Wednesday, February 18, 2015

Bado tembo wanakwisha Selous




Jumatano
Februari 18,  2015



 
  TEMBO
Na Peter Elias

Posted  Jumanne,Februari17  2015  saa 15:57 PM
Kwa ufupi
Asilimia 90 ya watalii wanaokuja nchini wanakuja kuona wanyama. Asilimia 10 zilizobaki ni utalii mwingine kama vile kuona mali kale, tamaduni mbalimbali na maeneo ya kihistoria.
Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa Novemba, 2014 na Taaasisi ya Uchunguzi wa Mazingira (EIA), zaidi ya tembo 25,000 waliuawa katika hifadhi ya taifa ya Selous pekee katika kipindi cha miaka minne kuanzia 2009 – 2013.
Miongoni mwa vitu ambavyo taifa inalitegemea katika kuongeza mapato ni utalii. Lakini sasa hakuna wanyama.
Asilimia 90 ya watalii wanaokuja nchini wanakuja kuona wanyama. Asilimia 10 zilizobaki ni utalii mwingine kama vile kuona mali kale, tamaduni mbalimbali na maeneo ya kihistoria.
Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa Novemba, 2014 na Taaasisi ya Uchunguzi wa Mazingira (EIA), zaidi ya tembo 25,000 waliuawa katika hifadhi ya taifa ya Selous pekee katika kipindi cha miaka minne kuanzia 2009 – 2013.
Tembom ambaye kwa kawaida umri wake hufikia miaka 60, anaweza kuliingizia taifa kiasi cha Dola za Marekani 1.6 milioni (Sh2.8 bilioni) kutokana na utalii pekee. Hii ina maana kuwa tembo mmoja anaweza kuchangia Dola za Marekani 22,966 (Sh41 milioni) kwa mwaka kwa utalii pekee.
Mshauri wa Masuala ya Elimu na Mawasiliano wa Kampuni ya Selous Safaris, Jane Kremer anasema zaidi ya Sh7 trilioni zimepotea katika kipindi cha miaka minne kutokana na idadi kubwa ya tembo waliouawa. Anasema tembo akiachwa na kuishi umri wake wote (miaka 60) anaweza kuongeza pato la taifa la Sh2.8 bilioni (Dola 1.6 milioni) kwa mwaka. Pato hili likisimamiwa vema, Kremer anasema linaweza kubadili maisha ya Watanzania wengi ambao wanaishi maisha duni.
“Watanzania wakipaza sauti zao na kusema ‘hapana ujangili’ kama walivyofanya katika kashfa ya escrow, tatizo la ujangili litakwisha kabisa. Hawatajihusisha tena katika biashara hiyo haramu,” anasisitiza.
Miaka ya hivi karibuni, tembo wamepungua sana katika hifadhi ya Selous ambayo ndiyo yenye tembo wengi zaidi nchini. Kremer anasema kampuni yake ya usafirishaji wa watalii inapata wakati mgumu kuwatembeza watalii kuwaona tembo, wakati mwingine hawaonekani kabisa. “Zamani tembo walikuwa wanaonekana kila sehemu ya hifadhi hii, lakini sasa lazima utembee maeneo mengi kuwatafuta walipo. Hii inamaanisha kuwa idadi yao imepungua sana tofauti na miaka ya nyuma,” anaongeza.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu anasema kosa kubwa walilolifanya kwa miaka mingi ni kutojua idadi kamili ya tembo wanaopatikana nchini na maeneo ambayo wanauawa kwa wingi. Anasema sensa ya tembo imefanyika na muda wowote itatolewa. Hata hivyo, waziri huyo anasema wizara yake imeanza kufanya maboresho ya maslahi ya askari wanyamapori ili kuwatia moyo katika kutekeleza majukumu yao ya ulinzi wa wanyamapori.
Nyalandu anabainisha kuwa Serikali pia inaangalia maslahi ya wananchi waishio kando kando ya hifadhi za taifa. Anasema wameanzisha mpango wa kushirikisha wananchi katika kusimamia wanyamapori (WMA).
“Changamoto kubwa ambayo tunayo ni kwamba Idara ya Wanyamapori inakusanya mapato, lakini mapato hayo hupelekwa hazina. Kuzipata hizo fedha tena ili zije kwenye bajeti yetu ndiyo inachukua muda sana. Sasa tunataka kufanya marekebisho ili Idara ya Wanyamapori iwe taasisi inayojitegemea, pia inayokusanya mapato na kuyatumia,” anabainisha Nyalandu.
Waziri huyo anasema Dola za Marekani 8 milioni zilitolewa mwaka jana katika hifadhi ya Ruaha ili kuwanufaisha wananchi waishio maeneo ya jirani na hifadhi hiyo. Anasema mpango wizara yake itahakikisha WMA inawanufaisha wananchi wote waishio karibu na mapori ya akiba.
“Ninaamini kuwa mabadiliko ya mfumo wa uongozi katika Idara ya Wanyamapori tunayoyasubiri yataleta ufanisi mkubwa katika uendeshaji wa mapori ya akiba, pia udhibiti wa ujangili utafanikiwa kwa kiasi kikubwa,” anafafanua Waziri Nyalandu.
Malalamiko ya wananchi
Wananchi waishio karibu na hifadhi za taifa wamekuwa wakilalamika kutonufaika na rasilimali zinazowazunguka licha ya kuwa Serikali inaingiza fedha nyingi. Jambo hilo linawafanya waingie ndani ya hifadhi ili kujipatia mahitaji yao.
Uhusiano kati ya askari wanyamapori na wananchi wa vijiji vinavyoishi karibu na hifadhi ya Selous yamekuwa si mazuri kwa muda mrefu sasa. Uhasama huo unatokana na baadhi ya wanakijiji kupigwa risasi na askari hao wakati wakifanya shughuli zao za uvuvi kwenye mto Rufiji.
Wananchi wa kijiji cha Mloka wanasema zaidi ya watu 30 wameuawa na askari hao kwa sababu wanakwenda kuvua samaki katika mto Rufiji ambao unapita katika hifadhi ya Selous.
Mkazi wa kijiji hicho, Hamis Mvuoni anasema shughuli yao kubwa ya kiuchumi ni uvuvi lakini wamekuwa wakipigwa risasi wanapokwenda kuvua katika mto huo. Anaongeza kuwa katika kijiji chao hakuna jangili hata mmoja lakini wanauawa kwa kuhisiwa kuwa ni majangili.
Mwisho.




No comments:

Post a Comment