Wednesday, October 30, 2013

ASKARI AKUTWA NA RISASI ,MAPANGA NA NYAMA PORI NYUMBANI



SIKU chache baada ya askari polisi wa idara ya upelelezi wilaya ya Serengeti wakiwa na raia wawili wakishirikiana kuuza jino la tembo,mmoja amekutwa na risasi,nyama mbichi ya pori na mapanga na sime nyumbani kwake.
Askari hao walikamatwa oktoba 25,mwaka huu majira ya usiku na kikosi cha oparesheni okoa maliasili kinachoongozwa na JWTZ baada ya kuweka mtego na kuwanasa kirahisi.
Upekuzi huo uliofanywa nyumbani kwa askari koplo Isaack na Sixbert na kushuhudiwa na maafisa wa polisi walikuta risasi 7 za bunduki aina ya SMG na SRA ,nyama mbichi ya porini kwenye ndoo ya mnyama anayedhaniwa kuwa nyumbu,mapanga 15 na visu 9 nyumbani kwa koplo Isaack.
Licha ya kubainika kuwepo kwa  Rco Mkoa wa Mara Mohammed kwenye upekuzi huo hata hivyo alipoulizwa kwa njia ya simu kushiriki upekuzi na nini kilibainika na inatoa ishara gani kwa idara yake alikana kuwa hakuwepo,”mimi sikuwepo huko Mugumu niko Musoma”alisema.
Alisema kuwa wao hawahusiki na operesheni hiyo,”kila wanachopata taarifa wanapeleka Dar es Salaam…sisi huku kama kuna information  kwa ajili ya kufanyia kazi tunawapa …nao wakituhitaji wanasema …tunashirikiana kwa karibu
Kukamatwa kwa vitu hivyo  kwa askari huyo kumezidi kuibua maswali na hofu kutoka kwa raia huku ikitiliwa shaka kuwa mtandao huo ni mkubwa na huenda wakawa na silaha maalum inayotumiwa kwa ajili ya uwindaji wa wanyama pori  na matukio mengine.
Kamanda wa polisi Mkoa wa Mara Fernandi Mtui akiongea na Mwananchi kwa njia ya simu kuhusiana na upekuzi huo alikiri ulifanyika lakini hakushiriki katika zoezi hilo kwa kuwa operesheni hiyo inaundwa na askari mchanganyiko na wanakuwa na hati maalum za upekuzi.
“Ni kweli upekuzi umefanyika lakini sikuhusika…sijajua kwa undani nini kimekamatwa…maana kikosi hicho wapo askari wa kwetu,usalama wa taifa,wanyamapori na JWTZ na wana searc warrant(Hati ya upekuzi)…mimi nasubiri kama wamekutwa na kosa wataletwa kwangu”alisema kamanda.
Kamanda Mtui alisema kwa kuwa si msemaji wa operesheni hiyo bado anasubiri taarifa ya uchunguzi na kama watabainika kuwa na tuhuma watashitakiwa kijeshi kabla ya kushitakiwa kiraia,”hapo ndipo nitakuwa na nafasi ya kulizungumzia hilo…nasema kila kitu kitawekwa wazi…sitawanyima taarifa.
Oktoba  25 majira kati ya saa 4-5 usiku  mwaka huu askari wawili waliotajwa kwa  jina moja moja la Koplo Isaack na Sixbert wa idara ya upelelezi walikamatwa wakiwa na raia mmoja Samweli Chacha walikamatwa  wakijaribu kuuza jino la tembo katika eneo la Sedeco mjini Mugumu baada ya kuweka mtego maalum.
Askari hao wakiwa na gari aina ya Toyota Corolla yenye namba za usajiri T269 BRN mali ya askari Sixbert walifika eneo hilo na jino hilo kwa ajili ya kuuza wakiwa na raia wawili  mmoja anadaiwa kutoroka baada ya wenzao kukamatwa.
Baada ya kukamatwa kwa askari hao  walichukuliwa na kupelekwa eneo la Andajenga lililomo ndani ya hifadhi ya Taifa ya Serengeti ambako kikosi hicho kina kambi maalum.


No comments:

Post a Comment