12th February 2015
Na Editor
Katuni.
Siyo siri tena kwamba ule uliokuwa
unaangaliwa kama muungano wa hiari (coalition of the willing) miongoni mwa nchi
wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), sasa unaonekana kukolezwa moto
ili Tanzania ipate madhara zaidi.
Kenya, Uganda na Rwanda kwa muda
sasa zimekuwa zikishirikiana katika miradi mikubwa ya miundombinu, kama vile
kusaini mikataba ya matumizi na upanuzi wa bandari, ujenzi wa reli na hata
bomba la mafuta miongoni mwake, huku Tanzania ikiwa ni mwanachama mwenzao
kwenye Jumuiya hiyo, ikitengwa.
Awali juhudi hizi zilionekana kama
kuitaka Tanzania kukubaliana na malengo ya nchi hizo ya kutaka pamoja na mambo
mengine kuharakisha shirikisho la kisiasa la Jumuiya hiyo, lakini pia zikitaka
Tanzania kufungua milango yake zaidi kwa wakazi wa Afrika Mashariki kutumia
ardhi ya Tanzania kwa uwekezaji.
Hatua za hivi karibuni kabisa za
kulazimisha Tanzania kwenda mwendo wa nchi hizo, ulichukuliwa na serikali ya
Kenya kwa kupiga marufuku magari ya kubeba watalii ya Kitanzania kuingia katika
viwanja vya ndege vya Kenya na katika mbuga za wanyama kwa kile kilichoelezwa
na wadadisi wa mambo kuwa ni ‘jeuri’ ya Tanzania ya kuendelea kuufunga mpaka wa
Tanzania na Kenya eneo la Bologonja ambao unatenganisha mbuga ya Taifa ya
Serengeti na ile ya Kenya, Masai Mara.
Mpaka huu ulifungwa wakati wa
utawala wa Mwalimu Nyerere miaka ya sabini kwa sababu za kimsingi za kiuchumi.
Hadi kesho, sababu hizo bado zina nguvu na watawala wote watatu waliomfuata
Mwalimu, Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na sasa Jakaya Kikwete, wameendelea
kutambua na kuheshimu uamuzi huo wa kizalendo uliofikiwa na serikali ya Mwalimu
ambayo asiliani haikuwa na mchezo kuhusu rasilimali za taifa.
Mbuga ya Taifa ya Serengeti ni moja
ya vivutio vya utalii vinavyoaminika na kuheshimika sana duniani. Mbuga hii ina
ukubwa wa kilometa za mraba 14,763 ikiambaambaa hadi kuingia Kenya ambako
huitwa Masai Mara. Uotoa na mfumo wa ikolojia ya Serengeti kitaalam
inachukuliwa kwa pamoja na Masai Mara yenye ukubwa wa kilometa za mraba 1,510.
Kwa maneno mengine Kenya inamiliki asilimia 10 tu ya uoto na ekolojia ya
Serengeti.
Kwa bahati mbaya, wanyama hawatambui
mipaka iliyowekwa na binadamu, ndiyo maana wanyama wa Serengeti husambaa eneo
lote la Serengeti na Masai Mara kama eneo lao moja la kujidai. Hii ndiyo
inafanya Serengeti na Masai Mara kuwa kitu kimoja hata kama ni mbuga ambazo
zinamilikiwa na nchi mbili tofauti.
Katika mazingira kama hayo, ni jambo
lisilofaa na kwa kweli lisilokubalika kwamba moja ya nchi hizi mbili inataka
kugeuza nyingine ngazi ya kunufaika tu na sekta ya utalii kwa kutaka kuwako kwa
mifumo ambayo kisayansi na katika utaalam wa uhifadhi wa wanyama pori
haukubaliki na haina tija kwa ustawi na uendelevu wa hifadhi hiyo.
Mgogogoro wa Kenya kutaka mpaka wa
Bologonja ufunguliwe ni wa kujipendelea. Mosi, kwamba watalii waingie Kenya,
walale Kenya, walipe fedha Kenya, lakini mchana wavuke tu mpaka wakitokea Masai
Mara eneo dogo ambalo kwa hakika litakuwa na wanyama wachache, waingie
Serengeti na kunufaika na wanyama kisha warejee Kenya jioni na Tanzania ibaki
mikono mitupu. Hii siyo haki. Huu ni uporaji wa mchana kweupe.
Mbili, kutaka kufungua mpaka wa
Bologonja ni kinyume cha taratibu za uhamiaji. Kokote duniani hakuna utaratibu
wa kuwa shughuli za binadamu ndani ya mbuga ya wanyama pori. Kwamba sasa
Bologonja iwe ni kituo cha forodha, uhamiaji na hivyo watu wapite tu hapo kama
wanavyopita vituo vingine vya mpakani, huu ni utaratibu mpya ambao Tanzania
haiwezi kuukubali.
Kwa maoni yetu sababu zilizotolewa
miaka ya sabini za kuufunga mpaka wa Bologonja, bado zingali na nguvu na ni za
msingi. Tanzania haina sababu ya kulazimisha Kenya kuruhusu magari ya kubeba
watalii kuingia nchini humo, lakini tunajua na tuna hakika kwamba mtalii
anayetaka kujionea maajabu ya Serengeti hatazuiwa na mbinu hizi ovu za kukataa
magari kuingia viwanja vya ndege.
Ni rai yetu kwamba kama taifa
tuimarishe miundombinu yetu, tujipange kwa makini zaidi kujitangaza kuwa tuna
vivutio bora zaidi vya utalii siyo Afrika Mashariki na Afrika tu, bali duniani.
Tuwaambie watalii waje washuhudie wanyama kwa wasaa wao, bila kubugudhiwa na
utitiri wa magari na hoteli mbugani.
Kwa uungwana kabisa tuwajibu Kenya
kwa kufanya mambo yetu kisayansi, kwa kuwa walichokifanya ni kukiri dhahiri
kwamba wana nia ovu dhidi yetu, wanamezea mate Serengeti na kwa kuwa wanyama ni
wetu na kipindi kikubwa cha mwaka hukaa Tanzania, basi wajipange upya kwani
neema hii ni baraka ya Mungu kwa Tanzania asiliani Kenya hawawezi kuichukua.
Muda wa kutishwa na kulazimishwa na watu wenye maslahi binafsi dhidi ya taifa
letu umepita siku nyingi, tusonge mbele. Tunataka kuwa na viongozi imara na
wenye fikra pevu katika kusimamia na kuongoza shughuli zote za maliasili ili
kuimarisha sekta ya utalii mara dufu.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment