25th January 2014
Hata hivyo serikali inajipanga ili kuanza operesheni tokomeza mpya na safari hii ikifanyika kwa umakini zaidi kutunza wanyamapori, maeneo ya hifadhi na kumaliza ujangili kwa kuzingatia haki za binadamu .
Tokomeza ni moja ya mbinu za kumaliza ujangili nyingine ni zipi? Ujangili uliokithiri ni kielelezo cha kushindwa kumudu sekta ya wanyamapori ni changamoto gani zilizojikita eneo hilo? Ni nini hatma ya sekta ya wanyama pori na uhafadhi?
NIPASHE inazungumza na mtaalamu wa ekolojia tasnis maingiliano baina ya viumbe hai binadamu wanyama,mimea na mazingira wa Chuo Kikuu cha Dar es Saalaam, Profesa Raphael Mwalyosi kuhusu sekta ya uhifadhi, wanyamapori na hatma yake.
Profesa Mwalyosi alifanya shahada za uzamili na uzamivu kwenye taaluma ya ekolojia ndani ya mbuga ya wanyama ya Ziwa Manyara na pia bonde zima la ziwa Manyara.
Anaanza kuzungumzia juu ya sekta ya uhafadhi akitahadharisha kuwa licha ya Tanzania kuwa na nia njema ya kuhifadhi wanyama na mimea kwa ajili ya taifa na dunia serikali haina rasilimali watu, fedha, vifaa na teknolojia vya kutosha kuendeleza sekta hii.
Mwanaekolojia huyu anaeleza;“asilimia 30 ya ardhi ya Tanzania imetengwa kwa ajili ya hifadhi. Hiki ni kiasi kikubwa sana, kinaifanya kuwa taifa linaloongoza duniani kwa kuwa na maeneo makubwa yanayohifadhiwa.”
Tanzania ina ukubwa wa kilometa za mraba 945,000 ambazo asilimia 30 ni hifadhi, hivyo rasilimali hizo zinahitajika kuhifadhi maeneo hayo..
Kwa mujibu wa Wizara ya Maliasili na Utalii hifadhi inahusisha mapori tengefu, wanyama, misitu ya hifadhi , hifadhi za baharini, milima mabonde majengo /magofu, michoro ya mapangoni na mambo ya kale ambayo ni nyayo za mtu wa kale zilizoko Laetoli mkoani Manyara.
Pia uhifadhi unahusisha hifadhi 28, mbuga za wanyama karibu 14 kama Tarangire, Ngorongoro, Mikumi na Serengeti. Ipo pia michoro ya mapangoni iliyoko Kondoa, mabonde mengi mfano bonde la Ngongoro, Olduvai na Ruaha.
Yapo magofu ya Kilwa, Mji Mkongwe wa Zanzibar , hifadhi ya Mlima Kilimanjaro na hifadhi za bahari zilizoko Bara na Visiwani.
Profesa Mwalyosi anasema yapo maeneo mengi na vivutio vingi na kwamba uhifadhi huu na uendelezaji wake unahitaji fedha na nguvu kazi za kutosha.Hata hivyo rasilimali hizo zinategemea zaidi msaada wa wafadhili jambo linalozua maswali mengi kuhusu hatma ya sekta hii.
TEMBO NA MAZINGIRA
Mwalyosi amebobea kwenye eneo la tabia na mienendo ya tembo akieleza kuwa mwaka 1975 alishiriki kuwahesabu wanyama pori akifanya kazi kwenye mbuga ya Manyara.Sensa hiyo iliwezesha pia kujifunza uharibifu wa mazingira unaofanywa na tembo.
“Tembo wanatabia ya kuharibu mazingira wakishazaliana wakaongezeka wanaharibu misitu na mapori na kuharibu uoto wa asili.Ni tabia yao wanavyofanya popote wanapopatikana.”
Anasema wanatabia hiyo kutokana na idadi yao kuongezeka na mazingira kuwakataa kwani hakuna chakula cha kuwatosha na baada ya kyharibu mapori huondoka.
Anasema sensa ya wanyama iliyofanyika Manyara ilihesabu tembo karibu 700 lakini mwaka 1978 walikuwa wamechakaza mapori na karibu wote waliondoka. Hata hivyo miti ikistawi wanarejea tena kwenye makazi ya awali,
Tembo ni waharibifu wa misitu na mapori na hata maeneo ya vijiji jirani kwa hiyo iwapo watazaliana na kuongezeka watahitaji mapori makubwa ya kutosha ili kwenda na kuanzisha makazi. Kwa ujumla ni wanyama wanaotaka sehemu kubwa za kuishi na uangalizi ili wasiuawe kupata meno.
Profesa Mwalyosi ambaye anazijua tabia na changamoto za tembo, anasema swali kubwa la kujiuliza ni hili Tanzania iko wapi katika kutunza na kuzifanya rasilimali hizi nyingi zilizosambaa nchi nzima ili ziwe endelevu? Anaanzia na ujangili;
UJANGILI
Anasema changamoto kubwa ya uhifadhi wanyama hao tembo na faru ni ujangili na kwamba zipo aina mbili kuu za ujangili ambazo ni kuwaua wanyama pori ili kupata kitoweo na kuua tembo na faru kupata vipusa vya biashara ya kimataifa.
