Sunday, September 15, 2013

HOTUBA YA NAIBU WAZIRI







HOTUBA YA MHE. LAZARO NYALANDU, NAIBU WAZIRI WA MALIASI NA UTALII KATIKA MAPOKEZI YA MATEMBEZI YA HIARI YALIYOANDALIWA NA ‘AFRICAN WILDLIFE TRUST’ TAREHE 12/09/2013 ENEO LA MNAZI MMOJA, DAR ES SALAAM

• Bw. Patric Patel, Mkurugenzi, African Wildlife Trust
• Washiriki wa Matembezi,
• Wageni waalikwa,
• Mabibi na Mabwana,

Kwa niaba ya Wizara ya Maliasili na Utalii na kwa niaba yangu mwenyewe, ninapenda kuwapa pole ninyi nyote mliotembea kwa hiyari yenu kutoka Arusha hadi hapa Dar es Salaam. Aidha, ninawapongeza African Wildlife Trust kwa kubuni matembezi haya ambayo yamebeba ujumbe mkubwa kuhusu kupiga vita ujangili nchini. Ninawapongeza pia wageni mliofika kwenye halfa hii ya kupokea matembezi haya.

Ndugu Wananchi,
Matembezi haya ya kupiga vita ujangili nchini yamefanyika wakati ambapo kuna ongezeko kubwa la ujangili, nchini hususan ujangili wa tembo. Ujangili huu unasababishwa na mambo kadhaa ikiwa ni pamoja na:
1. Kuongezeka kwa bei ya meno ya tembo katika masoko haramu huko Mashariki ya Kati na Asia;
2. Kuimarika na kuongezeka kwa magenge ya ujangili (poaching syndicates) pamoja na ubora wa mawasiliano;
3. Kudorora kwa uchumi na kuongezeka kwa umasikini katika jamii, hivyo kufanya watu wengi kujiingiza kwenye ujangili cha uhalifu mwingine;
4. Uroho wa kutaka utajiri wa haraka haraka ambao umewafanya baadhi ya wafanyabiashara wakubwa na wadogo na watumishi wa umma kujiingiza katika ujangili; na
5. Rushwa na mmomonyoko wa maadili katika jamii kwa jumla.

Ujangili umechangia sana katika kupungua idadi ya tembo nchini kutoka 350,000 miaka ya 1960 hadi 110,000 mwaka 2009. Idadi ya tembo wanaouawa na majangili inazidi kuongezeka kila mwaka. Kwa mfano, kwa kipindi cha miaka mitatu (2010 – 2012) tembo waliouawa na majangili ni kama ifuatavyo:
Mwaka 2010 - 259
Mwaka 2011 - 276
Mwaka 2012 - 473
Kati ya Januari na Julai 2013 tembo 378 pia walikuwa wameuawa na majangili.

Ndugu Wananchi,
Serikali, kupitia Wizara ya Maliasi na Utalii, imekuwa ikipambana na majangili hawa ndani na nje ya hifadhi za taifa. Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, (2010 – 2012) jumla ya majangili 4,066 walikamatwa na bunduki 1,899 kukamatwa na kutaifishwa. Serikali inaendelea na mikakati na mbinu mbalimbali za kukabiliana na majangili.

Serikali inajenga uwezo wa kukabiliana na majangili porini na matajiri waliopo mijin,i ambao wanafadhili ujangili. Baadhi ya wafanyabiashara wanasiasa na watumishi wa umma wanajihusisha na ujangili. Ninatoa wito na onyo kwao kwamba waache kabisa uovu huu, vinginevyo watajikuta wamenaswa na vyombo vya dola ambapo, mbali na kufikishwa mahakamani, watatangazwa kwenye vyombo vya habari ili umma na wananchi wote Tanzania wajue watu wanaohuJumu rasilimali zao. Dawa ya majangili imekwishachemshwa na inapelekwa mezani wakati wowote. Ole wake atakayenyweshwa na dawa hiyo.

Ndugu Wananchi,
Ninatoa wito kwa wananchi wote waendelee kushirikiana na serikali kupiga vita ujangili kwa kuwafichua majangili popote wanapowaona. Aidha, taasisi zote za umma zishirikiane kupambana na ujangili ili kuutokomeza kabisa.

Serikali itaendelea kushirikiana na taasisi na mashirika ya kimataifa katika kuukabili ujangili unaovuka mipaka. Wakati huo huo serikali itajengea watumishi wa sekta ya wanyamapori uwezo wa kuutokomeza ujangili.

Ni matumaini yangu kuwa Africa Wildlife Trust haitaishia kwenye matembezi haya bali itaendelea na juhudi nyingine za kupambana na ujangili ikiwa ni pamoja na kutoa fedha na vifaa kwa Sekta ya Wanyamapori ili kuunga mkono kikamilifu juhudi za serikali katika mapambano haya.

Ningependa kuona kwamba kwa kipindi cha muda mfupi ujao, ‘African Wildlife Trust’ inaandaa hafla ya kukabidhi vifaa na/au fedha za kusaidia kupambana na ujangili. Vivyo hivyo, ninatoa wito na changamoto kwa Kampuni za umma na binafsi pamoja na mtu mmoja mmoja kutoa fedha na vifaa kwa ajili ya kuzuia ujangili nchi nzima.

PICHANI:

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Lazaro Nyalandu (Mb) (watano kutoka kushoto msitari wa mbele) akiwa anandamana pamoja na waandamanaji wanaopinga ujangili wa tembo ‘Tembea kwa ajili ya Tembo’ mara baada ya kuwapokea leo, Ubungo jijini Dar es Salaam asubuhi. Maandamano hayo yamechukua muda wa siku 19 na waandamanaji wametembea kilomita 650, kutoka Jijini Arusha.

No comments:

Post a Comment