Sunday, December 22, 2013

Maliasili na Utalii, kaa la moto kwa mawaziri


  Jumatatu,Decemba23  2013  saa 9:14 AM
Kwa ufupi
  • Balozi Khamisi Kagasheki, aling’olewa na Rais Jakaya Kikwete, Ijumaa iliyopita ikiwa mwendelezo wa kutodumu kwa mawaziri kwenye wizara hiyo.
Dar es Salaam. Wizara ya Maliasili na Utalii imeelezwa kuwa ni kaa la moto kwa watu walioteuliwa kuongoza wizara hiyo kwani katika kipindi cha miaka 25, imeshaongozwa na mawaziri 10.
Balozi Khamisi Kagasheki, aling’olewa na Rais Jakaya Kikwete, Ijumaa iliyopita ikiwa mwendelezo wa kutodumu kwa mawaziri kwenye wizara hiyo. 

Tangu mwaka 1988 ni waziri mmoja tu, Zakhia Meghji ambaye alidumu kwa muda mrefu akiiongoza wizara hiyo kwa miaka minane kuanzia 1997 hadi 2005.

Kumbukumbu zinaonyesha pia kuwa awamu ya nne chini ya Rais Jakaya Kikwete imetia fora kwa kubadili mawaziri wa wizara hiyo kwani tangu mwaka 2005, imeongozwa na mawaziri watano tofauti na awamu ya tatu chini ya Rais Benjamin Mkapa ilipoongozwa na mawaziri wawili.

Wafuatiliaji wa mambo ya siasa wanaamini kutodumu huko kunatokana na mapato makubwa yanayotokana na rasilimali kama za utalii na uwindaji ambavyo  vimesababisha kuwapo kwa tuhuma nyingi za rushwa na ufisadi.

Kashfa nyingi katika wizara hiyo zimeitikisa Serikali mara nyingi kama ile ya uuzaji wa pori la Loliondo, kuuzwa kwa hoteli wa kitalii zilizokuwa zinamilikiwa na Serikali kwa bei ya kutupa, uuzwaji wa vitalu vya viwanja na biashara ya pembe za ndovu na vipusa.

Mawaziri waliopita Maliasili watoa neno

Baadhi ya mawaziri waliowahi kushika wadhifa huo wameelezea changamoto walizokabiliana nazo katika kipindi cha uongozi wao. Mmoja wao ni Arcardo Ntagazwa alisema tatizo lililopo kwa viongozi wa sasa ni kufanya uamuzi bila kumuogopa Mungu...

 “Wanasiasa na viongozi wa kada mbalimbali wanatakiwa kumtanguliza Mungu kabla ya kuchukua uamuzi, lakini pia wanatakiwa kutambua kuwa wao ni watumishi wa watu.”

Alisema akiwa waziri wa wizara hiyo aliwahi kuongoza Operesheni Uhai ambayo ililenga kutokomeza vitendo vya ujangili kama ilivyokuwa Operesheni Tokomeza Ujangili, na kusema hii ya sasa imekithiri matukio ya ajabu.

Kwa upande wake, Anthony Diallo ambaye pia aliwahi kuwa waziri wa wizara hiyo alisema: “Wizara ya Maliasili na Utalii imezungukwa na watu ambao wana mambo yao wanayafanya. 

Sasa kama kuna waziri ambaye ni mgumu (siyo rahisi kurubuniwa), lazima atawekewa vikwazo tu.” Alisema wakati akiwa waziri kulikuwa na baadhi ya watu wakiwamo watendaji wa Serikali waliomtengenezea majungu kutokana na kuwabana katika biashara zao za uvunaji wa magogo.

“Kipindi hicho tembo waliuawa wengi, uwindaji haramu pia ulikuwa ukifanyika,” alisema Diallo, ambaye sasa ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza.
Alisema baadhi ya viongozi hivi sasa hawajiamini katika utendaji wao wa kazi kutokana na kupata madaraka hayo kwa fedha zao. 

Alimtolea mfano Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli kuwa mmoja kati ya mawaziri wanaotenda kazi zao kwa kujiamini, mpaka kufikia hatua ya Serikali kuingilia uamuzi wake mara kadhaa na kuzuia utekelezaji wa jambo fulani ambalo aliliamua lifanyike.
“Mawaziri wa aina hii wamebaki wachache. 
Lakini kinachonishangaza ni kufanyika kwa Operesheni Tokomeza huku ikihusisha wizara zaidi ya moja, ilitakiwa isimamiwe na wizara moja ili kuondoa mwingiliano wa kiuamuzi, hakukuwa na utaratibu wa kupeana taarifa,” alisema.
Waziri mwingine ni Ezekiel Maige ambaye baada ya kung’olewa nafasi yake ilichukuliwa na Kagasheki alisema hawezi kuzungumzia suala hilo kwa sababu aliwahi kuwa kiongozi wa Serikali.

