MAHAKAMA
ya Hakimu Mkazi ya Wilaya ya Mpanda, mkoani Katavi imewahukumu watu watatu
kutumikia kifungo cha miaka 70 jela baada ya kupatikana na hatia ya
kukamatwa na meno manne ya tembo yenye thamani ya sh milioni 45.
Hukumu
hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi Mfawidhi, Chiganga Ntengwa, baada ya
kuridhika na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo na upande wa mashtaka.
Waliohukumiwa
kifungo hicho ni Gwabi Mayala (39) mkazi wa kijiji cha Majimoto, wilaya
ya Mlele, ambaye amehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela na kulipa fidia ya
sh milioni 45; na Mashaka Mabanga (33), mkazi wa Sumbawanga, mkoani Rukwa
na Adam Kalinzi (30), mkazi wa kijiji cha Majimoto, wamehukumiwa kila mmoja
kifungo cha miaka 20 jela.
Kabla ya
hukumu hiyo, washtakiwa Mashaka na Adam walikiri kukamatwa na meno hayo ya
tembo, lakini walidai meno hayo ni ya Mayala ambaye alikuwa amewaomba
wamtafutie wateja.
Kwa
upande wake, mshtakiwa Mayala aliiomba mahakama isikubaliane na maelezo ya
washtakiwa wenzake kwa kuwa hayana ukweli.
Awali
katika kesi hiyo, Mwanasheria wa Serikali, Fadhili Mwandoloma, alidai
washtakiwa hao walitenda kosa hilo Oktoba 10 mwaka huu, saa 4:00 usiku
katika kijiji cha Majimoto, wilayani Mlele.
Alidai
siku ya tukio washtakiwa walikamatwa wakiwa na meno manne ya tembo yenye uzito
wa kilo 16 wakiwa katika harakati ya kuyauza.
No comments:
Post a Comment