28/01/2014 | Posted by Shehe Semtawa Kitaifa
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imesema wafanyabiashara wanaoshirikiana na watendaji wa Bandari ya Dar es Salaam kupitisha makontena ya meno ya tembo watabainika baada ya kuanza kutumika kwa mfumo mpya wa kielektroniki bandarini hapo.
Wakizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam katika mafunzo mafupi yaliyohusu mfumo huo mpya, Naibu Kamishna wa TRA, Bellium Silaa, alisema mfumo huo umeanza kutumika katika bandari hiyo na utasaidia kupunguza utengenezaji wa nyaraka bandia unaofanikisha kupitisha makontena yenye bidhaa haramu yakiwemo meno ya tembo.
“Kwanza ni lazima tufahamu kuwa mfumo huu ni wetu, tumeubuni wenyewe na Wakorea wametusaidia kutengeneza, hivyo katika kupitisha mizigo yote lazima ionyeshe ni nani alihusika kufanya nini na wakati gani.
“Pia ni ngumu kutengeneza ‘export entry’ na hata mihuri haitakuwepo kwa maana hiyo hata utengenezaji wa nyaraka bandia utapungua,” alisema na kuongeza kwamba mfumo huo umegharimu dola milioni 11 za Marekani lakini unahitaji sana uadilifu wa watendaji wa bandari.
Kwa mujibu wa kamishna huyo, mfumo wa kielektroniki unaondoa mianya ya rushwa, unapunguza kufahamiana na hakuna msafirishaji au mwingizaji wa mzigo atakayeondoka na nyaraka mkononi bila kufanyiwa ‘scanning’ kwa kuwa kila kitu kitaendeshwa kwa mashine.
Alisema mfumo huo utaanza Machi mosi mwaka huu, ambapo mipaka na bandari zote zilizopo nchini zitahusishwa.
“Kama kuna mzigo utazidi basi ni lazima vitu vilivyomo ndani ya makontena hayo vipigwe mnada na taarifa za mnada unaohusu vitu hivyo vitawekwa ‘online’ ili wadau wote wafahamu,” alisema.
Alisema kuanza kwa mfumo huo kutahusisha idara mbalimbali zikiwemo Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Shirika la Viwango (TBS) na Mkemia Mkuu wa Serikali.
No comments:
Post a Comment