Waziri wa Maliasili na Utalii,
Lazaro Nyalandu.
Waziri wa Maliasili na Utalii,
Lazaro Nyarandu, amesema serikali itaendelea kuboresha uhusiano wake na
viongozi wa dini katika kupambana na wimbi la vitendo vya ujangili nchini.
Akizungumza katika mkutano na
viongozi hao jijini Dar es Salaam jana, Nyarandu alisema ongezeko hilo
limesababisha madhara makubwa kwa serikali kupoteza rasilimali za wanyama
ambayo ni tegemeo kwa mapato.
Alisema kundi la majangili limeingia
katika mbuga mbalimbali za wanyama kama Tarangire, Manyara, Mikumi, Ngorongoro
na kusababisha idadi kubwa ya wanyama kuuliwa bila sababu.
Alisema viongozi hao wana nafasi
kubwa ya kufichua kundi hilo la majangili kupitia nyumba za ibada yakiwamo na
maeneo mengine ya shughuli za kijamii.
Kadhalika, aliwataka viongozi hao
kuweka agano la pamoja katika kutatua changamoto hiyo hasa kwa kukubaliana ni
jinsi gani ya kuzilinda rasiliamali hizo.
“Tunachofanya ni kuweka mpango
madhubuti endelevu ila jukumu kubwa litakuwa kwa viongozi wa dini, kwa sababu
wao wanakutana na watu wengi kwa nyanja mbalimbali tofauti na serikali,”
alisema Nyarandu.
Alisema ili kukabiliana na ongezeko
hilo, wizara yake imeongeza kikosi cha askari wa wanyamapori kitakachodhibiti
majangili mara na baada ya kufanya uhalifu.
Pia, aliwashauri waweke mfumo
endelevu kwa kushirikiana na serikali kwa pamoja kuangalia namna ya kukabiliana
na changamoto hiyo, ingawa ni kubwa kuliko serikali inavyodhani.
Askofu wa Kanisa la Anglikana
Dayosisi ya Dar es Salaam, Valentino Mokiwa, alisema kutokana na mtandao
wa ujangili kukua kwa kasi nchini, huku ukiongoza kuwa mstari wa mbele
kuchangia nyumba za ibada, ni jukumu la viongozi kuwa makini na jambo hilo
maana ni dhambi mbele za Mungu.
“Nafikiri katika hili hata sisi
viongozi wa dini tunahusika kushtakiwa mbele za Mungu, kwa sababu tumekuwa
tukiwapa kipaumbele katika nyumba za ibada kwa kisingizio cha kutoangalia
matendo yake bali michango yao,” alisema Askofu Mokiwa.
Aliishairi serikali kutoa adhabu kwa
majangili inayofanana na ile ya mauaji mengine kwani kitendo hicho ni ishara
mbaya mbele za Mungu.
“Kumuua mnyama ni dhambi kama dhambi
nyingine, hivyo tunapendekeza adhabu zao ziangaliwe kuanzia shina, kiungo na
msambazaji,” alisema.
Naye Sheikh wa Mkoa wa Dar es
Salaam, Alhad Mussa Salum, aliwataka Watanzania kuwathamini wanyama kama viumbe
vingine vilivyoumbwa na Mungu.
Alisema Watanzania wengi wamekuwa
wakipotoshwa na waganga wa kienyeji kwa kuwatumia wanyama pori hasa kwa vitendo
vya kikatili kama sehemu ya kafara kwa mihadi mbalimbali ya
maradaka na kwamba usafirishaji wake hadi uuaji wake ni wa kikatili.
“Mungu ameruhusu mnyama auliwe kwa
sababu maalum, hivyo kuwatumia au kuwaua wanyama kinyume cha maandiko ya Mungu
ni dhambi,” alisema Sheikh_ Salum.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment