Mwenyekiti wa TATO,Wilbard Chambulo akiongea na waandishi wa habari kuhusiana na suala la ujangili unavyoathiri sekta ya utalii.
Journo Tourism-Arusha.
Arusha,Chama cha Mawakala wa utalii nchini(TATO),kimeitaka serikali, kupiga marufuku,uwindaji wa vibali wa Tembo na Simba ili kudhibiti,matukio ya ujangili ambayo yamekithiri nchini.
Chama hicho,pia kimeisihi serikali,iendelee na operesheni ya kutokomeza ujangili,kwani kusitisha operesheni hiyo ni sawa na kuwapa ushindi majangili.
Wakizungumza na waandishi wa habari,viongozi wa TATO,ambao ni wakurugenzi wa makampuni yanayotoa huduma za utalii nchini, walisema serikali sasa inapaswa kusitisha uwindaji ili kufanya tathimini ya Tembo na Simba waliopo.
Mwenyekiti wa TATO,Wilbard Chambulo,alisema kama serikali isipositisha uwindaji wa Tembo na Simba na pia ikisitisha operesheni, wanyama hao watatoweka kabisa na kubaki historia.
"Kama wanyama hawa wakitoweka tujue ndio mwisho wa utalii,kwani maelfu ya watalii wanakuja nchini kuona wanyama hawa"alisema Chambulo.
Alisema umefika wakati serikali kufanya maamuzi magumu ya kusitisha uwindaji na kuhamasisha utalii wa picha kama zilivyo nchi nyingine duniani.
"Utalii wa kupeleka wageni hifadhini na maeneo mengine ya utalii, unaingiliza zaidi ya dola bilioni 1.8 wakati uwindaji unaingiza dola 40 milioni pekee"alisema Chambulo.
Alisema ubaya wa uwindaji ni kuwa unafanyika jirani na hifadhi za Taifa na hivyo ni vigumu kubaini majangili na wawindaji wenye vibali .
Mwisho
No comments:
Post a Comment