|
Imeandikwa na
waandishi wetu, Dar es Salaam & Nairobi
|
Jumatano, Oktoba
23, 2013
|
·
JWTZ watisha, maofisa Maliasili 16
wakamatwa
·
Mmoja akutwa anamiliki bunduki 5 za
rifle kali
·
Mbunge Mtutura ahojiwa, Nchambi naye
atajwa
·
RCO aliahidiwa dola 3,000 akawaachia
Waarabu
Operesheni Tokomeza inayoendeshwa chini ya usimamizi wa Jeshi la
Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), imewakamata watumishi kadhaa wa
Serikali wanaotuhumiwa kujihusisha na ujangili. Operesheni hiyo inaongozwa na
Luteni Kanali A. Sibuti.
Pamoja na watumishi hao, wamo pia baadhi ya wabunge waliohojiwa na
wengine wakitarajiwa kuhojiwa. Miongoni mwa waliohojiwa ni Mbunge wa Tunduru,
Mtutura Mtutura (CCM).
Mtutura amezungumza na JAMHURI
na kukiri kuhojiwa na makamanda wa Operesheni Tokomeza. Hata hivyo,
amesisitiza kuwa hajihusishi na ujangili.
Uchunguzi uliofanywa umebaini kuwa wabunge wengine, akiwamo Mbunge wa
Kishapu, Suleiman Nchambi (CCM), watahojiwa wakati wowote kuanzia leo. Kwa
upande wake, Nchambi ameliambia JAMHURI kwamba hana taarifa za kuwamo kwenye
orodha ya watuhumiwa wa ujangili wanaotakiwa kuhojiwa.
Majina ya watuhumiwa yaanza kuanikwa
Hakuna shaka kuwa watuhumiwa wakuu wa mtandao wa ujangili nchini ni
watumishi wa Wizara ya Maliasili na Utalii wenyewe kuanzia Makao Makuu, Dar
es Salaam hadi ngazi za chini kabisa wilayani na ndani ya hifadhi za taifa.
Mmoja wao amekamatwa akiwa na bunduki tano aina ya rifle.
Operesheni hiyo imebaini kuwa pamoja na watuhumishi hao, mtandao wa
uhalifu umeimarika hadi ndani ya Jeshi la Polisi pamoja na Mahakama.
Uvunjaji wa mtandao huo umeanzia kwa watumishi wengi wa Wizara ya
Maliasili na Utalii. Afisa Wanyamapori Wilaya ya Meatu, Mohamed Ismail,
anayetuhumiwa kujihusisha na ujangili, sasa amefikishwa mahakamani kujibu
mashitaka.
Mohamed Hassan Kidunda ambaye ni Afisa Wanyamapori Wilaya ya Meatu,
naye amefikishwa mahakamani akikabiliwa na tuhuma kama hizo.
Katika Wilaya ya Serengeti, Omary Lutiginga, ambaye ni Afisa
Wanyamapori, wilayani Mugumu, naye anahojiwa kwa kujihusisha na ujangili.
Mhasibu wa Kikosi Dhidi ya Ujangili (KDU) Wilaya ya Bunda mkoani Mara,
Jail Adamson Mwakabenga, amefikishwa mahakamani kwa kukutwa akiwa na pembe
mbili za ndovu.
Afisa Wanyamapori Wilaya ya Bariadi, Jesca Mathias, naye amefikishwa
mahakamani baada ya kukamatwa akiwa na silaha na risasi, ngozi za chui
(mbili) ngozi ya chatu, na meno ya kiboko. Silaha alizokamatwa nazo ni
bunduki tano za rifle aina ya 458, risasi za shotgun 107, risasi za rifle 306
(47) na risasi moja ya Sub Mchine Gun (SMG).
Derrick Kasano Mboneka ambaye ni Mhifadhi Daraja la Pili katika
Hifadhi ya Maswa, anahojiwa kwa kujihusisha na vitendo vya ujangili.
Msiba Chiraka ambaye pia ni Mhifadhi Daraja la Pili katika Hifadhi ya
Maswa, naye amekamatwa akiwa na bunduki ya kivita aina ya SAR na risasi 13.
