Jengo la
Serikali ambalo pia lilitumika kama ngome ya gereza ya Kikoloni enzi hizo.
Picha na Maimuna Kubegeya
Na Maimuna
Kubegeya, Mwananchi
Posted Decemba14 2013
Posted Decemba14 2013
Kwa ufupi
Tofauti
na miji mingine ya kale mji wa Kilwa Kisiwani ulikuwa kiunganishi na kitovu
kikubwa cha biashara kati ya watu wa Bara la Afrika, Bara Asia na kwengineko.
Historia inaonyesha kuwako kwa majengo kadha wa kadhaa yaliyoacha historia
kubwa duniani.
Kilwa.
Mji wa Kilwa Kisiwani Mkoani Lindi ni miongoni mwa miji michache iliyobeba
historia ya Bara la Afrika. Inasadikiwa kuwa mji huu ulianza katika karne ya
saba baada ya Kristo takribani miaka 1,400 iliyopita.
Tofauti
na miji mingine ya kale mji wa Kilwa Kisiwani ulikuwa kiunganishi na kitovu
kikubwa cha biashara kati ya watu wa Bara la Afrika, Bara Asia na kwengineko.
Historia inaonyesha kuwako kwa majengo kadha wa kadhaa yaliyoacha historia
kubwa duniani.
Katika
makala zilizotangulia tuliona baadhi ya urithi wa kihistoria ulioachwa katika
eneo hili la Kilwa Kisiwani. Nikiwa mmoja kati ya watu waliobahatika kufika
kwenye mji huu, nilishuhudia vituo 10 muhimu vinavyopatikana Mafia Kisiwani.
Vituo
hivyo ni majengo muhimu yanayoendelea kuwapo hadi sasa yakithibitisha kuwapo
kwa vizazi vilivyokuwa vikiishi eneo hilo kama ifuatavyo;
Makutani
Palace
Neno
Makutani lilimaanisha eneo lenye kuta kubwa. Eneo hili lililokuwa
limezungushiwa ukuta mrefu. Ndani ya eneo hili kulikuwa na majengo mengi. Pia
lilikuwa ni eneo alilokuwa akiishi Mfalme Hassan bin Ibrahim, aliyekuwa
akijishughulisha na biashara. Ni eneo lililo upande wa Mashariki mwa Kisiwa cha
Kilwa.
Msikiti
mdogo
Hatua
chache kutoka eneo la Makutano kuelekea upande wa Magharibi mwa Kisiwa hiki,
kuna jengo la msikiti uliokuwa miongoni mwa misikiti 99, iliyopatikana ndani ya
Kisiwa hiki kwa wakati huo. Msikiti huu ulijengwa katika karne 15 na sasa una
takriban miaka 600.
Msikiti
mkuu
Unapomaliza
eneo la msikiti mdogo, unaingia kwenye eneo lililo na msikiti mkubwa. Msikiti
huu unatajwa kuwa mkubwa zaidi katika karne ya 11 kuwahi kujengwa Kusini mwa
Jangwa la Sahara. Msikiti mkuu ni misikiti miwili iliyounganishwa pamoja. Ndani
yake kuna ukumbi wa kuswalia na unasadikika kuwa ulijengwa tangu karne ya 11.
Pia kuna uwanja wa kutawadhia, wenye mabirika ya maji na mawe laini ya kufutia
miguu.
Ukumbi
mkubwa zaidi wa kusalia na sehemu kubwa zaidi ya kutawadhia vilijengwa
takribani miaka 1,320. Sultani Al Hassan Bin Sulaiman anatajwa kuhusika na
ujenzi wa msikiti huu. Ndani ya msikiti huu kuna chumba maalumu alichokuwa
akiswalia Sultani.
Ngome ya
Gereza
Hatua
chache kutoka msikiti mkubwa kuna jengo kubwa linalofahamika kama Ngome ya
Gereza. Tofauti na majengo mengine, jengo hili halikujengwa na wakazi wa Kilwa,
bali lilijengwa na Wareno, walioongozwa na Fransisco De Almeida.