Ifuatayo ni orodha ya mawaziri waliowahi kuongoza wizara hiyo na tangu mwaka 1988 na misukosuko iliyowakumba.
Arcado Ntagazwa
Aliongoza wizara hiyo kuanzia mwaka 1988 hadi 1990. Hakurudishwa kwenye wizara hiyo baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 1990. Katika kipindi hicho, wizara hiyo ililaumiwa kwa hatua yake ya kubinafsisha hoteli mbalimbali za kitalii zilizokuwa zinamilikiwa na Serikali kwa bei ya kutupa. Hoteli hizo ni pamoja na Lake Manyara, Ngorongoro, Seronera na Lobo. Hoteli hizo zilijengwa kwa gharama kubwa kwa msaada mkubwa wa serikali ya Israel. Pia uuzaji wa Hoteli za Mount Meru kwa kampuni ya Accor ya Ufaransa  na ile ya Mikumi ilisababisha malalamiko makubwa.
Abubakar Mgumia
Mbunge huyo wa zamani wa Tabora Mjini aliongoza wizara hiyo kuanzia mwaka 1990 hadi 1993. Katika kipindi cha uongozi wake ndipo Shirika la Utalii Tanzania (TTC) lilibadilishwa na kuwa Bodi ya Utalii. Katika kipindi hicho kulitokea malalamiko ya uharibifu mkubwa wa misitu kutokana na kupamba moto kwa biashara ya mbao.
Juma Hamad Omar
Ni kati ya mawaziri, ambao hawatasahaulika kirahisi katika historia ya uongozi wa wizara hiyo. Katika kipindi cha uongozi wake ndipo ilipotokea kashfa ya Loliondo. Kutokana na hatua ya wizara yake kuuza Pori la Loliondo kwa mwana wa Mfalme wa Falme za Kiarabu.
 Kashfa hiyo ni kati ya matukio makubwa yaliyotikisa nchi kwani ilisababisha kuundwa kwa Kamati ya Bunge iliyoongozwa na Mateo Qaresi na chanzo cha kuondolewa kwa Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori wakati huo, Muhidin Ndolanga. Omar aliondoka katika wizara hiyo mwaka 1995 baada ya Rais Mkapa kuingia madarakani.
Juma Ngasongwa
Aliongoza wizara hiyo kuanzia mwaka 1995 hadi 1997. Alilazimika kujiuzulu baada ya kuibuka kwa kashfa ya biashara ya minofu ya samaki kuuzwa nje ya nchi bila kulipa kodi. Kamati iliyoundwa chini ya Mbunge wa zamani wa Ilala, Iddi Simba ilifichua madudu katika biashara hiyo.
Zakhia Meghji
Ndiye waziri aliyedumu kwa muda mrefu zaidi kwenye wizara hiyo kuanzia 1997 hadi 2005. Meghji anasifiwa kutokana na kutangaza utalii wa Tanzania kwa kiasi kikubwa. Hakukumbwa na kashfa yeyote pengine doa pekee lilikuwa ni kuuzwa kwa Hoteli ya Kilimanjaro.
Anthony Diallo
Aliteuliwa Rais Kikwete alipoingia madarakani mwaka 2005.

 Alidumu kwa kipindi cha miaka miwili baada ya kutokea mtikisiko mkubwa juu ya uuzwaji wa vitalu vya uwindaji. Aliingia katika mvutano mkali na watendaji wa wizara hiyo. 
Alishindwa katika vita hiyo na kujikuta akiondolewa. Ingawa aliondolewa katika kipindi ambacho Rais Kikwete alikuwa anataka viongozi kutenganisha masuala ya biashara na uongozi.
Profesa Jumanne Maghembe
Ni waziri ambaye alikaa muda mfupi zaidi kwenye wizara hiyo. Alikaa kuanzia mwaka 2007 hadi 2008. Katika kipindi chake, matatizo mbalimbali yalipamba moto na hasa juu ya uuzwaji wa vitalu na pia uvunaji wa misitu.
Shamsa Mwangunga
Aliongoza wizara hiyo kuanzia mwaka 2008 hadi 2010. Katika kipindi cha uongozi wake alitikiswa na kashfa ya uuzwaji wa vitalu.

 Alituhumiwa kuongeza muda wa umilikaji wa vitalu kinyume cha sheria. 
Aliwaongezea wamiliki hao muda wa miaka mitatu kinyume cha Azimio la Bunge la kuzuia kuongezwa kwa muda wa umiliki wa vitalu ili utaratibu mpya uandaliwe.
Ezekiel Maige
Alipandishwa kuwa Waziri kamili wa wizara hiyo aliyokuwa Naibu chini ya Mwangunga. Aliongoza kuanzia mwaka 2010 hadi 2012. Alikuwa na kibarua cha kupambana na uuzaji wa vitalu. Hata hivyo, alijikuta akiondolewa katika wadhifa huo kufuatia maagizo ya Bunge baada ya kuibuka kwa kashfa ya uuzaji wa wanyama hai.
Khamisi Kagasheki
Aliteuliwa kushika wadhifa huo mwaka 2012. Kagasheki alipata msukosuko wa kwanza wa kisiasa baada ya kutangaza eneo hilo la kilomita 1,500 la Loliondo kuwa ni pori tengefu na wananchi kuachiwa kilomita 2,500.

 Agizo lake lilitenguliwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda. Hata hivyo, amejikuta akiondolewa baada ya mateso yaliyowapata wananchi wakati wa utekelezaji wa Operesheni Tokomeza Ujangili iliyokuwa na lengo la kupambana na biashara haramu ya pembe za ndovu. Hatua hiyo ilifuatia uchunguzi uliofanywa na Kamati ndogo ya Bunge.

No comments:

Post a Comment