Afisa Wanyamapori Wilaya ya Meatu, Michael Andrew, naye anahojiwa
akituhumiwa kujihusisha na ujangili.
Mhifadhi Daraja la Pili katika Hifadhi ya Maswa, Yasinta Modest,
amekamatwa akiwa na silaha ya kazini aina ya SAR na risasi 21 nyumbani kwake.
Philimony Ntandu ambaye ni Mhifadhi Daraja la Pili katika Hifadhi ya
Maswa anahojiwa kwa kosa la kujihusisha na vitendo vya ujangili.
Uchunguzi wa JAMHURI umebaini kuwa kwenye orodha hiyo wapo pia William
Lugobi Peter ambaye ni Afisa Wanyamapori, KDU Arusha.
Operesheni Tokomeza imemnasa pia Deonatus Makene ambaye ni Afisa
Wanyamapori Arusha. Anahojiwa kwa tuhuma za kuwasaidia wahalifu wa tuhuma za
ujangili.
Afisa Wanyamapori KDU Arusha, Michael Melakiti anahojiwa kwa tuhuma
kama zinazomkabili Makene.
Afisa Wanyamapori Wilaya ya Serengeti, Cuthbeth Boma, yeye amefikishwa
mahakamani kwa kosa la kupatikana na pembe 10 za ndovu, tembo; meno manane ya
kiboko na mikia sita ya ndovu.
Katika eneo la Ngorongoro nako Operesheni Tokomeza imeingia. Aliyenaswa
ni Fredrick Flegence ambaye ni Askari Wanyamapori katika Hifadhi ya Taifa ya
Manyara. Anahojiwa kwa tuhuma za kuua wanyama ndani ya Mamlaka ya Hifadhi ya
Ngorongoro (NCAA).
Askari Wanyamapori katika Hifadhi ya Taifa Manyara, Novatus Mosha,
anahojiwa kwa tuhuma za kuua wanyama ndani ya Mamlaka ya Hifadhi ya
Ngorongoro.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kata ya Makuyuni, Monduli
mkoani Arusha, Bakari Salim (32), naye ni miongoni mwa waliotiwa mbaroni
akiwa na kilo 40 za pembe za ndovu.
Pamoja na hao, bado majangili wengine wanalindwa na viongozi wa Wizara
ya Maliasili na Utalii. Majangili hao ni Raia wa Ugiriki Pano Canavias na
raia wa Afrika Kusini, John-Martin Venter. Huyu alikamatwa mwaka 2011 na
wenzake wawili, lakini aliachiwa huku magari yao yakiwa na wanyamapori
waliouawa. Kwa mujibu wa jarida la The Hunting Report, Venter anaendelea
kuwinda katika vitalu vya moja wa makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Utekelezaji wa Operesheni Tokomeza ulianza rasmi Oktoba 5, mwaka huu
katika maeneo ambayo yamelemewa kwa matukio ya ujangili. Imegawanyika katika
Kanda nne. Inashirikisha JWTZ, Polisi, Usalama wa Taifa, Mamlaka ya Hifadhi
za Taifa (TANAPA), NCAA, na Idara ya Wanyamapori.
Vituko vya maafisa
Kamati inayoongoza operesheni hii imekutana navituko vya mwaka. Sheria
inawataka askari wanyamapori kurejesha silaha wanazokuwa nazo wakati wa kazi
na kuzisajili katika kitabu maalum, lakini operesheni imebaini kuwa silaha
zote ikiwamo bunduki wanakaa nazo nyumbani kama mali zako kwa saa 24 hata
siku wasizokuwa kazini.
Kilichoisikitisha kamati inayoendelea na operesheni, imebaini kuwa
wengi wa maofisa hao walioshitakiwa walikuwa na tabia ya kukodisha bunduki za
Serikali kwa majangili ambao walikuwa anatumia bunduki na risasi za serikali
kuua tembe wanaopaswa kuwalinda.
“Kilichosikitisha wengi wamekutwa na pembe za ndofu kwenye ofisi zao
na nyumbani kwao, ambazo hazikusajiliwa popote wakati sheria iko wazi kuwa
wakikamata pembe za ndogu wanapima uzito na kusajili kwenye kitabu maalum
kisha zinatunzwa,” kilisema chanzo chetu.
Pia chanzo kingine kilisema kuwa ilikuwa imefikia hatua ambayo maafisa
wanyamapori wakikamata mtuhumiwa ana pembe za ndovu zenye uzito wa kilo 20 au
zaidi, wanauza pembe hizo kisha wanatafuta pembe za tembo wadogo zenye uzito
wa kilo saba au chini ya hapo na kuzihifadhi kama ushahidi wa pembe
zilizokamatwa kumbe pembe halisi ziliishauzwa siku nyingine.
Baadhi ya maofisa wa polisi wasio na biashara ya aina yoyote
wamethibitika kumiliki fedha na majumba makubwa wasiyoweza kuthibitisha iwapo
imetokana na mishahara wanayolipwa.
RCO Arusha atorosha majangili
Uchunguzi unaonyesha kuwa Operesheni hii imewatia mbaroni raia wengi
mno wa ndani na nje ya nchi, lakini mara kadhaa wanaoiendesha wamekumbana na
matukio ya kuingiliwa, ama na watendaji serikalini, au wanasiasa wenye
mamlaka makubwa.
Katika tukio la Arusha, raia wa kigeni wawili kutoka Saudi Arabia
walikamatwa mwanzoni mwa mwezi huu. Raia hao ni Alhassan Alli Auwayship
mwenye hati ya kusafiria namba IC 886898 na Nader Ali Mbooh mwenye hati namba
L 381854.
Walikamatwa Loliondo baada ya taarifa za kiintelejensia wakiwa na kilo
84 za pembe za ndovu na silaha mbili. Hata hivyo, uchunguzi unaonyesha kuwa
waliachiwa kwa amri ya Mkuu wa Upelekezi (RCO) Mkoa wa Arusha wa Arusha,
Duani Nyanda akishirikiana na msaidizi wake kutoka katika Kituo Kikuu cha
Polisi Arusha Mjini, OCD Ngonyani.
Taarifa zinaonyesha kuwa watuhumiwa hao walitakiwa kuachiwa kwa sharti
kuwa wangetoa dola 3,000 (Sh milioni 4.8) kwa kamanda huyo wa polisi ili awaachie
watuhumiwa hao. Dola moja ya Marekani ni shilingi zaidi ya 1,600.
Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI umebaini kuwa baada ya
kuachiwa, hati za kusafiria zilibaki kituoni ila baada ya muda na kwa
maelekezo ya vigogo walirudishiwa na hivyo kuwafanya watoroke.
Walioshiriki kuwawekea dhamana ni Salum Islam Salehe, ambaye ni raia
mwenye asili ya Kiarabu. Kwa mjini Arusha, Salehe anajulikana kwa jina
maarufu la “Kichwa”. Inadaiwa kuwa huyo ndiye aliyefanikisha kutoroka kwa
watuhumiwa hao.
Salehe imebainika kuwa ni wakala wa kupokea wageni kutoka nje ya nchi
na kufanya mipango ya kuwinda. Kazi hiyo ameifanya kwa muda mrefu.
Oktoba 7, mwaka huu Salehe akiwa na wenzake, Shafii Firozi Dalla
(ambaye ana asili ya Kiasia), Gerald Kashiro Joseph ambaye ni Mtanzania,
walikamatwa kwa tuhuma za kujihusisha na uwindaji haramu.
Hata hivyo, mtuhumiwa Salehe hadi jana taarifa zinaonyesha kuwa
alikuwa hajaandikiwa hati ya mashitaka, jambo ambalo lilionekana wazi kuwa
kulipangwa aachiwe bila kuchukuliwa hatua za kisheria.
Watuhumiwa ni wengi mno
Taarifa kutoka ndani ya Operesheni hiyo zinasema kuwa idadi ya
watuhumiwa wanaokamatwa pamoja na zana zao ni kubwa mno.
“Tunakamata bunduki za kivita ambazo hatujawahi kuziona hapa Tanzania
, zina darubini na hiyo inathibitisha kuwa wana uwezo wa kumlenga na kumuua
tembo akiwa mbali kabisa.
“Ukubwa wa janga hili la ujangili unawafanya viongozi wetu wanuie
kuomba waongezwe muda ili kuendelea kutokomeza majangili haya, kama hali hii
ingeachwa, nakuhakikisha ndani ya miaka mitano Tanzania isingekuwa na tembo
wala mnyama yoyote porini,” kimesema chanzo chetu.
Habari ambazo hazijathibitishwa zinasema Amiri Jeshi Mkuu Rais Jakaya
Kikwete ameamua kuongeza muda wa Operesheni hiyo. Hadi sasa Serikali
haijapokea msaada wa kifedha kutoka nje kufadhili operesheni hii. Fedha zote
za operesheni zinatoka Hazina ya Tanzania .
JAMHURI lilikuwa la kwanza kuandika kuanza kwa Operesheni Tokomeza
katika toleo lake namba 104. Hata hivyo, viongozi kadhaa wa Wizara ya
Maliasili na Utalii walikanusha jambo ambalo tayari Rais Kikwete
alishautangazia ulimwengu wakati akiwa Marekani.
Baada ya Operesheni Tokomeza kuzinduliwa, kilichofuata ni kusambazwa
kwa askari katika mapori mbalimbali, wakianza na yale yaliyoandamwa mno na
majangili. Kati ya mapori hayo ni Pori la Akiba la Selous ambalo linajulikana
miongoni mwa majangili kama ‘shamba la bibi.’
Kamati ya Bunge: Tembo wanakwisha
Kamati ya Kudumu ya Bunge imesema ujangili dhidi ya tembo kwa sasa ni
janga la kitaifa.
“Ni ukweli usiofichika kwamba leo hii si tu tembo wanauawa, bali
wanateketezwa. Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Taasisi ya Utafiti wa
Wanyamapori (TAWIRI), taarifa zinazoshabihiana na za utafiti wa kimataifa
zinaonesha kwamba tembo wasiopungua 30 wanauawa kwa siku, tembo 850 wanauawa
kwa mwezi, na tembo 10,000 wanauawa kila mwaka (TAWIRI 2011).
“Kutokana na kasi kubwa ya kuuawa kwa tembo, taarifa za kitaalamu
kutokana TAWIRI zinathibitisha kwamba idadi ya tembo imepungua kutoka 109,000
mwaka 2009 hadi tembo chini ya 70,000 mwaka 2012.
“Endapo kasi hii ya ujangili wa tembo itaendelea bila kudhibitiwa mara
moja, ni wazi kuwa tembo watakuwa wametoweka nchini katika kipindi cha miaka
saba ijayo,” imeonya Kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Kahama, James
Lembeli.
Kamati hiyo imeongeza kusema, “Hali hii ni hatari na aibu kwa nchi
yetu ambayo ni ya pili barani Afrika kwa kuwa na idadi kubwa ya tembo.
Kinachosikitisha ni kwamba Wizara imekuwa na kigugumizi katika kuitikia kauli
ya Rais Jakaya Kikwete iliyoitaka Wizara kuomba msaada kwake kama tatizo la
ujangili limewashinda. Jambo hili linaweza kutafsiriwa kuwa ni hujuma
inayofanywa na baadhi ya watendaji wa Wizara ambao wamepuuza kauli ya
Mheshimiwa Rais.”
Kamati inapendekeza kufanywa kwa Operesheni kama Operesheni Uhai kwa
nchi nzima kama ilivyofanya miaka ya 1980. Pia imependekeza Sheria ya
Wanyamapori Namba 5 ya mwaka 2009 ifanyiwe marekebisho kwa kuweka adhabu kali
kwa watu watakaothibitika kuhusika na ujangili, hasa wa tembo.
CHANZO -gazeti la Jamhuri
|
No comments:
Post a Comment