Lengo kuu
la ujenzi huu ilikuwa ni kupata eneo litakalotumika kama ngome ya ulinzi
itakayotumika kuona maadui kabla ya kufika ndani ya kisiwa hicho.
Jengo
hili lilijengwa katika karne ya 15, Ikiwa ni ngome ya kwanza kuwahi kujengwa na
Wareno katika Pwani ya Afrika Mashariki, wakati huo Wareno hao walijaribu
kudhibiti maeneo mengi ya Pwani wakilenga kudhibiti pia biashara ya za
maliasili, hasa madini yaliyokuwa yakipatikana katika maeneo hayo.
Ngome
nyingine zilizojengwa na Wareno katika karne hiyo ni pamoja na Ngome Kongwe ya
Zanzibar, Fort Jesus ya Mombasa nchini Kenya na Fort Sao Sbastiao ya Beira
Msumbiji wakati ule ikijulikana kama Sofala.
Msikiti
na makaburi ya Malindi
Majengo
ya msikiti huu yalijengwa katika karne ya 15 na kufanyiwa marekebisho katika
karne ya 18. Yanapatikana hatua chache ubavuni mwa Ngome ya Gereza. Pembeni ya
msikiti huu kuna makaburi ya wanafamilia walioishi katika kisiwa hicho
waliokuwa na asili ya Kenya.
Makaburi
hayo yanafanana na makaburi mengi ya Kisultani yaliyokuwa yakijengwa katika
karne hiyo kwenye maeneo mbalimbali hasa Pwani.
Husuni
Kubwa
Umbali wa
kilometa mbili kutoka makaburi ya Malindi. Linapatikana jengo kubwa zaidi
kuwahi kujengwa Kusini mwa Jangwa la Sahara katika karne ya 14 hadi 15. Likiwa
na vyumba 100, mabwawa ya kuogelea, kumbi za mikutano na kumbi za kufanyia
biashara. Jengo hili lililojulikana kama Husuni kubwa lilijengwa katika karne
ya 18. Sultan Al- Hassan Bin Sulaiman ndiye hasa aliyefanya ubunifu huo.
Husuni
kubwa lilikuwa jengo la ghorofa lililo kando ya Bahari ya Hindi. Ni jengo
lililotengenezwa kwa mawe na chokaa, likiwa na mapambo ya kila aina kama
yalivyobiniwa na wasanifu wa majengo wa wakati huo
Husuni
ndogo
Jengo
hili linapatikana pembezoni mwa Husuni Kubwa. Ni miongoni mwa majengo
yaliyoharibika zaidi, kwani kwa sasa linaonekana sehemu yake ya chini pekee ambayo
ni msingi mkuu wa jengo hilo.
Inaaminika
kuwa jengo hili liliwahi kuwapo kabla ya kujengwa kwa Husuni kubwa. Kwa mujibu
wa wataalamu wa mambo ya historia, Husuni ndogo ilijengwa kati ya karne ya 12
na 13.
Inasadikika
kuwa ndani ya jengo hili kulikuwa na stoo kubwa iliyotumiwa kuhifadhi madini ya
dhahabu, pembe za ndovu na vitu vingine vya thamani kwa ajili ya biashara.
Makaburi
ya Sultan
Hili ni
eneo kubwa la makaburi lililopo ndani ya kisiwa hiki. Makaburi mengi yaliyopo
katika eneo hili ni ya viongozi mbalimbali waliowahi kuishi ndani ya kisiwa
hicho tangu karne ya 16.
Ushahidi
unaonyesha kuwa kuna makaburi mengine yaliyojengwa katika karne ya 17, 18 na
19.
Mengi ya
makaburi haya yameandikwa kwa lugha ya Kiarabu, jambo linalothibitisha kuzikwa
kwa watu wenye asili ya Uarabuni, waliokuwa wakiongoza na kujulikana kama
masultani.
No comments:
Post a Comment