Monday, December 30, 2013

Mapigano wakulima, wafugaji yaua wanane

Na Augusta Njoji

30th December 2013

Hali si shwari katika Wilaya Kiteto mkoani Manyara kufuatia kuzuka kwa mapigano baina ya wakulima na wafugaji na kusababisha vifo na majeruhi.

Kufuatia hali hiyo, Chama cha Wakulima na Wafugaji wilayani Kiteto (Chawaki), jana kiliitisha mkutano kujadili mapigano hayo na kusaka suluhu.

Baada ya mkutano huo kuanza, zilizuka vurugu huku wafugaji jamii ya Kimasai wakiwapinga viongozi wa chama hicho na kumlazimu Mkuu wa Kituo cha Polisi wa wilaya hiyo, Foka Dinya, kuuvunja mkutano huo kwa madai kuwa kuna hali ya uvunjifu wa amani.

NIPASHE ilishuhudia vurugu hizo ambazo chanzo chake ni kugombea eneo la hifadhi ya Mbuga ya Embloi Murtangosi na polisi kufyatua mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wakazi hao pia walilalamikia kunyanyasika huku wakimtuhumu Mbunge wao, Benedict Ole Nangoro, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi kwa madai kuwa amekuwa akichochea vurugu hizo kwa kuwabagua wakulima.

Walidai kuwa tangu Desemba 16, mwaka huu, vurugu hizo zimesababisha watu watano kupoteza maisha na wengine 10 kujeruhiwa.

Mmoja wakulima hao, Ramadhani Machaku, alidai kuwa wanasikitishwa kuwapo kwa vitendo hivyo na maisha yao yapo hatarini, lakini hakuna hata kiongozi mmoja ambaye amejitokeza kutafuta suluhu.

Alidai kuwa watu wanachinjwa kama kuku na kupoteza maisha yao na wafugaji kwa kuwavamia usiku wakiwa wamelala huku serikali mkoani humo ikiwataka wakulima kuondoka katika eneo la hifadhi, hatua ambayo alidai haiwatendei haki.

“Mpaka sasa hatuelewi hatma yetu licha ya uongozi wetu kuwapo hapa, hatuelewi wanafanya nini, lakini jambo moja nasema hivi hatutaondoka katika maeneo haya hadi kieleweke kwani kilimo ndicho kinachotusaidia kuishi,” alisema Machaku.

Naye dada wa mmoja wa marehemu ambaye aliuawa na katika mgogoro huo, Sada Ally, alisema kuwa mdogo wake alichomwa mkuki tumboni wakampeleka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, lakini alifariki dunia wakati akipata matibabu.

“Mgogoro huu ni wa wakulima na wafugaji, wafugaji wamekuwa hawataki wakulima walime, bali wao wachunge mifugo, hali hii imesababisha mdogo wangu apoteze maisha mpaka sasa,” alisema.

Aliongeza: “Serikali naomba itusaidie jamani wakulima wanateseka Kiteto, wakulima hawana mtu wa kuwaangalia, viongozi wao wote wa Kiteto ni Wamasai, hivyo wanakuwa upande wa wafugaji moja kwa moja na hawawasikilizi wakulima,” alidai Sada.

Msemaji wa Chawaki, Hassan Losioki, alisema kuwa tamko la chama hicho ni kuitaka Serikali irejeshe ardhi vijijini kwa mujibu wa Sheria namba nne na tano ya Mwaka 1999 ili wananchi wafanye maamuzi ya matumizi ya ardhi wao wenyewe.

Pia Losioki alimuomba Rais Jakaya Kikwete, aingilie kati mgogoro huo ambao ni wa muda mrefu takribani miaka minane sasa.

“Mgogoro huu umekuwa ni wa muda mrefu kwani umedumu kwa miaka minane sasa ambapo kila mwaka kumekuwapo na mauaji ya watu hasa unapofika msimu wa kilimo, “ alisema Hassan.
Hata hivyo, alisema kuwa vijiji vitano kati ya saba vilivyopo katika hifadhi hiyo vya Nati, Emaliti, Engusilisidani, Lotepesi na Kimana, vimejitoa katika hifadhi hiyo kupitia mikutano halali ya serikali za vijiji husika.
Mkuu wa Polisi wa wilaya hiyo, OCD Foka Dinya, alithibitisha kuwa hali si shwari Kiteto na kwamba wanawatafuta wanaohusika na mauaji.

“Mimi siwezi kuzungumzia mauaji yalitotokea kuanzia tarehe 16 mwezi huu nilikuwa likizo, ninachojua ni mfugaji mmoja aliyeuawa ambaye alizikwa jana nikiwa tayari nimerudi kazini,” alisema na kuongeza:

“Hata hivyo, sitazungumza sana kwani mimi si msemaji wa Jeshi la Polisi mkoani kwetu…Leo (jana), kuna watu wawili ambao wamejeruhiwa katika vurugu hizi na wamepelekwa hospitali na polisi bado wanaendelea na doria kutokana na hali kutokuwa shwari.”

Akijibu tuhuma hizo, Ole Nangoro alisema kuwa hahusiki na uchochezi wa vurugu hizo na kufafanua kuwa hifadhi ya Embloi Murtangosi imesajiliwa kama hifadhi ya kijamii.

“Na ipo katika vijiji saba vya Wilaya ya Kiteto, wananchi wa eneo hilo walisema wataitumia ardhi hiyo watu 133,000 kwa ajili ya hifadhi ya jamii na baadaye eneo hilo lilivamiwa na watu wengi toka nje ya wilaya hiyo,” alisema.

“Kwa mwaka 2003, 2004 na 2006 waliondolewa, mwaka 2007 watu 50 walikwenda Kiteto Mahakama ya Ardhi kufungua kesi dhidi ya Halmashauri wakashinda na baadaye halmashauri ilikata rufaa na ikashinda, hivyo mahakama ikamteua `court broker' aliyesimamia uendeshaji wa kuwaondoa watu waliovamia katika eneo hilo,” alisema Naibu Waziri huyo.

Alibainisha kuwa mgogoro huo unachochewa na wale wanaopingana na sheria.
Kuhusu madai ya kuwapo kundi la Wamasai katika boma lake lililopo eneo la Olpopong’i ambao wanatuhumiwa kuhusika na mauaji na wamekodiwa kutoka Kenya, Ole Nangoro alisema vyombo vya dola viende kuwatafuta nyumbani kwake na wawakamate lakini akasisitiza kuwa hakuna kitu kama hicho. 




No comments:

Post a Comment