chanzo-TanzaniaDaima |
MBUNGE
wa Serengeti, Dk. Kebwe Stephen Kebwe, amesema msako wa majangili unaofanywa
na vikosi mbali mbali vya ulinzi katika hifadhi ya Serengeti, unaendeshwa
kiholela hata kufikia kukamatwa watu wasiohusika na kadhia hiyo.
Alisema
askari walio katika operesheni hiyo wanaacha kufanya kazi kitaalamu na badala
yake wanaishia kufanya kazi kwa hisia na kuelezea hali hiyo imesababisha
wilaya ya Serengeti kubaki bila ya askari wa wanyama pori.
Dk.
Kebwe alitoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam, jana wakati akizungumza na
waandishi wa habari kutokana na kukamatwa kwa wafanyakazi wawili wa Idara ya
Wanyamapori katika Halmashauri ya Serengeti wakidaiwa kukutwa na nyara
za serikali katika ofisi za serikali.
Aliwataja
wafanyakazi waliokamatwa kuwa ni Wilbard Boma na Omari Hussein ambao ni
waajiriwa wa halmashauri ya Wilaya ya Serengeti katika idara ya wanyamapori.
Alisema
wafanyakazi hao kabla ya kukamtwa walikuwa wameshakamata nyara mbali mbali za
serikali na kuzihifadhi katika ofisi zao kutokana na wilaya ya Serengeti
kutokuwa na sehemu ya kuhifadhia nyara zinazokamatwa au kutelekezwa na
majangili.
“Wamewakamata
hawa waliokuwa wakitusaidia kwa kazi za kuwadhibiti wanyama pori wale
wasumbufu, wamefanya hivi kwa hisia tu, hivi kweli mtu mwenye dhamira ya
uhalifu anaweza kuweka nyara za serikali katika ofisi anazotumia tena wazi
wazi?” alihoji Dk. Kebwe.
Alisema
ni wakati wa serikali kuhakikisha wilaya ya Serengeti inakuwa na wafanyakazi
wengine wa wanyama pori wakati wakishughulikia tuhuma dhidi ya maofisa
waliokamatwa ili kuepusha mali na maisha ya wakazi wa wilaya hiyo dhidi ya
wanyama wakali.
Aliongeza
kuwa baada ya kukamatwa kwa wafanyakazi hao na kupelekwa katika vituo vya
polisi Bunda badala ya Serengeti athari zake zimeshaanza kuonekana baada ya
tembo kuuwa ng’ombe wawili huku waliosalia wakiogopa kuwadhibiti kwa hofu ya
kuambiwa wanawawinda wanyama hao kwa ajili ya biashara.
Kaimu
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Jumanne Kwila, akiongea kwa
njia ya simu na Tanzania Daima alisema wafanyakazi hao walikutwa
na meno ya tembo 10, vipande vya meno hivyo 13 na meno matatu ya kiboko
yakiwa ndani ya ofisi za serikali zinazotumiwa na waajiriwa hao wa
halmashauri.
|
No comments:
Post a Comment