Thursday, October 31, 2013

chambuzi- Operesheni dhidi ya ujangili iungwe mkono




Na Mwananchi

Posted  Alhamisi,Oktoba31  2013  saa 24:0 AM
Kwa ufupi
Ni kweli, operesheni hiyo inatakiwa isiwe ya mateso, unyanyasaji, ukatili wala fursa ya ulipaji wa visasi, bali inatakiwa kuendeshwa kwa umakini, weledi na haki ili kuhakikisha kila mmoja anatendewa kadri ya matendo yake.
Kwa wiki kadhaa hapa nchini inaendeshwa operesheni ya kupambana na ujangili wa tembo na wanyama wengine chini ya kikosi maalumu kinachoundwa na maofisa kutoka katika vyombo vya dola, maarufu kwa jina la Operesheni Tokomeza.
Taarifa mbalimbali zimekuwa zikiripotiwa kuhusiana na utekelezaji wa majukumu ya kikosi hiki, ikiwamo watu mbalimbali kukamatwa wakidaiwa kuhusika na ujangili, hasa wa meno ya tembo, uhalifu ambao kwa siku za karibuni umeichafua sana nchi yetu kimataifa.
Watu mbalimbali wakiwamo viongozi wa umma na wa kisiasa wamekamatwa katika maeneo ya Serengeti, Ngorongoro, Arusha, Ruaha, Iringa, Mahenge, Maswa, Meatu na kwingineko ambako pia, ushahidi wa aina tofauti umepatikana kuhusiana na vitendo vya ujangili.
Kukamatwa kwa watuhumiwa katika maeneo yote hayo ni ushahidi kwamba majangili wana mtandao mpana unaotumia nguvu za kifedha, kisiasa au za ulinzi wa dola kujiimarisha katika maeneo mengi ya nchi, na kuendelea kuhujumu maliasili za taifa.
Hata hivyo, pamoja na lengo zuri la operesheni hiyo, yapo madai ya kikosi hicho kutumia mabavu na ukiukwaji wa haki za binadamu, ikiwamo kupiga watu ovyo, kujeruhi na hata kuua watu kadhaa wanaotuhumiwa kujihusisha na ujangili.
Pamoja na kwamba malalamiko dhidi ya operesheni hiyo yanatakiwa kushughulikiwa na ukiukwaji huo wa haki za binadamu kukomeshwa, madai hayo yanatakiwa kutazamwa kwa umakini kulingana na unyeti wa tukio na mazingira yake.
Ni kweli, operesheni hiyo inatakiwa isiwe ya mateso, unyanyasaji, ukatili wala fursa ya ulipaji wa visasi, bali inatakiwa kuendeshwa kwa umakini, weledi na haki ili kuhakikisha kila mmoja anatendewa kadri ya matendo yake.
Tunatambua kuwa operesheni yoyote inayowahusisha watu wazito inakuwa na changamoto na vikwazo vingi, hali inayowasukuma hata wabunge kuanza kushinikiza Serikali kutoa orodha ya vigogo wanaodaiwa kujihusisha na vitendo vya ujangili.
Kwa mujibu wa madai ya wabunge hao na taarifa za vyombo vya habari, biashara hiyo haramu inawahusisha baadhi ya wabunge, mawaziri, watumishi wa Serikali na maofisa katika vyombo vya dola.
Jeshi la Polisi limetajwa kuongoza miongoni mwa makundi manne ya majeshi, ambayo watumishi wake wamekamatwa wakijihusisha na ujangili katika matukio saba ya ujangili. Wengine ni kutoka Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na Magereza.
Mathalan, kwa jinsi tatizo hilo lilivyo kubwa, katika matukio ya karibuni yaliyohusisha maofisa wa vyombo vya dola, jumla ya meno ya tembo 686 yaliyotokana na kuuawa kwa tembo 343 yalikamatwa, na vipande vingine 447 vilipatikana.
Kwenye operesheni ya namna hii ambayo Serikali imekiri kuwapo fununu za wanasiasa kuwa miongoni mwa majangili, ni lazima kuwepo vikwazo na shinikizo la kuizuia au kukwamisha, kwa vitisho au malalamiko ya umma kutoka kila kona ili kuhakikisha operesheni husika haifanikiwi.
Kutokana na hali hiyo, tunaunga mkono kauli ya Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha aliyoitia juzi bungeni akiwataka wanasiasa kuacha kushikiza kwa kutumia nguvu zao za kisiasa, kusitishwa kwa operesheni hiyo kwa sababu yoyote, kwa kuwa tunaamini shughuli kama hii haiwezi kufanikiwa iwapo itaendeshwa kama lelemama.

No comments:

Post a Comment