Anasema ujangili wa kitoweo hufanywa na baadhi ya jamii zilizo karibu na mbunga mfano Serengeti wananchi huwinda wanyama kupata nyama maarufu kama ‘kimolo’, hii hutokea wakati wanyama wakihama.
Anatahadharisha kuwa wanyama wanaouawa ili kupata kitoweo ni kiasi kikubwa kwa mwaka ukilinganisha na taarifa zinazokusanywa. Hata hivyo majangili hawa wa kitoweo hawaui tembo bali wanawinda mbogo, pundamilia, nyumbu na swala.
Ujangili mwingine ni wa kibiashara wawindaji haramu wanasaka meno ya tembo na vipusa vya faru, hawa wanaangamiza tembo na vifaru.
VICHOCHEO
Anasema zipo sababu kadhaa za ujangili huu wa kibiashara lakini mojawapo ni kupatikana kwa masoko ya uhakika na wanunuzi kutoka nchi za Mashariki ya Mbali kuwepo nchini ili kufanikisha uhalifu huo.
“Tangu zamani ujangili ulifanyika, kwa mfano kwenye mbuga za Ruaha na Manyara ulikuwa ukifika msimu fulani tembo waliwindwa na meno kukusanywa zikuwepo meli maalumu zilizofika bandarini kibiashara lakini pia zilichukua nyara hizo.”
SOKO LA UHAKIKA
Anasema zama hizo meno ya tembo yalikuwa na soko la msimu ilikuwa vigumu kuuza meno kwa haraka, kwa wakati mmoja na kupata fedha ilikuwa yasafirishwe hadi ughaibuni hadi soko litakapopatikana.
Profesa anasema nyakati hizi masoko yapo, wanunuzi wanapatikana hapa nchini hakuna kuhangaika na kusubiri meli za msimu .
Anaeleza kuwa kuwepo wafanyabiashara na wanunuzi wa meno haya hapa nchini kunachochea ujangili kwa kasi kubwa.
TEKNOLOJIA
Teknolojia na ubunifu inakuza pia ujangili kwa kuwa wengine wanayachakata meno ya tembo kutengeza vipande vidogo na kuvivaa kama shanga. Wengine huyasaga unga badala ya kubeba meno mazima kufanya hivyo kunarahisisha ujangili hivyo biashara kuwa nyepesi na usafirishaji kuwa rahisi na unaoweza kukwepa mitego.
ULINZI HAFIFU
Anasema ulinzi hafifu unaotokana na kukosa rasilimali watu kama askari wa wanyama pori, vifaa magari, helkopta, silaha na viona mbali kwenye hifadhi unaochangia ujangili kukomaa.
Tanzania inahifadhi nyingi, ndiyo inaongoza hapa duniani kwa kuhifadhi maeneo makubwa ya ardhi ambayo ni mbuga za wanyama, mapori ya akiba, misitu,mapori tengefu na maeneo oevu (wetlands).
Hata hivyo hakuna fedha za kutosha za kuyamudu na kuyaendeleza maeneo na rasilimali zillizoko ndani yake.
Ukweli ni kwamba mapori haya ni makubwa nchi ni maskini zinahitajika rasilimali nyingi na watu wa kuyatunza kama askari wa wanyama pori wa kuyasimamia na vitendea kazi na motisha na mishahara kwa ajili yao,kwa nchi hii maskini fedha hizo zinatoka wapi?
Kwa ujumla Tanzania haiwezi kusimamia na kutunza sekta hii kwa kuwa imehifadhi maeneo makubwa mno. “Nakumbuka kipindi fulani hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere alisema tunahifadhi kwa ajili ya ulimwengu mzima, akitarajia dunia itasaidia kutunza rasilimali hizi,”anakumbusha Profesa Mwalyosi.
Anasema yako baadhi ya mashirika ya kimataifa yanayochangia sekta ya wanyama pori kama Frankfurt Zoological Society ya Ujerumani, Shirika la Wanyama walio katika hatari ya kuangamia (CITIES) na lile la Umoja wa Mataifa la Utamaduni na Sayansi (UNESCO).
“Michango yao ni midogo haitoshi kwa sababu kuna maeneo makubwa sana na vipo vitu vingi wanyama wengi sana wanaohitaji kuhifadhiwa na kulindwa, ” anafafanua na kuongeza:
“Tanzania haina uwezo huo, nchi ilitegemea dunia isaidie lakini msaada unaotolewa ni kidogo kuna wakati Rais Jakaya Kikwete, alisema ukitoa eneo liwe urithi wa diunia watu wote wanafurahi lakini ina kuwa vigumu dunia kuchangia kikamilifu kuyaendeleza maeneo ya urithi yaliyotengwa kwa ajili ya wote.”
Makala hii itaendelea wiki ijayo kueleza nini kifanyike kuifanya sekta hii kuwa endelevu.
CHANZO: NIPASHE
Habari Zaidi
No comments:
Post a Comment