• Raia wa kigeni
aliowaita majangili, walibambikwa kesi
na Grace Macha, Arusha-Chanzo Tanzania Daima
|
JESHI
la Polisi mkoani Arusha, limeingia kwenye kashfa nzito baada ya kubainika
kumdanganya Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki kwa
kuwahusisha raia wawili wa kigeni na biashara ya ujangili wakati si kweli.
Hatua
hiyo inakuja baada ya Waziri Kagasheki kudai kuwa watumishi wa serikali
wanakwamisha juhudi za kukabiliana na majangili wa tembo, akitolea mfano wa
Mkuu wa Upelelezi wa Polisi mkoani hapa (RCO), Duwan Nyanda, kwamba
aliwatorosha raia wawili wa Saudia ambao walikamatwa wakiwa na meno ya tembo
pamoja na silaha nzito.
Kwa
mujibu wa vyanzo mbalimbali na nyaraka kadhaa, Tanzania Daima limebaini kuwa
raia hao waliingia nchini Septemba 12, mwaka huu, kupitia Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) na kisha kufikia kwenye hoteli ya kitalii
ya Mount Meru.
Nyaraka
hizo zinaonyesha kuwa wageni hao waliondoka nchini Oktoba 4, mwaka huu,
kupitia uwanja huo huo.
Kwa
mujibu wa waraka wa upekuzi wa polisi (search order) uliosainiwa na Inspekta
James, maofisa wa jeshi hilo walifika kwenye hoteli hiyo Oktoba 3, mwaka huu,
na kupekua vyumba vya wageni hao, lakini hawakukuta kitu chochote
kinachohusiana na nyara za taifa za maliasili kama ilivyodaiwa na Waziri
Kagasheki.
Nyaraka
hiyo inaonyesha kuwa walioshuhudia upekuzi huo mbali na waliokuwa watuhumiwa,
Ali na Nader, ni pamoja na Gidion David na Joseph Enock ambao
waliisaini.
Tanzania
Daima lilifika hotelini hapo na kuzungumza na meneja mapokezi, Enock Maselle
ambaye pia alithibitisha kuwa Oktoba 3, mwaka huu, walifika polisi kwa ajili
ya kukagua vyumba vya wateja wao, Ali na Nader.
Alisema
kuwa waliwaruhusu, lakini akadai ni vigumu kujua nini kiliendelea.
Raia
hao wanadaiwa kujihusisha na kutafuta watu nchini mwao ambao huwaleta Tanzania
kutalii, na kwamba waliingia nchini na kundi la wageni tisa ambao walifanya
safari kwa nyakati mbili tofauti, wakitembelea hifadhi za taifa za Manyara na
Tarangire na
Ngorongoro iliyopo chini ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro
(NCAA).
Mmiliki
wa kampuni ya uwakala wa utalii ya Kalabash, Ally Kalabash aliliambia gazeti
hili kwa simu kuwa Ali na Nader walimletea wageni tisa ambao alifanya nao
safari ya siku tatu katika mbuga za Manyara, Ngorongoro na Tarangire.
“Hawa
ni mawakala wapya, na hii ni mara yangu ya kwanza kufanya nao kazi, ila
wageni walioniletea niliwahudumia mpaka siku wanaondoka, kwani wengine
walilala Mount Meru Hotel na wengine Themi Suite,” alisema.
Naye
Salim Islam Salim ambaye ndiye alikuwa karibu na raia hao wa Saudia, alisema
kuwa walipokuwa hapa nchini walikutana na Richard Kalembe ambaye
aliwaambia anamiliki kampuni ya uwindaji wa kitalii ya RS Kalembe Hunting
Routes.
Alisema
kuwa Septemba 14, mwaka huu, Ali na Nader walimlipa Kalembe malipo ya awali
kwa ajili ya kwenda kuwinda kitalii, kiasi cha dola za Marekani 3,000.
Salim
alifafanua kuwa Kalembe aliwapatia wageni hao risiti yenye namba 012
ikionyesha kuwa bado wanadaiwa dola 7,000 endapo watatumia siku tano na ikiwa
watatumia siku tisa wakiwinda, basi wangelazimika kuongeza dola 9,000.
Kwa
mujibu wa Salim, baada ya Kalembe kupokea malipo hayo, hakufanya mawasiliano
tena na wageni hao, hatua iliyowalazimu kutoa taarifa polisi Oktoba 2, mwaka
huu.
