Ofisa Mhifadhi Wanyamapori atupwa jela miaka mitatu.
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
Mahakama ya Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam,
imemhukumu Ofisa Mhifadhi Wanyamapori wa Wizara ya Maliasili na Utalii,
Richard Nchasi, kulipa faini ya Sh. 900,000 au kwenda jela miaka mitatu
baada ya kukutwa na makosa matatu.
Hukumu hiyo ilisomwa na Hakimu Mkazi, Juma Hassan, juzi baada ya
kupitia ushahidi uliotolewa na upande wa Jamhuri na kumtia mshtakiwa
hatiani kwa makosa hayo matatu.
"Kati ya makosa manne, mahakama imemtia hatiani mshtakiwa kwa
makosa matatu ya kutumia nyaraka kwa lengo la kumdanganya mwajiri kwa
kutoa hati za uwindaji wa wanyama," alisema Hakimu Hassan.
Hata hivyo, mahakama hiyo ilisema upande wa Jamhuri umeshindwa
kuthibitisha shitaka la kuisababishia wizara hiyo hasara ya Dola 1,860
za Marekani (sawa na Sh. 2,976,000).
Awali, Mwendesha Mashitaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na
Rushwa (Takukuru), Leonard Swai, alidai kuwa katika tarehe tofauti kati
ya Januari na Septemba, 2008, katika ofisi za wizara hiyo, jijini Dar es
Salaam, mshtakiwa akiwa na wadhifa huo, aliandaa hati yenye namba
01235414 ya Agosti Mosi, 2008.
Inadaiwa kuwa hati hiyo ilikuwa ikionyesha kwamba Safari Club (T)
Ltd, inatakiwa kulipa Dola 5,080 za Marekani (sawa na zaidi ya Sh.
milioni 8.5) ikiwa ni ada ya uwindaji wa wanyama sita katika eneo la
Kilwa South Mbemkulu, huku akijua si kweli.
Nchasi anadaiwa kuwa katika kipindi hicho, aliandaa tena hati yenye
namba 01235410 ya Februari 21 mwaka 2008, kuonyesha kwamba kampuni hiyo
inatakiwa kulipa ada ya Dola 6,580 (sawa na zaidi ya Sh. milioni 11) ya
uwindaji wa wanyama watano katika eneo hilo.
Ofisa Mhifadhi huyo anadaiwa katika kipindi hicho, aliandaa tena
hati yenye namba 01235415 ya Agosti Mosi, 2008, kuonyesha kampuni hiyo
inatakiwa kulipa Dola 6,335 (sawa na zaidi ya Sh. milioni 10.6) ikiwa ni
ada ya uwindaji ya wanyama saba kwenye eneo hilo.
Katika shitaka la nne, Nchasi anadaiwa katika kipindi hicho, jijini
Dar es Salaam, akiwa mwajiriwa wa wizara hiyo, kwa kuelewa na kwa
uzembe, aliisababishia wizara hiyo hasara ya Dola 1,860 (sawa na zaidi
ya Sh. milioni 2.9) .
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment