Saturday, January 11, 2014

GOMBE: Hifadhi yenye sokwe wanaoishi kama binadamu


TANZANIA imejaliwa kuwa na hifadhi zenye vivutio mbalimbali  wakiwamo wanyama, ndege, maua, milima, vijito, fukwe nzuri na maporomoko ya maji.
Hifadhi zilizopo ni Mlima Kilimanjaro, Gombe, Rubondo, Katavi, Ruaha, Kitulo, Tarangire, Mkomazi, Saadani, Mikumi, Udzungwa, Manyara, Serengeti, Mahale, mji wa Arusha na Saanane.
Hifadhi ya Taifa ya Gombe iliyopo Kigoma ilianzishwa mwaka 1943, ikiwa kama pori la akiba, baada ya kuwaondoa wananchi waliokuwa wakiishi ndani ya eneo hilo mwaka 1942.
Lengo hasa la kutenga eneo hilo la Gombe na kuanzishwa kwa hifadhi ni kuhakikisha wanyama adimu kama sokwe mtu wanaofanana kitabia na kiumbo na binadamu wanaendelea kulindwa na kudumu kwa ajili ya vizazi vijavyo.
Gombe ina ukubwa wa kilometa za mraba 52; ni hifadhi ndogo kuliko zote nchini na ina umaarufu mkubwa kutokana kuwepo kwa wanyama aina ya sokwe.
Pia sehemu kubwa ndani ya hifadhi hii ni milima, mabonde na misitu minene ya kijani kwa mwaka mzima.
Hifadhi ya Gombe inapakana na vijiji vya Mwamgongo, Mtanga, Bubango, Chankele na Mtaraganza na haipo mbali na Burundi upande wa kaskazini, ambapo ni mwendo wa takriban saa moja na nusu kwa usafiri wa boti za injini.
Sokwe hawa kwa hapa nchini si kwamba wanapatikana katika Hifadhi ya Gombe pekee, bali wanapatikana pia katika Hifadhi ya Mahale na Kisiwa cha Rubondo katika Ziwa Victoria, Mwanza.
Ndani ya hifadhi kuna nyani wa kijivu, mbega mwekundu, kima mwenye mkia wa bluu na chotara, pia katika hifadhi hiyo kuna pongo, ndege wa aina mbalimbali na nyoka wakubwa wakiwamo chatu.
Sifa nyingine ya hifadhi hii ni kuwa kando kando mwa Ziwa Tanganyika na vyanzo vya maji vinavyotiririsha maji ndani ya Ziwa Tanganyika.
Historia inaonyesha kuwa mwaka 1960 mtafiti maarufu wa wanyama duniani, Jane Goodall, raia wa Uingereza alifika Gombe na kuvutiwa na uhifadhi wa sokwe; hivyo alianza kufanya utafiti wa wanyama hao adimu.
Utafiti wa Jane ulizaa matunda ambapo mwaka 1965 kilianzishwa kituo cha utafiti wa sokwe na mazingira yake na miaka mitatu baadaye, yaani mwaka 1968 eneo la Gombe lilipandishwa hadhi na kuwa hifadhi kamili ya taifa.
Shughuli za utalii zilianza mwaka 1978, ikiwa ni pamoja na kupata wageni mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi, hivyo kuliwezesha taifa kuongeza pato kwa ajili ya maendeleo.
Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Gombe, Noelia  Myonga, anasema huwezi kuizungumzia Hifadhi ya Gombe bila ya kulitaja Ziwa Tanganyika, kwa sababu ya ukaribu wake na hifadhi hiyo na pia sehemu ya ziwa hilo ipo ndani ya hifadhi.
Myonga anasema Ziwa Tanganyika linachangia katika utalii kwa sababu lina aina 400 za samaki, ambapo wengi wao hawapatikani kwingine.
Anaitaja sifa nyingine ya ziwa hilo kuwa ni la kwanza duniani kwa ujazo wa maji baridi, lina takriban kilometa za ujazo 18,900, sawa na asilimia 17 ya maji baridi duniani.
Myonga anasema hadi sasa hifadhi ina sokwe 106, Hifadhi ya Mahale ina sokwe 700 na Hifadhi ya Rubndo ina sokwe 30, hivyo kuifanya Tanzania kuwa na sokwe 836.
“’Wakati Hhifadhi ya Gombe inaanzishwa ilikuwa na sokwe 150 lakini kutokana na haya mambo ya ujangili wa miaka ya nyuma, magonjwa na kuzeeka, kumesababisha sokwe kupungua hadi kufikia 106,” anasema.
Anazitaja shughuli zinazofanywa na watalii wanapofika  katika Hifadhi ya Gombe  kuwa ni pamoja na safari ndefu ya kutembea kwa miguu kuangalia sokwe mtu na wanyama wengine ndani ya hifadhi hiyo.
Pia kuogelea na matembezi mafupi katika fukwe safi na nzuri za Ziwa Tanganyika, kutazama maporomoko ya maji (Kakombe na Mkenke) na kupanda katika kilele cha mlima kiitwacho Janes Peak.
Shughuli nyingine ni kutembea katika msitu mnene wa asili na kingo za Bonde la Ufa la mashariki.
Myonga anataja mafanikio ambayo nchi imeyapata kutokana na hifadhi hiyo ya kuwa ni pamoja na kupokea wageni 1,707 kwa mwaka 2010/2011, ambao waliliingizia taifa sh 252,283,100 na mwaka 2011/2012 walipokea wageni 1,809 walioingiza sh 309,391,000.
Mhifadhi huyo anasema sehemu kubwa ya mapato hayo yamekuwa yakiwanufaisha wananchi hasa wanaoishi jirani na hifadhi.
“Tumekuwa tukishirikiana na vijiji vinavyozunguka hifadhi katika kutekeleza miradi mbalimbali inayoibuliwa na serikali ya vijiji, miradi hiyo ni kama kujenga madarasa, madawati, nyumba na ofisi za walimu.