Alisema
kuwa siku iliyofuata, raia hao walipigiwa simu na polisi wa upelelezi
aliyemtaja kwa jina moja la James, akiwaambia kuwa mtuhumiwa wao
ameshapatikana, hivyo wafike polisi ili wakakabidhiwe fedha zao.
“Katika
hali ya kushangaza, walipofika polisi waligeuziwa kibao na kuwekwa chini ya
ulinzi, wakitakiwa kwenda kupekuliwa kwenye vyumba vyao katika hoteli
waliyofikia ya Mount Meru, ambako hata hivyo hawakukutwa na kitu.
“Baadaye
walirudishwa polisi na kuelezwa sababu za kupekuliwa, kwamba walitiliwa
shaka kuwa wanajihusisha na ugaidi,” alisema Salim.
Alifafanua
kuwa polisi waliwaambia kuwa kutokana na tukio la kigaidi lililotokea
hivi karibuni nchini Kenya, wamekuwa makini kwa kila
mtu wanayemuhisi au kumtilia shaka, na hivyo humfanyia upekuzi.
Kwa
mujibu wa Salim, baada ya maelezo hayo walielezwa kuwa wanaweza kuwadhamini.
Yeye na mtu mwingine aliyemfahamu kwa jina moja la Ibra, walimdhamini
Ali huku Nader akidhaminiwa na msichana mwingine ambaye hakumfahamu vizuri.
“Oktoba
4, tulifika pale polisi asubuhi, baada ya panda shuka, watuhumiwa hao
waliwaeleza polisi kuwa wanapaswa kuondoka siku hiyo, hivyo wakaomba wapewe
ruhusa wakabadili tiketi zao au wapelekwe mahakamani ili wajue wanashikiliwa
kwa makosa gani.
“Tukiwa
pale, akaja polisi mmoja mwanamke akasema ‘kama hawa mmewapekua mkaona hawana
kitu, waachieni waende zao’. Ilikuwa kama saa tano asubuhi,” alisema.
Salim
alisema kuwa wageni hao walipewa simu na hati zao za kusafiria na hivyo
wakaondoka kituoni hapo, na baadaye jioni walipanda ndege ya Shirika la Ndege
la Ethiopia na kurudi kwao.
Alisema
kuwa alishangazwa na taarifa zilizoandikwa na vyombo mbalimbali vya habari
zikiwahusisha Ali na Nader na uwindaji haramu huku wakidaiwa kukutwa na pembe
za ndovu, jambo alilodai ni uongo na upotoshaji mkubwa.
Salim
alisema madai ya kwamba dola 3,000 zilitolewa polisi kama rushwa si ya kweli,
kwani kiasi hicho ni fedha anazodaiwa Kalembe alizochukua kwa raia hao,
huku akidai taarifa iko polisi.
Alipotafutwa
Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Liberatus Sabas kuzungumzia sakata hilo,
alisema hayuko tayari kwa sababu linashughulikiwa na mkuu wa jeshi hilo, IGP
Said Mwema ambaye ameunda tume ya uchunguzi.
Naye
Waziri Kagasheki alipotafutwa, simu yake iliita bila kupokelewa.
Salim
ageuziwa kibao
Katika
hatua nyingine, Salim na Gerald Kashiro wamelalamikia kitendo cha kukamatwa
na askari wa kuzuia ujangili kwa nyakati tofauti na kupewa mateso makali,
huku mfanyabiashara Shafiq Feroz akidai kuwa alishikiliwa bila kuteswa.
Walisema
chanzo cha mateso hayo ni nyama ya nyati kilo tano ambayo Feroz alimpatia
Kashiro baada ya kuwa amemsindikiza kuwinda kwenye pori la Terati wilayani
Simanjiro.
Kashiro
alisema kuwa yeye alipopewa nyama hiyo alimwachia mke wake, Judith
Gerald nyumbani akiendelea kuiandaa, huku yeye akiendelea na shughuli
zake.
Alisema
kuwa baadaye alipigiwa simu akiambiwa kuwa mkewe na mama mkwe, wamekamatwa na
askari wa Kikosi cha Kuzuia Ujangili (KDU) wakiwa na wanajeshi.
