Saturday, September 28, 2013

JWTZ KUSAKA MAJANGILI WATEMBO NA FARU

                     
               Na Mwandishi wetu


RAIS Jakaya Kikwete ametangaza kuwa ataliamrisha Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kuongoza mapambano dhidi ya ujangili wa tembo na faru na ukataji haramu wa miti kwa shughuli za biashara ambao umefikia kiwango kikubwa nchini.
Alisema kuwa sekta ya utalii nchini sasa imeanza kutishiwa na uvunaji wa wanyama hao na biashara haramu ya meno ya tembo na faru, na kwamba tishio hilo ni kubwa kwa sababu sekta hiyo inachangia kiasi cha asilimia 17 katika mapato ya taifa na inaajiri watu 300,000.
Rais Kikwete alitangaza uamuzi huo juzi wakati alipozungumza kwenye mkutano wa viongozi wa nchi na serikali kuhusu biashara haramu ya wanyama na bidhaa zake pamoja na biashara haramu ya bidhaa za miti na mbao jijini New York, Marekani.
Aliuambia mkutano huo, ulioandaliwa na Rais Ali Omar Bongo Ondimba wa Gabon na Serikali ya Ujerumani kwenye Makao Makao ya Umoja wa Mataifa kuwa mwaka 1960, Tanzania ilikuwa na tembo 350,000 lakini kutokana na ujangili idadi hiyo ilishuka hadi 110,000 ilipofika mwaka 2009.
Kuhusu faru, Rais Kikwete alisema kuwa mwaka 1974 walikuwepo 700 na sasa wako chini ya 100 kwa sababu ya vitendo vya kijangili.
“Katika miaka ya 1980 na 1990 wakati wa kilele cha ujangili katika mikonga ya wanyama, tulilazimika kutumia jeshi kutuliza hali hiyo. Tuliona matokeo mazuri na tulikuwa na utulivu wa aina fulani.
“Lakini katika miaka minne iliyopita, tumeshuhudia kuongezeka kwa vitendo vya ujangili kwa ari na kasi mpya. Kwa mfano kati ya mwaka 2010 na Julai, 2013, zaidi ya tembo 1,386 waliuawa nchini,” alisema.
Rais Kikwete aliongeza kuwa wamechukua hatua kali za kupambana na ujangili ikiwa ni pamoja na kurekebisha sera, sheria na kanuni.
Aliongeza kuwa wamesaini mikataba mbalimbali ya kimataifa ya kupambana na ujangili huu.
“Vile vile, tumechukua hatua za kukamata majangili na hata kukamata silaha zinazotumika katika ujangili. Kati ya mwaka 2010 hadi katikati ya mwaka huu, majangili 5,189 wametiwa mbaroni na silaha 1,952 zimekamatwa.
“Isitoshe vipande 3,788 vya meno ya tembo vyenye uzito wa kilo 10,756 vilikamatwa nchini. Nimeamuru JWTZ kukabiliana na hali hiyo na naamini kuwa tutapata mafanikio makubwa zaidi katika operesheni inayoandaliwa,” alisema.
Wakati huo huo, Rais Kikwete alisema kuwa mifuko ya hifadhi nchini itaendelea kuchangia maendeleo kwa kugharamia miradi mbalimbali, lakini kwa namna ya kuilinda ili serikali isije kuua ‘bata wa dhahabu anayetaga mayai ya dhahabu’.
Rais alisema kuwa misaada inayotolewa na Shirika la Misaada ya Maendeleo la Marekani (MCC) ni ya aina yake duniani kwa sababu wanufaika wakubwa wanapewa uhuru wa kuamua ni miradi gani ndani ya nchi igharamiwe na misaada hiyo.
Vile vile, Rais Kikwete alizitaja sekta kubwa ambako wawekezaji kutoka Marekani wanaweza kuwekeza mitaji yao kama njia ya kuongeza uwekezaji wao katika Tanzania, na hivyo kusaidia kukuza kwa kasi zaidi uchumi wake.

No comments:

Post a Comment