiyo ya wafanyakazi pekee haitakuwa na maana iwapo hawatakuwa na vifaa
maalumu vya kisasa vitakavyowawezesha kukabiliana ipasavyo na tishio la
ujangili.
Katika mkakati wa
maboresho hayo, Kikwete alisema wanafanya jitihada za kuongeza idadi ya magari,
kuongeza vifaa vya kisasa kwa ajili ya doria na vifaa vya mawasiliano, ambavyo
vinahitaji uwezo mkubwa wa kifedha ambao utaweza kutekelezwa na serikali kwa
kipindi kirefu iwapo haitapata msaada wa uwezeshaji kutoka kwa wadau.
Msimamo
wa Wizara
Akizungumzia msimamo na
mikakati ya Wizara ya Maliasili na Utalii, Waziri Lazaro Nyalandu alisema
kutokana na ukubwa wa tatizo, wanahitaji vifaa vya kisasa zaidi, ikiwamo
helikopta na ndege zisizo na rubani kwa ajili ya kufanya doria kwenye maeneo
yote ya mbuga na hifadhi za taifa.
Aliwatahadharisha
wafugaji wanaopenda kuingiza mifugo yao kwenye maeneo ya hifadhi, akiwataka
kuondoa mifugo yao mapema kwa kuwa katika operesheni hiyo hakuna atakayeachwa.
“Katika operesheni hii,
hakuna jangili wala mfugaji atakayeachwa iwapo atakutwa kwenye maeneo ya
hifadhi,” alisema.
Alifafanua kwamba, msaada
huo wa magari utapelekwa maeneo tofauti, matano kanda nane za Selous, mengine
matano Hifadhi ya Serengeti na moja Hifadhi ya Maswa.
Mwaliko wa vyombo vya
habari
Nyalandu alisema Wizara
yake imevialika vyombo vyote vya habari vya kimataifa kwa ajili ya kuja kupata
taarifa sahihi kuhusu kampeni dhidi ya ujangili zinavyotekelezwa ili kuepuka
ripoti za upande mmoja kwa ajili ya kuweka usawa.
Alisema hatua hiyo ilichukuliwa na wizara
yake walipokwenda kwenye mkutano maalumu na Rais Kikwete ulioandaliwa na mtoto
wa Mfalme wa Uingereza, Prince Charles kwa ajili ya kuangalia namna ya kulinda
wanyama walio hatarini kutoweka duniani, wakiwemo tembo na faru.
No comments:
Post a Comment