HIFADHI ZA TAIFA TANZANIA
TAARIFA KWA UMMA
TANAPA KUENDESHA MAFUNZO MAALUM KWA ASKARI WAKE
Jumla ya Askari mia moja (100)
waliofuzu usaili wa awali wa ajira ya uaskari wanatarajiwa kuanza rasmi mafunzo
maalum ya mbinu za medani kwa miezi mitatu katika Hifadhi ya Taifa ya Katavi
kuanzia Oktoba Mosi mwaka huu.
Askari watakaofuzu vema mafunzo
hayo ndio watakaoajiriwa na shirika katika utaratibu mpya ulioanzishwa na
shirika wa kuandaa mafunzo hayo kwa askari hawa waliopitia mafunzo ya uaskari
katika Jeshi la Kujenga Taifa na Chuo cha Wanyamapori Pasiansi Mwanza.
Aidha, shirika linaendelea
kuchunguza na kuchukua hatua za kinidhamu na kisheria kwa wafanyakazi
wanaobainika kujihusisha na vitendo vya ujangili kwa kushirikisha vyombo vya
dola. Uchunguzi bado unaendelea kufanyika kwa baadhi ya wafanyakazi na
utakapopatikana ushahidi wa kisheria kwa wote wanaojihusisha na mitandao ya
ujangili hatua kali za kinidhamu na kisheria zitachukuliwa.
Mafanikio kadhaa yameweza
kufikiwa na shirika katika kukabili ujangili ambapo uimarishwaji wa doria za
magari na miguu pamoja na matumizi ya mbwa katika hifadhi nchini umepunguza kwa
kiwango kikubwa vitendo hivi ambapo katika kipindi cha miezi sita iliyopita
ujangili uliokuwa umeshika kasi katika Hifadhi za Tarangire na Ziwa Manyara
uliweza kudhibitiwa kwa asilimia 100 ambapo hakuna tembo aliyeuawa ndani ya
hifadhi hizo tangu
mwezi Februari hadi leo.
Vile vile, Shirika
limeanzisha Kikosi Maalum cha Kupambana na Ujangili na matukio ya dharura
(Rapid Response Team). Kikundi hiki kina Askari 40 ambao wamepewa mafunzo
maalumu ya ujasiri na ukakamavu wa hali ya juu kwa ajili ya kukabiliana na
vitendo vya ujangili katika kipindi cha miezi sita iliyopita ambapo mafunzo
hayo yalifanyika katika Hifadhi ya Ruaha.
Mafanikio mengine
yaliyoweza kufikiwa na shirika katika muda wa miezi sita iliyopita ni pamoja na
i.
Ukamataji
wa majangili 1,116 katika hifadhi kwa kipindi cha Aprili –Juni 2013. Hifadhi ya
Serengeti pekee iliweza kukamata majangili 248.
ii.
Katika
kipindi cha Aprili-Juni 2013, Askari wetu waliweza kukamata silaha za moto 85
toka kwa majangili. Silaha hizo ni pamoja na Civilian Rifle (7), muzzle
loaders/magobore 60 Automatic Rifle (5) na shortgun 13. Aidha, silaha za kienyeji zipatazo 795
zilikamatwa na pia kufungua waya zinazotumika kutega wanyama 25,422.
iii.
Askari
wa hifadhi waliweza kukamata mbao 2,245 na nguzo 1030 kwa kipindi hicho katika
hifadhi zake.
iv.
Askari
waliweza pia kukamata mifugo (ng’ombe) 6,650 waliokuwa wakichungwa ndani ya
hifadhi bila vibali. Wenye mifugo hiyo walitozwa faini stahili.
Kwa
ujumla hali ya ujangili ndani ya maeneo ya hifadhi imedhibitiwa kwa kiwango
kikubwa ambapo kama tulivyosema awali shirika litaendelea kuchukua hatua za
kinidhamu mara moja pale itakapobainika kuhusika kwa watumishi wake katika
vitendo hivi kama ambavyo limeshachukua hatua za kufukuza kazi na kuandika
barua za onyo kali kwa baadhi ya maafisa wake..
Mwisho, katika siku za usoni
shirika linatarajia kubadili mfumo wake wa utendaji kazi kutoka ule wa kiraia
na kuwa mfumo wa kamili wa kijeshi (paramilitary system) kwa watumishi wote ili
kuweza kukabili kwa umakini janga la ujangili nchini.
Imetolewa
na Idara ya Uhusiano
HIFADHI
ZA TAIFA TANZANIA
22.09.2013
No comments:
Post a Comment