Posted by Williammalecela.com on Thursday, August 06, 2015
|
Wizara ya Maliasili na Utalii imepokea taarifa kupitia Vyombo vya Habari
inayohusu kukamatwa kwa nyara zinazojumuisha meno ya tembo yenye uzito
wa kilo 262, kucha na meno ya simba vyenye uzito wa kilo moja(1). Tukio
la kukamatwa kwa nyara hizo limetokea kwenye uwanja wa ndege wa Zurich
nchini Uswisi tarehe 06 Julai, 2015. Kwa mujibu wa taarifa hizo, nyara
hizo zilipatikana ndani ya masanduku manane (8) zikiwa njiani kwenda
Beijing-China kutokea uwanja wa ndege wa Dar es Salaam kupitia Zurich.
Wizara inachukua nafasi hii kupongeza Uongozi wa uwanja wa ndege
wa Zurich, na Serikali ya Uswisi na wote walioshiriki kubaini na
kukamata nyara hizo. Wizara imepokea kwa masikitiko makubwa taarifa hizi
na kwamba nyara hizo zimesafirishwa kupitia uwanja wa ndege wa JN Dar
es Salaam. Tukio hili linadhihirisha kuwa tatizo la ujangili bado
linaendelea ndani na nje ya nchi yetu licha ya jitihada nyingi
zinazofanywa na Serikali kwa kushirikiana na Jumuiya za Kimataifa.
Wizara inapenda kuuhakikishia umma kuwa sisi kama nchi tunafanya na
kutumia jitihada zote kupambana na vitendo vya ujangili unaotishia
kutoweka kwa rasilimali za wanyamapori wetu.
Baada ya kupokea taarifa hizo, Wizara imeanza kufanya uchunguzi kwa
kushirikisha mamlaka husika ikiwemo Mamlaka ya Viwanja vya ndege (TAA)
pamoja na vyombo vya Ulinzi na Usalama ili kuchukua hatua stahiki ikiwa
ni pamoja kuwabaini wote waliohusika na kadhia hii. Wizara inapenda
kutoa wito kwa yeyote mwenye taarifa zinazoweza kusaidia kufanya
uchunguzi huu aziwasilishe kwenye mamlaka za Ulinzi na Usalama.
Imetolewa na
Lazaro S. Nyalandu
Waziri wa Maliasili na Utalii. |
No comments:
Post a Comment