Thursday, June 27, 2013

TANZANIA: Viboko wa ajabu wasiojulikana kwa watalii



Viboko wakijidai majini 

Licha ya Bwawa la Mto Nyange kuwa na vivutio vya asili hakuna mkakati wowote wa kutangaza eneo hilo la utalii na kuiingizia Serikali mapato.
Ni kilometa 123 kutoka Kilwa Masoko yalipo makao makuu ya Wilaya ya Kilwa. Katika wilaya hiyo kuna Kijiji cha Makangaga na kuna kivutio kizuri cha utalii kwa mfano viboko wa ajabu ambao wanatii amri mbalimbali.
Wakazi wa kijiji hicho chenye wakazi wapatao 1525 wanaotokana na makabila ya Wamwera, Wangindo, Wamakonde, na Wamachinga ambao wanalitumia eneo hilo kama kivutio cha utalii ambalo linachangia pato la wakazi wa eneo hilo mpaka taifa kutokana na watalii wa ndani na nje.
Viboko wa ajabu
Katika Kijiji cha Makangaga, kilometa tisa kutoka kijijini hapo, kuna Mto Nyange uliosheheni viboko wa ajabu ambao wana tabia ya ‘kucheka’ na kutii amri zinazotolewa, hakika ukifika unajua wamefundishwa, ni fursa nzuri ya utalii kama itatumiwa vyema.
Majira ya usiku viboko hao wanapenda kutembea kando ya maeneo yao kwa ajili ya kujipatia vyakula na sehemu kubwa wanakula majani na pia wana tabia za ziada.
Zaidi ya miaka 100 iliyopita mto huo uliotengeneza bwawa na haukuwa na kiboko hata mmoja, wakazi wa maeneo hayo walitumia bwawa hilo kwa shughuli za uvuvi na mahitaji ya maji kwa kazi za kawaida.
Mkazi wa eneo hilo Yahaya Selemani Engema anaeleza chanzo ni mkazi mmoja aliyetajwa kwa jina la Kimombo ambaye alikuwa mvuvi hodari kwenye bwawa hilo.
Lakini siku moja alipokwenda kuvua hakurejea na historia kuanzia hapo baada ya wananchi kuona kiboko mmoja kwenye bwawa hilo.
“Ndugu zake baada ya kusubiri kwa siku sita wakiamini atarejea, waliamua kwenda bwawani hapo kwa nia ya kumtafuta, walimwita kwa kutumia lugha ya kabila la Wamachinga, ajabu baada ya kutokea Kimombo kama walivyotarajia alitokea kiboko ambaye alicheka kama ishara ya kuitika, kutokana na hali hiyo ndugu wa familia ya mvuvi huyo waliamini ndugu yao alizama kwenye bwawa hilo na kubadilika kuwa kiboko ambao wanatabia ya kucheka,”anasema Omari Yanda mmoja wazee maarufu kijiini hapo.
Kila mwaka hivi sasa inakadiriwa kuwa wanafikia zaidi ya viboko 300, na kwamba wanatii amri ya ukoo wa Kimombo.
“Familia iliyoshikilia wanyama hao ni ya Kimombo wanarithishana kwa kuwa kiboko wa kwanza alitoka katika familia hiyo, wageni wanaofika kuwaona viboko hao huwaita viboko hao kwa kutumia jina la Kimombo ndipo viboko hao hujitokeza wakicheka,” anasema Yanda.
Miongoni mwa maajabu ya viboko hao ni kuwa wana uwezo wa kujitokeza pindi wanapohitajika kwa maana wakitakiwa wajitokeze wadogo wataibuka wadogo na wakitakiwa wajitokeze wazee watajitokeza wazee wote waliomo bwawani.

 Pia tabia nyingine ya ajabu ni kutokuwa waharibifu wa mazao ya wakulima ambayo viboko hao hawafanyi uharibifu wowote wa mazao ya wakulima yanayozunguka katika bwawa hilo.

Vilevile hawana madhara kwa binadamu yeyote hata wakikutana ana kwa ana au wavuvi wanaovua kwenye bwawa hilo hawaguswi au kuwadhuru. Wavuvi wanaendelea na shughuli za uvuvi bila kujeruhiwa wala kuuliwa na viboko hao.
Licha ya uwapo wa viboko hao pia eneo hili lina kivutio kingine kikubwa ambacho ni msitu mnene uliotokana na miti ya asili na kusababisha eneo hilo kuwa tulivu na mahali pazuri pa kujipumzisha iwapo patawekewa mazingira rafiki hii inatokana na kutokatwa miti.
Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Makangaga, Muhidini Mkungula alisema eneo hilo lipo kwenye usimamizi wa kijiji na uongozi wa kijiji umeweka mkakati wa kuulinda msitu huo na kuwachukulia hatua kali wale wanafanya uaharibifu wa kukata miti.
“Tunashukuru wananchi wetu wanatoa ushirikiano katika utunzaji wa msitu huu”anasema Mkungula.
Tambiko la jadi
Wenyeji wa vijiji hivyo kwa imani ya viboko hao wanalitumia eneo la bwawa la Mto Nyange kwa shughuli za jadi na kila mwaka huenda siku maalumu na wenyeji hao wanapika pombe za kiasili na kucheza ngoma za kiasili, kunywa pombe hiyo na kufanya tambiko kubwa kwa lengo la kuomba mizimu.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Makangaga Said Ali Kilete anasema licha ya tambiko hilo la kila mwaka pia wananchi wa maeneo yanayozunguka eneo hilo wanatumia eneo hilo kwa maombi maalumu akitolea mfano iwapo kunajitokeza tatizo la ukame wananchi wanaomba mvua kwa kutumia eneo hilo.
Serikali inasemaje?
Licha ya eneo hili kuwa na vivutio bado Serikali haina mkakati wowote wa kulifanya kuwa ni moja ya maeneo yatakayochangia pato la taifa au kuwa eneo la kitalii.
Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Abdalah Ulega anaeleza kwamba licha ya kupata taarifa ya eneo hilo, wilaya haina mkakati wowote wa kuendeleza na kulitangaza na kuwa sehemu maalumu ya utalii.
Ofisa Uhusiano wa Bodi ya Utalii nchini, Godfrey Tengeneza anaeleza kwamba Bodi ya utalii inatambua eneo hilo na maeneo mengine wilayani Kilwa yenye vivutio ambavyo ni vya kitalii na kwamba hivi sasa bodi hiyo imeanza kuvitangaza vyanzo hivyo.

  Anasema wameanza kutangaza vyanzo hivyo lakini hivi sasa eneo hawajaweka mkakati wote wa kutangaza viboko wa ajabu.

“Kilwa ina vivutio vingi ambavyo vinatosha kuwa vya kitalii na hivi sasa bodi inaanza kuviwekea mikakati ili vivutir watalii,”anasema Tengeneza.

No comments:

Post a Comment