UMOJA wa Waongoza Watalii Tanzania (TATO),
wameiomba serikali kushirikiana nao kikamilifu kukuza sekta ya utalii
hapa nchini ili kuongeza mapato ya taifa.
Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa TATO,
Wilbard Chambulo, alipokuwa akijibu hoja za wabunge mbalimbali
waliohudhuria semina iliyoandaliwa na umoja huo kwa lengo la
kuwaelimisha umuhimu wa sekta ya utalii.
Chambulo alisema Kenya inapiga hatua kubwa
katika kutangaza utalii, kuongeza watalii, kurekebisha sheria na
kukarabati miundombinu kutokana na serikali ya nchi hiyo kushirikiana
na sekta binafsi zinazojishughulisha na masuala ya utalii.
Alisema kama Serikali ya Tanzania
haitabadili dhana yake dhidi ya sekta binafsi inayojishughulisha kwenye
utalii na kushirikiana nayo kikamilifu pato la taifa pamoja na ajira za
wanaofanya shughuli hizo zitazidi kudidimia siku hadi siku.
Chimbulo alibainisha kuwa Tanzania imekuwa
ikiwakaribisha wawekezaji na kusajili kampuni za utalii bila
kuzifuatilia kwa ukaribu zaidi, jambo linalochangia kuongezeka kwa
kampuni za mifukoni pamoja na ujangili wa tembo na uhalifu wa
rasilimali za taifa.
Naye Waziri wa Maliasili na Utalii, Khamis
Kagasheki, alikiri kuwa serikali imekuwa na mtazamo usio sahihi kwa
kampuni binafsi za utalii hali iliyochangia kusuasua kwa maendeleo
kwenye utalii.
“Tuna sheria nyingi zinazochangia kukwaza
sekta ya utalii, mfano hapa kwetu vibali vya kufanya utalii vinaweza
kuchukua hadi miezi sita wakati wenzetu wa Kenya vinapatikana ndani ya
siku zisizozidi mbili, hapa ni lazima tubadilike ili tujinusuru kwenye
anguko hili,” alisema.
Naye Mbunge wa Viti Maalumu, Ritta Mlaki
(CCM), alisema serikali imewatelekeza waongoza watalii hapa nchini,
hali inayowafanya wajiongoze kama watoto yatima hatua inayochangia
ufanisi na tija kutopatikana kwa kiwango kinachokidhi mahitaji ya
taifa.
“Ndugu zangu wa TATO nyinyi ni watoto
lakini kuanzia sasa tumeamua kushirikiana nanyi, tuleteeni mikakati ya
kukuza sekta ya utalii na sisi tutaishauri na kuisimamia serikali ili
tuongeze ajira na fedha zitakakuza uchumi wetu,” alisema.
Naye Katibu Mtendaji wa TATO, Mustapha
Akunaay, alisema wameandaa semina hiyo kwa wabunge wa Kamati ya Bunge
ya Ardhi, Maliasili na Mazingira pamoja na Kamati ya Bajeti ili
waifahamu zaidi sekta ya utalii na waandae mazingira bora ya kuiboresha
kwa lengo la kukuza ajira na uchumi wa taifa.
|
No comments:
Post a Comment