Tanapa
kuchunguza tuhuma za ujangili
Na Daniel Mjema na Ibrahim
Yamola, Mwananchi
Kwa ufupi
Kwa ufupi
- Shelutete
alisema kutokana na majangili kubuni mbinu mpya kila siku, shirika
limeunda kikosi maalumu (Rapid Response Team) kwa ajili ya
kukabiliana na uhalifu kwa haraka zaidi.
Arusha/Dar es Salaam. Shirika la Hifadhi za Taifa nchini
(Tanapa), limeanzisha uchunguzi dhidi ya baadhi ya watumishi wake wanaotajwa
kuwapo katika mitandao ya ujangili wa wanyama wakiwamo tembo.
Meneja Uhusiano wa Tanapa, Paschal
Shelutete aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa, wale watakaothibitika
kujihusisha na vitendo hivyo watachukuliwa hatua za kinidhamu na kisheria.
“Tumepokea tuhuma dhidi ya baadhi ya
watumishi wetu kujihusisha na mitandao ya ujangili na uchunguzi dhidi yao umeanza
ukishirikisha vyombo vya kiuchunguzi,” alisema Shelutete.
Shelutete alisema, tatizo la ujangili
ni la kimtandao ukishirikisha majangili wa kimataifa wanaotumia ushawishi wa
fedha na silaha za kisasa katika kuua tembo kwa lengo la kujipatia vipusa. “Wapo
watumishi wamejikuta wakishawishiwa kujiunga na mitandao ya ujangili jambo
ambalo ni kinyume kabisa na maadili ya kazi na hawa wakibainika kwa kweli
hatuna msalie mtume,” alisema.
Shelutete alisema kutokana na
majangili kubuni mbinu mpya kila siku, shirika limeunda kikosi maalum (Rapid Response Team) kwa ajili ya kukabiliana na uhalifu kwa haraka
zaidi.
Alisema uanzishwaji wa kikosi hiki
umeonyesha mafanikio makubwa na kutoa mfano katika kipindi cha miezi sita
iliyopita hakuna tembo aliyeuawa ndani ya Hifadhi za Manyara na Tarangire.
Shelutete alisema kwa miezi sita,
majangili 1,116 walikamatwa katika hifadhi mbalimbali huku Hifadhi ya Taifa ya
Serengeti (Senapa) pekee ikikamata majangili 248.
Akizungumza katika maadhimisho ya
Siku ya Tembo nchini yaliyoandaliwa na UDSM kitengo cha Taasisi ya Kutathimini
Rasilimali, Profesa Alexander Songorwa alisema wananchi ni wadau muhimu katika
kampeni ya kupambana na ujangili.
No comments:
Post a Comment