Thursday, October 31, 2013

TAHARIRI-TANZANIA DAIMA -Watawala wanawalinda majangili




JANA vyombo mbalimbali vya habari hapa nchini viliandika kuhusu madai ya wabunge kutaka kuwafichua mapapa wa ujangili.
Madai hayo yaliibuliwa siku ya kwanza ya mkutano wa 13 wa Bunge unaoendelea sasa mjini Dodoma baada ya Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola (CCM), kuituhumu serikali kwa kutoa hoja nyepesi bungeni.
Mbunge huyo alikuwa akitaka kujua hatua iliyofikiwa na serikali kwenye uendeshaji wa Operesheni Tokomeza Ujangili inayofanyika kwenye mbuga zote nchini.
Mbunge alilaani namna operesheni hiyo inavyoendeshwa kwa kukiuka haki za binadamu kwa sababu watu wasio majangili wanakamatwa, kuteswa na kuharibiwa mali zao ilhali majangili wanaojulikana wakiachwa waendelee na uhalifu wao.
Wakati mbunge huyo akilalama, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha, aliwatuhumu wabunge na wanasiasa wengine kwa kuingilia utendaji wa operesheni hiyo kwa kuwatetea wanaokamatwa kwa tuhuma za ujangili.
Kauli ya Waziri Nahodha, ililenga kumpiga kijembe Waziri mwenzie wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, ambaye hivi karibuni, msaidizi wake (ofisi ya ubunge) alikamatwa mkoani Iringa kwa tuhuma za ujangili.
Hoja ya Lugola ni kuitaka serikali kuhakikisha wanakata mizizi ya ujangili kwa kuwa biashara hiyo inafanywa na matajiri wakubwa wenye ushawishi kwa watawala ndani na nje ya nchi.
Tunaunga mkono hoja hiyo kwa maana ya kuitaka serikali kuacha kukamata ‘vidagaa’ wa ujangili huku ‘mapapa’ yakifumbiwa macho.
Tanzania Daima tunafahamu kwamba ujangili, hasa wa tembo na bidhaa zake unatishia ustawi wa wanyama hao.
Takwimu zinaonyesha kwamba kila siku tembo 30 wanauawa kwenye hifadhi mbalimbali nchini. Hiyo ni dalili kwamba katika kipindi cha miaka isiyozidi 10 Tanzania itakuwa na hifadhi zisizo na tembo.
Katika hili tunaitaka serikali kuchukua hatua makini bila kutizamana machoni, licha ya ukweli kwamba utekelezaji wa operesheni hiyo utawaacha wahusika, sababu ni biashara inayofanywa na matajiri wakubwa wenye uswahiba na watawala.
Tunaishangaa serikali kwa kuendelea kuwaacha kazini makamanda wa polisi wanaopakana na hifadhi mbalimbali. Hao lazima wawe watuhumiwa wa kwanza wa ujangili kabla ya kwenda kuwakamata wanavijiji wanaoingia mbugani kutafuta kitoweo.
Mara kadhaa makamanda hao wamehusishwa ama wakiwalinda majangili na kuwavusha mipakani au kwa kutumia magari ya serikali kufanya uwindaji haramu.
Si hivyo tu, makamanda hao wanatuhumiwa pia kuvuruga ushahidi na wakati mwingine kuwatorosha watuhumiwa wa ujangili jambo linalokwamisha utendaji wa mahakimu wanaosikiliza kesi za ujangili.
Kuwakamata makamanda hao inashindikana kwa sababu waliowaweka ndiyo wanaowatuma kuwalinda majangili wanaoua wanyamapori wetu.
Dhamira ya kweli ikiwepo, ikasukumwa na utashi wa kisiasa kisha wananchi wakaelezwa athari za kuua wananyama pori hao, tunaamini mitaji ya mapapa wa ujangili itapungua kwa kiasi kikubwa.

No comments:

Post a Comment