Taarifa za kiitelijensia
zinavyookoa tembo
Kwa ufupi
- 419 Idadi ya tembo waliouawa
katika hifadhi mbalimbali nchini.
- 1,645Mbao zilizokamatwa baada ya kuibwa katika hifadhi nchini
- Habari hii imeandikwa na Daniel Mjema-Moshi.
Kinapa
inatakiwa kutoaelimu zaidi ya ujasiriamali kwa jamii ili kuwapa uwezo wa
kuanzisha miradi.
Hifadhi
ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro (Kinapa) ni moja ya hifadhi 16 nchini ambayo
imefanikiwa kudhibiti vitendo vya ujangili wa tembo ambao wamekuwa wakiuawa na
wahalifu wanaotafuta vipusa.
Takwimu
zilizotolewa na Mhifadhi Mkuu wa Shirika la Hifadhi za Taifa nchini (Tanapa),
Mtango Mtahiko zinaonyesha kati ya 2009 hadi 2012, wanyamapori 15,227 waliuawa
ndani ya hifadhi hizo.
Kati ya
wanyamapori hao, 419 ni tembo waliouawa katika hifadhi mbalimbali huku hifadhi
ya Ruaha ikiongoza kwa tembo 131 kuuawa ikifuatiwa na Serengeti 92, Tarangire
53, Katavi 36 na Mikumi 30.
Mkuu wa
Idara ya Ulinzi na Uokoaji Kinapa, Sebastian Gambares anasema ujangili wa tembo
umepungua kwani mwaka 2012/2013 hakukuwa na tukio la kuuawa kwa tembo ndani ya
hifadhi hiyo.
“Hata
matukio ya nyuma ya kuuawa kwa tembo yalihusisha matukio ya kuuawa nje ya
hifadhi, Kinapa tumekuwa makini sana katika kudhibiti Majangili,”anabainisha
mhifadhi huyo.
Anasema
wanapobaini kuwapo kwa tembo katika eneo fulani hasa tembo wanaotoka Hifadhi ya
Amboseli nchini Kenya, basi kikosi cha kupambana na ujangili kinakuwapo karibu
na maeneo hayo.
Naye Mkuu
wa Hifadhi ya Kinapa, Kanda ya Kaskazini Magharibi, Imani Kikoti anasema moja
ya mikakati iliyosaidia udhibiti wa ujangili ni kubadilishana taarifa za
kiitelejensia kwenye maeneo ya mipakani.
Kikoti
anasema Kinapa imeamua kudhibiti ujangili wa tembo kwa kuwa wanaweza kutoweka
kama udhibiti makini hautakuwapo katika maeneo waliopo.
Kwa
mujibu wa Kikoti, katika kipindi cha 2009 hadi 2012, idadi ya majangili
wanaokamatwa imekuwa ikipungua kutoka 320 mwaka 2009 hadi majangili 278 mwaka
2012/2013.
Anasema
mikakati ya kukabiliana na ujangili inahusisha pia ujangili wa mazao ya misitu,
kuwasha moto kwenye hifadhi na uingizaji mifugo kwenye maeneo ya hifadhi kwa
uharibifu huo unaathiri vyanzo vya maji.
Kikoti
anasema kushuka kwa idadi ya mbao na nguzo zinazokamatwa ni dalili tosha kwamba
vitendo vya ujangili wa mazao ya misitu ndani ya hifadhi vimekuwa vikidhibitiwa
kwa kiasi kikubwa.
Mathalani,
mwaka 2009/2010 mbao zilizokamatwa zilikuwa 1,645 na nguzo 229, lakini mwaka
2012/2013 idadi hiyo ilishuka hadi mbao 636 na nguzo 198.
“Mlima
Kilimanjaro ni chanzo muhimu cha maji kwa hiyo mifugo ikikanyaga maeneo hayo
vyanzo hivyo vinakauka na kuathiri mikoa mbalimbali inayotegemea vyanzo
hivi,”anabainisha Kikoti.
Mkuu wa
Idara ya Ujirani mwema ya Kinapa, Theodora Aloyce, anasema kipindi cha
2007/2008 hadi 2012/2013, Kinapa imefadhili miradi ya wananchi yenye thamani ya
sh1.29 bilioni ikiwamo ujenzi wa madarasa na madawati.
Miradi
hiyo imetekelezwa katika wilaya tano zinazozunguka mlima huo ambazo ni Hai,
Siha, Rombo, Moshi na Longido.
Theodora
anasema miradi mingine iliyofadhiliwa na Kinapa kwa kuchangia asilimia 70 huku
wananchi wakichangia asilimia 30 ni ujenzi wa shule za walimu, hosteli za
wanafunzi, maabara na miradi ya maji.
Theodora
anasema katika miaka ya karibuni, kumekuwapo na vikundi kadhaa vinavyoendesha
miradi ya kihifadhi kama kuanzishwa kwa vitalu vya miti ya asili na kufuga
Nyuki.
Moja ya
shule zinazonufaika ni amabazo ziko jirani na Mlima Kilimanjaro ni Shule ya
Sekondari, Uru Kishumundu, Wilaya ya Moshi vijijini ambayo Kinapa
imefadhili ujenzi wa bweni la wanafunzi wa kike.“Tuishukuru sana Kinapa kwa kwa
kutujengea jengo la ghorofa tatu,”anasema Philip Nzao ambaye ni Makamu Mkuu wa
shule.
No comments:
Post a Comment