Akisimulia
mkasa mzima, Salim alisema kuwa Kashiro alimpigia simu akimuomba ampeleke
alipo Feroz ili aweze kupeleka vibali vyake vya uwindaji kwa kambi ya KDU
iliyopo Njiro waweze kuwaachia mkewe na mama mkwe.
Alisema
kuwa baada ya kumfikisha kwa Feroz, aliwaacha wakaelekea Njiro, na yeye
akarudi kuendelea na shughuli zake, lakini wakampigia simu tena wakimuomba
akawadhamini kwani wameshikiliwa.
Kwa
mujibu wa Salim, juhudi za kuwadhamini Kashiro na Feroz
hazikufanikiwa, hivyo aliamua kuondoka. Lakini kabla hajafika kwenye
lango kuu la kutokea, akaitwa na kuulizwa na askari nyumbani kwake ni wapi
ili wakampekue.
Aliongeza
kuwa alipopekuliwa nyumbani kwake Kimandolu, alikutwa na bunduki tatu aina ya
riffle na bastola aina ya short-gun ambazo zote anazimiki kihalali na kwamba
walijiridhisha baada ya kuwaonyesha nyaraka zote muhimu kisha wakarudi naye
hadi KDU Njiro.
“Mimi
na Feroz tuliambiwa tujidhamini wenyewe kwani tunaacha silaha zetu pale.
Feroz naye alikuwa amepekuliwa kwenye hoteli ya Themi Suites alipokuwa
amefikia kutoka Dar es Salaam anakokaa.
“Tulitakiwa
kurudi siku inayofuata, yaani Oktoba 8, mwaka huu, lakini tulipofika siku
hiyo, tukachukuliwa na kufungwa pingu, tukapakiwa kwenye
gari tukapelekwa Terati. Huko kuna eneo limefungwa hema, tulipofika
sikuamini kama Tanzania kuna watu wanateswa hivyo,” alidai.
Kwa
mujibu wa Salim, aliwekewa vijiti katikati ya vidole vyake na kuanza
kuminywa, lakini akawahakikishia kwamba hajihusishi na ujangili.
“Wakachukua
dumu la maji baridi la lita 10 na muda huo ni usiku, baridi ni kali,
wakanimwagia mwili mzima nikiwa na nguo, kisha wakaniambia nitambae kwenye
mchanga mpaka saa tisa usiku ndipo nilipewa fursa ya kulala,” alisema Salim.
Alisema
kuwa walikuwa watu wengi wanaopatiwa mateso ya aina mbalimbali, ikiwemo
kuchapwa viboko pamoja na kufanyishwa kwa nguvu mazoezi ya kupiga ‘push-up’.
Waliondolewa baada ya siku tatu wakapelekwa Serengeti kwenye eneo
lililotengwa kwa ajili ya kikosi hicho.
Salim
alisema kuwa walipofika huko waliendelea kuteswa, na aliomba kuonana na
daktari baada ya hali yake kuzidi kuwa mbaya kwani anakabiliwa na matatizo ya
kisukari pamoja na figo iliyokuwa ikimuuma sana kutokana na mateke
aliyopigwa.
“Daktari
alishauri nipatiwe dawa na nipumzishwe, jambo lililonipa hauweni ya
kutoendelea kupata mateso, maana nilihamishiwa Kituo cha Polisi Bunda
nilikokaa kwa siku nne kabla ya kufikishwa mahakamani.
“Hata
hivyo, baada ya kufikishwa mahakamani sikusomewa shitaka lolote, bali hakimu
aliniambia kuwa mahakama inaniachia huru kwani sina kosa. Nilihoji ni kwanini
nikateswa bure siku 14,” alisema.
Kashiro
ambaye naye alilalamikia kuteswa, alisema kuwa amefunguliwa shitaka la
uhujumu uchumi pamoja na Feroz. Watatakiwa kufika mahakamani Bunda Novemba 7,
mwaka huu wakati shauri lao litakapofika kwa ajili ya kutajwa.
Operesheni
Tokomeza Ujangili ilianza rasmi Oktoba 5, mwaka huu katika hifadhi za taifa,
mapori ya akiba na mbuga za wanyama ikishirikisha Jeshi la Wananchi wa
Tanzania (JWTZ), Polisi, Usalama wa Taifa, Mamlaka ya Hifadhi za Taifa
(TANAPA), Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) na Idara ya Wanyamapori.
|
Saturday, October 26, 2013
Waziri Kagasheki matatani
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment