Saturday, November 16, 2013

Kamati ya Maliasili kuanza kazi Jumatatu


 Asha Bani | Dar |

MWENYEKITI wa Kamati ya Maliasili na Mazingira, James Lembeli, amesema kamati hiyo itaanza kazi ya kuchunguza tuhuma mbalimbali zilizotolewa na wabunge kuhusu mwenendo mzima wa Operesheni Tokomeza Majangili iliyositishwa hivi karibuni Novemba 18 mwaka huu.
Akizungumza na Tanzania Daima jana alisema kamati yake itaanza kazi ya kuchunguza mikoa mbalimbali iliyolalamikiwa kuwa operesheni hiyo imesababisha mauaji ya mifugo na binadamu.
Alisema maeneo watakayoenda ni Kigoma, Rufiji, Maswa, Meatu, Simiyu, Bukombe, Kahama na Biharamulo huku akiahidi yeye na kamati yake kufanya kazi hiyo kwa ufanisi, maadili na kutoa ripoti iliyo sahihi.
Hata hivyo, Lembeli ambaye pia ni Mbunge wa Kahama alimpongeza Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, kwa kuendelea kuwanasa majangili wanaoendelea kuua tembo.
Alisema watu wengi na hasa wanasiasa wanafanya jambo hilo kuwa la kisiasa na wakidhani kuwa ni jambo la kitoto bila kujua ukubwa wa tatizo lenyewe na kuwataka badala ya kuweka siasa wawape moyo wale wote walio katika mapambano hayo.

No comments:

Post a Comment