Jumamosi,
Octoba 12, 2013 Na Christina Gauluhanga, Dar es Salaam
WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, amesema Bodi ya
Utalii Tanzania (TTB), imechangia kwa kiasi kikubwa uwepo wa mikataba mibovu
ambayo imelinyima taifa mapato katika sekta ya utalii.
Akizungumza Dar es Salaam jana, wakati wa mkutano wa pamoja na Chama cha Wakala wa Utalii Tanzania (TATO), Waziri Kagasheki alisema mikataba mingi iliyopo katika hoteli za kitalii zilizopo kwenye mbuga za wanyama, imepitwa na wakati na haisaidii serikali kuongeza kipato.
“Hoteli nyingi za kitalii, mfano zilizopo katika Mbuga ya Serengeti na nyinginezo, zimepewa mikataba ya kufanya biashara kwa miaka 30 na ukiangalia vizuri Serikali inapoteza mapato…. Tumejikuta inatuwia vigumu kuivunja,” alisema Kagasheki.
Alisema kutokana na hali hiyo, ushirikiano wa dhati unahitajika baina ya wizara zote na mawaziri wake, ili kuondoa changamoto hizo na kuinua pato la taifa ambapo wizara yake inafanya mchakato wa marekebisho ili sera hiyo iendane na wakati.
“Katika hili tunahitaji ushirikiano wa dhati. Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi pamoja na wizara nyingine, ni vyema zikajenga uhusiano ili kuhakikisha pato la taifa linaongezeka, vinginevyo hali itazidi kuwa mbaya,” alisema Kagasheki.
Alisema umefika muda wa viongozi kuwa watendaji na kuacha siasa za kwenye magazeti, kwani bila sekta binafsi uchumi wa nchi hauwezi kukua.
Naye, Mbunge wa kuteuliwa kutoka Chama cha NCCR – Mageuzi, James Mbatia, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kikao cha Bajeti, alisema sera ya utalii imepitwa na wakati na inahitaji mabadiliko.
“Sheria inayoongoza utalii nayo imepitwa na wakati, inahitaji mabadiliko kwa sababu iliyopo haisaidii kukuza uchumi wa nchi,” alisema Mbatia.
Alisema muda umefika sasa kwa Watanzania kwa pamoja kuacha kulalamika na badala yake, wafanye kazi kwa kujituma na kuondoa kasoro zilizopo.
Alisema ili kupata undani wa shughuli za utalii ambao utawapa fursa ya kuweza kuisimamia vizuri serikali, wamepanga kukutana na vyama vinne vinavyojihusisha na utalii, baada ya kumaliza vikao vya Bunge lijalo ambapo watakutana na vyama vya TATO, uwindaji, hoteli na ndege.
Kwa upande wake, Mwenyekiti mstaafu wa Chama cha Wakala wa Utalii Tanzania (TATO), Leopold Kabendera, ameomba biashara ya huduma za utalii itambuliwe kama biashara ya nje.
Alisema kuendelea kwa sekta ya utalii hapa nchini ni lazima biashara ya huduma za kitalii kutambuliwa na kupewa uzito wake.
Aliiomba serikali kuondoa baadhi ya tozo na ushuru ambao unakwamisha mashirika mengi ya kimataifa na yameacha kutua ndege zao hapa nchini.
Alisema ni vyema serikali ikaangalia upya tozo ya ushuru shindani kulinganisha na washindani wa kikanda wa biashara, kurahisisha mifumo ya udhibiti ya mashirika ya ndege ya kimataifa na taasisi za Serikali zinazosimamia shughuli za utalii ziheshimu, kutambua na kushirikisha wadau wa sekta binafsi kwenye maamuzi yenye athari kwa pande zote.
Wakati huohuo, Mbunge wa Viti Maalum, Susan Kimwanga (CHADEMA), alisema Tanzania imejaaliwa rasilimali ambazo kama sekta ya utalii ingejengewa mazingira na kusimamiwa vizuri, serikali ingepata uwezo hata wa kuwajengea nyumba wananchi wake.
Alisema Tanzania ni sawa na bustani ya Edeni, ambayo kama sekta ya utalii ingejengewa mazingira mazuri, basi shida ndogondogo kwa wananchi zisingekuwepo.
No comments:
Post a Comment