SERIKALI mkoani Manyara imewataka
wakulima walio eneo la hifadhi ya msitu wa jamii ya Embreloy Murtangus,
wilayani Kiteto kuondoka kwa hiari yao kabla ya Desemba 27 mwaka huu.
Rai hiyo
ilitolewa juzi na Mkuu wa Mkoa wa Manyara Elaston Mbwilo wakati akizungumza na
waandishi wa habari ofisi kwake juu ya mgogoro wa ardhi kati ya wakulima na
serikali wilayani humo kugombea eneo la hifadhi ya jamii.
Alisema
mgogoro huo ulianza mwaka 2006 ambapo ilionekana hao wavamizi ambao ni wakulima
wana haki na ilifikia mahali walishtaki halmashauri ya wilaya na kijiji
mahakama ya wilaya na Mahakama Kuu ambako walishinda kesi.
Hata
hivyo, wilaya ilikata rufaa Mahakama Kuu ambayo Desemba mwaka jana iliamuru
ardhi hiyo irejeshwe kwenye kijiji na halmashauri ni baada ya kuona vijiji
viliamua kutoa eneo kwa ajili ya hifadhi.
“Wananchi
waliamua kutoa eneo kwa ajili ya kulihifadhi kwa manufaa mbalimbali ikiwemo
kuvuna wanyama ambao wapo ndani ya msitu huo, kuweka mizinga ya asali, mbao, huku
wafugaji wakifaidika na malisho wakati wa msimu wa ukame,” alisema Mbwilo.
Alisema
kabla ya kuzuka kwa mgogoro huo, baadhi ya wakulima kutoka nje ya Mkoa wa
Manyara kama mikoa ya Iringa, Dar es Salaam na Dodoma, waliingia ndani ya msitu
huo kwa kufanya uharibifu wa kufyeka msitu na kuanza kufanya shughuli za kilimo
bila utaraibu huku wengi wao wakijimilikisha sehemu kubwa ya ardhi.
“Mnakumbuka
mwaka jana wakulima hao waliandamana na matrekta yao zaidi ya 400 wakimweleza
Waziri Mkuu kuwa matrekta hayo walikopa kwa ajili ya kulima kwenye eneo hilo
sasa fedha zake watarejeshaje,” alihoji.
Alisema
maamuzi ya kuondolewa kwa wakulima ndani ya hifadhi hiyo sio suala la Mkuu wa
Mkoa wala Mkuu wa Wilaya bali ni la Mahakama ya Rufaa ambayo ilitoa uamuzi huo.
“Sio suala
tena la kusema sisi hatutoki hapa, sisi tutatekeleza maamuzi ya mahakama,”
alifafanua Mbwilo.
No comments:
Post a Comment