Saturday, October 26, 2013

TAHARIRI-TANZANIA DAIMA

Ujangili ni zao la kulindana


KWA muda mrefu sasa nchi mbalimbali zimekuwa kwenye mapambano ya ujangili, hasa ule wa meno ya tembo.
Inakadiriwa kila dakika 15 tembo mmoja huuawa duniani.
Biashara ya meno ya tembo hivi sasa imeshamiri zaidi.
Kwa mujibu wa Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki jino moja huuzwa kati ya dola za Marekani 1,500 na 2,000.
Pamoja na jitihada za kupambana na ujangili huu, bado matukio ya vifo vya tembo yanaongezeka kila kukicha kutokana na ukosefu wa vifaa pamoja na uadilifu mdogo wa watendaji waliopewa jukumu la kusimamia.
Tunaamini kama utaratibu wa kulindana, kuoneana aibu na kupuuzia mambo usingekuwepo, Tanzania ingepiga hatua kubwa katika mapambano dhidi ya ujangili.
Limekuwa jambo la kawaida kila kukicha kusikia watendaji wa serikali, vyombo vya dola, idara au taasisi mbalimbali kukamatwa wakiwa na meno ya tembo na nyara mbalimbali ambazo ni kosa la kisheria.
Pamoja na watu hao kukamatwa na nyara hizo, bado inaonekana hakuna uwajibishanaji ndiyo maana watumishi wengine wamekuwa wakiendelea na uahalifu huo, na hata kushirikiana na watu kutoka nje.
Tunaamini kuwa mpango wa serikali wa kutumia ndege zisizo na marubani kupambana na ujangili hauwezi kufanikiwa kama tabia ya kulindana, kuoneana aibu haitakomeshwa.
Tunaamini ‘Operesheni Tokomeza Majangili’ itakuwa na manufaa zaidi ikiwa Wizara ya Maliasili na Utalii itasafisha kwanza nyumbani kwake, ikiwemo kuwachukulia hatua kali watumishi wanaohusishwa na uhalifu.
Tunachukua fursa hii kumpongeza Waziri Kagasheki kwa kutangaza hadharani kuwa Kikosi Cha Kupambana na Ujangili (KDU), wanasiasa, watumishi wa umma na wafanyabishara mbalimbali wanahusika na biashara hii.
Tunajua kuwatangaza watu kuhusika na biashara hii ni hatua moja muhimu, hivyo ni vema hatua nyingine ya kuwakamata na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria ikachukuliwa.
Bila kuwajibishana, kudhibitiana, biashara ya meno ya tembo, faru na mazao ya misitu itaendelea kushamiri huku taifa likiangamia kwa kukosa mapato yatokanayo na wanyama hao.
Tunaamini kuwa serikali itaitumia kikamilifu Operesheni Tokomeza Ujangili kukabiliana na watu wote wanaohusishwa na vitendo hivyo vya kihalifu bila kujali nyadhifa zao.

No comments:

Post a Comment