“Unajua miradi kama hii inatufanya tuwe na uhusiano mzuri na wananchi wanaoishi kuzunguka maeneo ya hifadhi, sababu wanaona manufaa ya kuwa na hifadhi, hivyo hutusaidia katika kuitunza,” anasema Myonga.
Anasema wananchi wanaoishi kandokando ya hifadhi hunufaika na wageni wanaoingia katika hifadhi hiyo ambapo hucheza ngoma za asili kwa ajili ya kuwakaribisha wageni na hujipatia kipato cha moja kwa moja kutoka kwa watalii, pia wananchi hupata ajira za kazi zinapotokea hifadhini.
Pamoja na mafanikio hayo, Myonga anasema zipo changamoto ikiwemo miundombinu mibovu, hasa ya barabara katika Mkoa wa Kigoma, hali inayosababisha watalii wachache kutembelea Kigoma.
Changamoto nyingine ni ulinzi hafifu wa wanyama hao adimu na kuhakikisha wanapata mahitaji yao ya kila siku ikiwemo chakula katika mazingira wanayoishi.
Pia ongezeko la idadi ya watu, kujenga maeneo ya hifadhi, huku wakiendesha shughuli kama za kilimo pamoja na usalama wa watumishi, kwani kumekuwepo na wimbi la utekaji wa boti ndani ya Ziwa Tanganyika.
Myonga anatoa rai kwa serikali kuendelea kuhifadhi maeneo ya Ziwa Tanganyika kwa ajili ya shughuli za kiuchumi na kitalii, pia anaishukuru serikali kukubali kuongeza kilometa 21 katika mipaka ya hifadhi.
Mhifadhi huyo anawataka wakazi wa Kigoma kujenga tabia ya kutembelea hifadhi zao na kuwapeleka watoto kipindi cha likizo kutembelea hifadhi.
Anasema kwa sasa gharama za kutembelea Hifadhi ya Gombe ni sh 1,500 kama kiingilio na sh 500 kama fedha ya kutembea.
Malazi pia hupatika kwa sh 5,000 kwa siku, gharama ya chakula ni sh 5,000 kwa mlo mmoja,  soda ni sh 1,500 na  bia ni sh 2500.
“Wananchi wajitokeze kutembelea Hifadhi yao ya Gombe kwani usafiri wa kufika huku na kurudi  upo wa boti na ni wa uhakika, watoto chini ya miaka 15  hawaruhisiwi kuingia hifadhini kutalii, kwa sababu ya usalama wao, wanabaki katika nyumba zetu za kupumzikia wageni,” anasema Myonga.
Daktari wa wanyama wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), Jane Raphael, anasema kwa kawaida sokwe huishi miaka 50.
Anasema majike huishi miaka mingi kuliko madume ambao huishi takriban miaka 35.
Daktari huyo anazitaja baadhi ya tabia ambazo sokwe hufanana na binadamu ni kuwa wakifiwa hukusanyika pamoja na kulia kwa huzuni, ambapo huomboleza hadi mwili wa mwenzao uoze.
“Wakiona mwili wa mwenzao aliyekufa umeshaoza, hasa wanapoona inzi wengi, ndipo hujua kwamba mwenzao amekufa, wanaondoka na kwenda eneo jingine, lakini huwa na huzuni sana,” anasema Dk. Raphael.
Anasema sokwe nao hupangilia uzazi kama binadamu, kwani huzaa kila baada ya miaka mitano au minne; pia wanaheshimiana sana, huwezi kukuta anaoa kaka au dada.
“Wanaheshimiana sana, huwezi kukuta kampanda mama yake, na mama huwa anatembea na mtoto wake hadi anapokua na kwenda kuanza kutembea na kundi lake,” anasema.
Dk. Raphael anasema wanyama hao wana tabia ya kujenga nyumba kama za binadamu, ingawa zao ni sawa na viota juu ya miti, nyumba zao huziezeka kwa nyasi au majani, ila panapopambazuka huamia eneo jingine, hivyo hujenga kila siku nyumba zao.
Ofisa Utalii wa Hifadhi ya Gombe aliyejitambulisha kwa jina moja la Anifa, anasema wananchi hawana uelewa wa kutosha juu ya utalii na uhifadhi.
“Wananchi wengine wanadhani mtalii ni Mzungu pekee, hapana, mtalii ni mtu yeyote anayetembelea mahali fulani tofauti na anapoishi kwa muda usiopungua saa 24 na usiozidi mwaka mmoja kwa lengo la kupumzika, kustarehe na mafunzo,” anasema Anifa.
Anifa anasema vitu vinavyosababisha utalii wa Kigoma kutokukua ni tatizo la mawasiliano ya uhakika kati ya mgeni na wenyeji, usafiri usio na uhakika na huchukua muda mwingi kufika Kigoma kutokea maeneo mbalimbali.
Ofisa huyo anasema Kigoma ni mkoa muhimu katika utalii wa nchi, kwani kuna vivutio muhimu vya kihistoria, kiasili na kitamaduni.
Anavitaja baadhi ya vivutio hivyo kuwa ni Pori la Akiba la Moyowosi, makumbusho ya Dk. Livingstone Ujiji na mji wa Ujiji.
Wananchi wanaoishi Kigoma huu ndio wakati wa kuchangamkia fursa ya kufaidika na Hifadhi ya Gombe, kwani hivi sasa idadi ya watalii wanaokwenda Gombe na kulala imeongezeka, hivyo zinahitajika hoteli nzuri na nyumba za kulala wageni.

No comments:

Post a Comment