Thursday, August 23, 2012

Waziri Kagasheki


Waziri Kagasheki amng'oa mkurugenzi wanyamapori

MKURUGENZI wa Wanyamapori katika Wizara ya Maliasiali na Utalii, Obeid Mbangwa na wenzake wawili, wamefukuzwa kazi kwa kashfa ya kutorosha wanyama hai 136 wa aina 14 tofauti kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) usiku wa Novemba 26, 2010.
Hatua hiyo imefikiwa baada ya tume mbili zilizoundwa kuchunguza suala hilo bila kuhusisha wizara yenyewe, kumaliza kazi yake na kukabidhi ripoti kwa Waziri.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki alisema jana mjini Dodoma kuwa mbali na watuhumiwa hao, mtumishi mwingine wa wizara hiyo amevuliwa madaraka, wawili wamepewa onyo kali la maandishi na wawili uchunguzi dhidi yao unaendelea.
Mbangwa wakati wa kashfa hiyo ya kusafirisha wanyama hai wanaokadiriwa kuwa na thamani ya Sh170 milioni kwa ndege ya kijeshi ya Qatar, alikuwa Mkurugenzia Msaidizi Matumizi ya Wanyamapori.
Wengine waliotumuliwa kazi ni Simon Gwera na Frank Mremi waliokuwa maofisa Uwindaji wa Kitalii, Cites na Utalii wa Picha mkoani Arusha.
Mkurugenzi Msaidizi, Uendelezaji Wanyamapori, Boneventura Midala amevuliwa madaraka kutokana na kutochukua hatua kikamilifu za ulinzi ambazo zingeweza kuzia kutokea kwa utoshaji wa wanyama.
Wakati tukio hilo alikuwa kurugenzi Msaidizi, Sehemu ya Kuzuia Ujangili.
Katika hatua hizo, maofisa wanyamapori Daraja la pili wawili waliotekeleza maelekezo ya wakuu wao wa kazi yaliyo kinyume cha sheria wamepewa onyo kali la maandishi.
Kagasheki aliwataja kuwa ni Martha Msemo, Ofisa Leseni ya Uwindaji wa Kitalii, Cites na Utalii wa Picha Arusha na Anthonia Anthony ambaye ni Ofisa Leseni Ofisi ya  Uwindaji wa Kitalii, Cites na Utalii wa Picha Dar es Salaam.
Rungu la wizara hiyo pia limemwangukia Mkuu wa Kituo cha uwindaji wa kitalii, Cites na utalii wa Picha Arusha, Silvanus Ukudo aliyepewa onyo kali la maandishi kwa kushindwa kufuatilia kupata maelekezo ya mkurugenzi wa wanyamapori kuhusu mtumishi wake aliyekiuka sheria katika utoaji wa vibali.
Ukudo pia ameonywa kwa kushindwa kupeleka kwa katibu mkuu taarifa kuhusu mtumishi huyo ili achukuliwe hatua za kinidhamu.
Kagasheki alisema uchunguzi unaendelea dhidi ya watumishi wengine wawili, Mohamed madehele, Ofisa Matumizi Endelevu ya Wanyamapori na Mariam Nyallu, Ofisa wa kituo cha Uwindaji wa Kitalii, Cites na Utalii wa Picha Arusha.
Alisema kwa upande wa wafanyabiashara waliohusika katika kashfa hiyo, kesi inaendelea mahakamani, na kwa upande wa Qatar, Serikali inaendelea kusubiri majibu, japo ni kwa muda mrefu, kwa kuwa Serikali ya nchi hiyo imendelea kukaa kimya.
“Tumefanya kila jitihada, tumewasiliana kupitia Makao Makuu ya Cites, Geneva, Uswis, lakini Qatar pamoja na kukubali kupokea maombi yetu kutoka Cites, imekaa kimya,” alisema Kagasheki.
Kuhusu hatua zaidi dhidi ya watuhumiwa hao, Waziri Kagasheki alisema, “kwa kuwa imebainika walihusika na vibali vilisababisha hao wafanyabiashara wakamatwe walivitoa wao, suala hilo halijaishia hapo.”
Waziri huyo alisema atajitahidi kadiri ya uwezo wake kusimamia wizara hiyo ili kuhakikisha sheria na taratibu zinafuatwa.
“Sheria zipo nzuri, udhaifu mkubwa ni kwa watendaji wetu,” alisema.

Kauli ya Mbangwa
Alipotakiwa kuzungumzia suala hilo Mbangwa alisema hajui chochote.
Alisema hadi jana alikuwa hana taarifa za kufukuzwa kwazi hivyo hawezi kusema chochote hasa bila ushahidi.
“Unasema wamenifukuza kazi, ndo wametangaza hivyo? Mimi sina taarifa hizo na hivyo  siwezi kuelezea chochote”alisema Mbangwa.




No comments:

Post a Comment